Sikio la kufa halisikii dawa

13Feb 2018
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Sikio la kufa halisikii dawa

“ASIYEJUA maana haambiwi maana.” Hapana haja ya kujisumbua kumweleza mtu asiyejua faida ya jambo.

Methali hii yaweza kutumiwa kumpigia mfano mtu anayejisumbua au kujipa taabu ama unayemweleza faida za jambo linalomhusu lakini anapuuza.

Safu hii ya ‘Tujifunze Kiswahili’ imekuwa ikikosoa maneno yanayotumiwa vibaya kwenye vyombo vya habari, hasa magazeti ya Kiswahili. Lengo la safu hii ni kufafanua maana ya maneno ya Kiswahili na matumizi yake.

Hata hivyo yaleyale ninayoyatolea ufafanuzi ndio yatumiwayo na waandishi kwa namna wanayojua wao, mradi magazeti yanunuliwe! Yaelekea wahariri, waandishi na wanaodurusu lao moja … hela kwanza, ufasaha wa Kiswahili baadaye!

“Juzi Jumamosi ndio ilikuwa balaa zaidi kwani kuanzia saa moja za asubuhi mashabiki kutoka mjini Iringa na mikoa jirani ya Mbeya, Njombe walianza kumiminika kwenye Uwanja wa Samora wakinunua tiketi na wengine wakitumia fursa hiyo kuuza jezi.”

Sentensi hii yenye maneno 37 yaeleza jinsi watazamaji walivyokuwa na shauku ya kuuona mchezo wa jioni ile kati ya Lipuli na Yanga, hususan wachezaji wa Yanga ambao hawajaonekana Iringa kwa muda mrefu.

Haieleweki mwandishi alikuwa na sababu gani kuandika “ … Jumamosi ndio ilikuwa balaa zaidi …” Ni kama huko nyuma kulikuwa na balaa ila Jumamosi aliyoizungumzia, balaa ilizidi.

Kadhalika kichwa kidogo cha habari kiliandikwa: “Mchana balaa zaidi … licha ya mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishuhudia mechi hiyo, lakini bado wengine walilazimika kuzuiwa kuingia uwanjani hapo kutokana na uwanja huo kujaa na kukosa sehemu ya kukaa mashabiki …”

Maana ya ‘balaa’ au ‘baa’ ni janga lililoenea katika jamii au kwa mtu binafsi; beluwa.

Kuna sehemu imeandikwa hivi: “Hata hivyo, kipindi cha pili kilionekana kuwa na matukio kadhaa kwa wachezaji kupewa kadi za njano ambapo wachezaji wa Lipuli Adam Salamba alimzawadia kadi ya njano.

He! Kumbe kadi za onyo hutolewa zawadi kwa wachezaji wanaocheza rafu eh! 

“Huko mitaani tambo mbalimbali za mashabiki huku mastaa kama Papy Kabamba Tshishimbi, Ibrahim Ajibu, Obrey Chirwa wakiwa gumzo na kuwapa mzuka waliotaka kuwaona uwanjani baada ya kuwachungulia tu kwenye runinga.”

Sielewi kwa nini waandishi wa michezo hupenda sana kutumia neno ‘mzuka’ katika habari/makala zao. ‘Mzuka’ ni kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa  kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo. Kwa nini wanadamu wafananishwe na pepo?

“… waliotaka kuwaona uwanjani baada ya kuwachungulia tu kwenye runinga.” Jamani! Kuwachungulia au kuwaona? ‘Chungulia’ ni kitendo cha kuangalia kupitia uwazi mdogo au nafasi nyembamba; kitendo cha mtu au mnyama kutazama kwa kujificha.

Nimenukuu na kutolea ufafanuzi maneno yote yaliyotumiwa na mwandishi mmoja tu ili muone jinsi Kiswahili kinavyotushinda!

“Makuukuu ya tai si mapya ya kengewa*.” Mambo anayoyafahamu tai hayawi mapya kwa kengewa ambaye ni aina ya mwewe. Wote wamo katika jamii moja; kwa hiyo haikosi anayoyafahamu tai kengewa anayaelewa.

*Kengewa ni ndege aina ya mwewe lakini mdogo anayekula kuku.

Methali hii huweza kutumiwa kumpigia mfano mtu ambaye ameishia kuzifahamu siri na kunga za mwenzake mwenye uwezo kiasi cha kuwa hashtushwi na matendo yake. Huweza pia kutumiwa kuelezea hali au tabia ya vijana inavyoweza kutofautiana na ya wazee.

‘Pa’ maana yake ni kitendo cha mtu kutoa kitu kwenda kwa mwingine. ‘Zawadi’ ni tunu anayopewa mtu kuonesha ishara ya kuridhika na jambo alilofanya.

Sasa tujiulize: Wachezaji wanapofanya makosa uwanjani ‘hupewa’, ‘huzawadiwa’ au huoneshwa kadi na kuonywa? Maana ‘wakipewa’ au ‘kuzawadiwa’,  mwamuzi hatokuwa na kadi ya ziada kuwaadhibu wachezaji wengine watakaofanya makosa!

Waandishi wasitumie maneno wasiyojua maana yake kama huyu aliyeandika: “Kwa namna Yanga ilivyopambana jihad Samora kwa hakika walistahili kutoka ushindi huo wa kwanza mjini humo baada ya miaka mingi …”

‘Jihadi’ (mwandishi kaandika ‘jihad’) ni hali ya mtu kujitolea kwa nafsi yake au mali yake katika kutekeleza au kueneza maamrisho ya Mwenyezi Mungu; vita vitakatifu vinavyopiganwa na waislamu.

Kuthibitisha jambo hili, hebu soma alivyoandika mwandishi:

“Mwanjala alisema katika makisio yao ilikuwa waingize mashabiki 10,000 uwanjani lakini hali ilikuwa tofauti watu walizidi mara madufu.”

‘Madufu’ ni wingi wa ‘dufu’ (nomino) na maana yake ni kifaa kidogo chenye umbo la duara kilichoambwa upande mmoja na hupigwa kwenye maulidi. Maana ya pili ya ‘dufu’ ni –enye ufahamu mdogo.

Mithali: Wanosha miti minazi kifa ngaa.

[email protected]

0715 334 096 /0622 750 234