Sikio la kufa halikumsikia RC Albert John Chalamila

13Jun 2021
Thobias Mwanakatwe
Nipashe Jumapili
SIASA
Sikio la kufa halikumsikia RC Albert John Chalamila

​​​​​​​JUNI 10, 2021 itabaki kuwa historia kwa aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila, kutokana na kuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kutumbuliwa na Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan.

Albert Chalamila.

Chalamila amemaliza takribani siku 17 tangu alipoteuliwa na Rais Samia Mei 15, 2021 kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akitokea Mkoa wa Mbeya ambao alihudumu huko kwa miaka kadhaa.

Kimsingi, ni mtendaji mzuri lakini tatizo kubwa alilonalo ni kauli zake kwa kuwa hajui kuchunga ulimi wake. Hajui jambo hili aliongelee mahali gani na inawezekana hilo ndilo limemponza japo siri ya kutenguliwa kwake itabaki kwa aliyemteua.

Kutenguliwa huko kwa Chalamila, kumeonyesha mawazo halisi namna watu walivyokuwa wanamtazama kijana huyo mzaliwa wa Mkoa wa Iringa.

Kiburi cha Chalamila kilianzia siku ambayo Hayati Dk. John Magufuli, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa ametua kwenye ziara mkoani Mbeya.

Nakumbuka Dk. Magufuli aliwaambia wananchi katika uwanja wa Ruanda Nzovwe kuwa licha ya kujua kuwa hawamtaki Chalamila ataendelea kumwacha pale pale na akafanya hivyo.

Duru za siasa zinaeleza kuwa kwa ukaribu wa Chalamila na Hayati Dk. Magufuli hata baadhi ya wajumbe wa kamati nyeti za Mkoa wa Mbeya ikiwemo Kamati ya Siasa ya CCM mkoani humo walikuwa wakimwogopa badala ya kumheshimu.

Hali hiyo ikamfanya Chalamila kuwa mpweke kwa kuendelea kusifiwa huku 'wakimg'ong'a' au kumzodoa huku yeye akidhani anakubalika kumbe wanammaliza kiaina.

 

Na kimsingi alichokifanya Rais Samia ni mabadiliko sahihi yanayoenda kuboresha utendaji wa kazi ndani ya mikoa yao na serikalini kwa ujumla.

Chalamila mara kadhaa amekuwa mtu wa kutoa kauli mbalimbali ambazo kwa lugha nyepesi unaweza kumwita mropokaji. Kwa nafasi yake kama mkuu wa mkoa si busara sana kuwa mropokaji.

Ninachoweza kusema Chalamila siku nyingi sana alikosa maadili ya kiutumishi ndiyo maana ilikuwa kila anapozungumza lazima aibue jambo jipya na la kushangaza.

Alijisahau kuwa maadili ni viwango vya uadilifu vinavyotazamiwa na wananchi kwa mtumishi yeyote wa umma. Maadili huwekwa kwa njia ya Misingi, Kanuni, na Miongozo inayotakiwa katika Utumishi.

Kwa hiyo mwenendo wa kila mtumishi wa umma hutazamiwa na wananchi kufuata kanuni, misingi na miongozo hiyo. Kanuni na misingi hiyo huwekwa kwa kuzingatia utu, dhamira safi, maslahi ya walio wengi, ubora na utamaduni wao. Maadili huzuia matumizi mabaya ya madaraka au dhamana.

Maadili huiwezesha serikali na taasisi zake kufanya kazi kwa kuaminiana na kutegemeana na pengine pasipo kuingiliana. Kwa hiyo, maadili hutumika kupima ubora wa huduma au dhamana iliyotolewa na waliokabidhiwa. Chalamila kama angeyajua yote haya mapema yasingemtokea yaliyomtokea.

Nakumbuka siku moja alipofanya ziara katika wilaya ya Kyela ambako wananchi walikuwa wamekumbwa na mafuriko.

Maneno aliyowaambia wale waathirika wa mafuriko hayakuwa mazuri kiukweli na wananchi wale walibaki kunung'unika maana hawakuamini mtu mwenye hadhi ya RC anaweza kutoa maneno ya ajabu kama yale.

Katika kuonyesha Chalamila hakupendwa na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mbeya, siku Rais Samia anamhamisha Mbeya na kumpeleka Mwanza, kinamama wajasiriamali wa eneo la SIDO, walifanya sherehe kufurahia kuhamishwa kwake.

Kimsingi, viko vituko vingi ambavyo vimefanywa na Chalamila katika utumishi wake ambavyo havikuwafurahisha wananchi na hata viongozi wenzake wa serikali.

Juni 2, mwaka huu, wakati Rais Samia akizungumza na viongozi wateule baada ya kuwaapisha, Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma, alisema Chalamila ni petroli na kueleza kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike, yeye ni kiberiti kwa sababu ni mkimya lakini ana mambo yake katika utendaji.

Chalamila, kwa mtazamo wake aliona kuelezwa hivyo ni kama amepewa sifa, badala ya kujitafakari basi akaendelea kulipuka hata mambo ambayo hayana msingi.

Kimsingi nimalizie kwa kusema Chalamila lilikuwa ni sikio la kufa ambalo halikusikia dawa.