Siku wanawake duniani ichochee usawa wa kijinsia

26Feb 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Siku wanawake duniani ichochee usawa wa kijinsia

MACHI 8 kila mwaka, huwa ni siku ya kimataifa ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoangazia masuala yanayohusu wanawake katika harakati mbalimbali, hasa za masuala ya usawa wa kijinsia.

Wiki mbili zijazo, Tanzania itaungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa, katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu usemayo: "Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na Baadaye"

Serikali imetoa maelekezo kuwa maadhimisho yafanyike ngazi ya mkoa, kutoa wigo kwa wanawake, wadau wengine kutathmini hatua ambazo taifa limefikia katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana.

Kimsingi usawa wa kijinsia ni moja ya mambo muhimu na unahamasishwa, ili kuhakikisha hakuna ubaguzi kwenye jamii katika kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwamo za uzalishaji mali.

Kutokana na umuhimu wa usawa wa kijinsia, baadhi ya nchi zimekuwa zikifanya juhudi za kuwapa wanawake nyadhifa kubwa za uongozi ili kwamba waweze kutoa mchango wao katika kuongoza.

Tanzania inatajwa kuwa ni miongoni mwa za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo imewezesha wanawake kujikita zaidi katika kujiwezesha kukuza mitaji na kuinua uchumi wao.

Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutambua sheria za usawa wa kijinsia.

Ni katika moja ya hotuba zake wakati akizindua machapisho ya kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kwa nchi za SADC, kwamba masuala ya kuwawezesha wanawake katika sekta mbalimbali yanaonekana.

Anasisitiza kuwa serikali inatambua uwepo wa usawa wa kijinsia na uendelezwaji wanawake nchini na kwamba hilo limetambuliwa katika Katiba ya nchi kama suala muhimu kwa haki za binadamu.

Wakati huu ambao dunia inaelekea katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ni muhimu kutambua kuwa haiwezekani kuwa na mafanikio katika jamii iwapo baadhi ya makundi yataachwa nyuma, hasa wanawake.

Ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi ni suala muhimu, lengo likiwa ni kuhakikisha maendeleo yanaletwa na Watanzania wote bila kubagua ikiwa ni njia mojawapo ya kufikia usawa wa kijinsia.

Ni kweli kwamba wanawake nchini, wamekuwa wakiwezeshwa kielimu na kushirikishwa katika ngazi za maamuzi na uongozi, siyo vibaya kasi hiyo ikaongezeka ili kupata wanawake wengi zaidi katika ngazi za maamuzi.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu iwe ni chachu ya kufikia kile ambacho serikali imekusudia kwa ajili ya usawa wa jinsia nchini na pia kumaliza ukatili wa kijinsia unaoendelea kwenye baadhi ya jamii.

Serikali ilishaandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana -(1998).

Serikali inaamini utekelezaji wa mpango huo utachangia katika utekelezaji wa mipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto.

Kwa kawaida binadamu huzaliwa na jinsi ya kike au kiume, na jinsi hizo ni tofauti ya kibaologia, lakini hazihusiani na nani kati ya mwanamke au mwanamume ni wa hali ya juu zaidi ya mwingine.

Kwa hiyo serikali inapochukua hatua mbalimbali za kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwapo na pia kutokomeza vitendo vya ukatili wa jinsia, jamii haina budi kuunga mkono hatua hizo.

Ninasema hivyo, kwa sababu uhusiano uliyopo umejengwa na jamii yenyewe (wanaume na wanawake), lakini unaweza kubadilishwa na ukaleta usawa wa kijisia iwapo jamii itabadilika.

Ikumbukwe kwamba udhalilishaji kijinsia hutokea pale tafsiri za jamii kuhusu haki, wajibu na majukumu inapoashiria kujenga tabaka au 'mapengo' kati ya mwanamke na mwanamume katika ngazi mbalimbali.