Siku ya Wanawake itapendeza kwa kupinga ukatili kivitendo

08Mar 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Siku ya Wanawake itapendeza kwa kupinga ukatili kivitendo

VITENDO vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, vikiwamo kutopandishwa vyeo, kutolipwa maslahi na ujira mdogo, kutoajiriwa na kuombwa rushwa ya ngono ili wapate haki zao, ni changamoto inayowakabili wanawake.

Mbali na hivyo, vitendo vingine ni kupoteza ajira pale wanapojifungua, kunyimwa kinga na likizo za uzazi, hata ruksa ya kunyonyesha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ndiye anaamua kukemea hayo, kwamba ni dhana ya kibaguzi na haikubaliki.

Anaeleza kwamba, zina madhara makubwa kwa wanawake, kwa sababu vinawanyima fursa sawa katika ajira, hivyo kusababisha watumbukie katika lindi la umaskini na kuathiri mchango wao katika ukuzaji uchumi wa nchi.

Waziri Mhagama, alitamka hayo mwaka juzi, alipofungua kikao cha viongozi wanawake wa vyama vya wafanyakazi nchini wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) jijini Dodoma. Hapo ndipo, alipovitaja vitendo vya ukatili, ambavyo wanawake wanakumbana navyo.

"Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Namba 6 ya 2004, inaeleza ni marufuku kwa mwajiri kumbagua mfanyakazi katika masuala yahusuyo kazi na ajira, kwa misingi ya jinsia, ujauzito na majukumu ya kifamilia," anasema Mhagama.

Anasema nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ikiwamo Tanzania, zilipitisha ajenda ya Maendeleo Endelevu 2030 yenye malengo 17. Miongoni mwake ni lengo namba tano linalohusu usawa wa kijinsia katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii.

Pamoja na vitendo hivyo, bado kumekuwapo na changamoto kadhaa zinazowakumba wanawake, zikiwamo hizo anazotaja Waziri Mhagama, ambazo kimsingi zinahitaji kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Leo ni tunaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Tanzania ikuungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hiyo, kupitia kaulimbiu: "Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu."

Ni siku inayoadhimishwa kila Machi 8 ya mwaka, ikiwa na kaulimbiu za mwaka zinazolenga kuhamasisha jamii kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na kuzingatia usawa wa kijinsia.

Historia inaonyesha kuwa zaidi ya karne sasa imepita, umma unaadhimisha siku hiyo, lakini bado wanawake wameendelea kukumbana na changamoto zinazochangia kuwafanya waonekane ni wanyonge.

Siku ya Wanawake Duniani, inatathmini maendeleo ya wanawake katika jamii kwa namna mbalimbali, ikiwamo kiuchumi inalenga kuondoa mfumo dume, ambao umewafanya wanyanyasike.

Serikali nchini imeshaweka wazi kwamba imeandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto, kwa lengo la kupunguza kiwango cha ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Inasema kwamba, mpango huo ni utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana - (1998).

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alikaririwa akisema hayo Desemba mwaka jana, alipozindua kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia. Alisema serikali imeandaa mpango huo kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika ngazi ya makundi ya jamii za kitanzania, kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Anautafsiri ukatili wa kijinsia, ni utendaji wa maovu, na vinavyodhalilisha, kutesa, kunyanyasa, kukandamiza, visivyojali haki za kuishi kwa binadamu yeyote, awe wa kike au wa kiume.

Majaliwa anasema, ukatili wa kijinsia huja katika taswira nyingi, kuanzia vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi, lugha na vitendo vya udhalilishaji, pia kunyimwa fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

"Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji wowote unaofanywa na mtu dhidi ya mwingine, bila ya kujali umri, maumbile, kabila, rangi, dini au mtazamo wa kisiasa.

“Unyanyasaji huu unahusisha mambo mengi kama kumpiga mwanamke au mwanaume, kumnyima mtoto elimu, kumlawiti mtoto wa kike au kiume, kumbagua mtu katika mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi warithi wanaohusika," anasema Majaliwa.

Hivyo, Tanzania inapoungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku hiyo, ni vyema suala la kukomesha vitendo vya ukatili kwa wanawake lizidi kutiliwa mkazo.