Simba, Azam zisajili wageni wenye viwango

12Jun 2016
Adam Fungamwango
Lete Raha
Jicho Pevu
Simba, Azam zisajili wageni wenye viwango

NIMESIKA uongozi wa klabu ya klabu ya Azam FC wakisema kuwa wanapeleka mapendekezo Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kuomba kuongezwa kwa wachezaji wa kigeni kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Azam imeomba kuanzia msimu ujao kuwe na wachezaji 10 wa kigeni.

Inasema imeomba hivyo kutokana na tathmini waliyoifanya kwenye michuano ya kimataifa, na kugundua kuwa moja ya tatizo lililowafanya wafanye vibaya ni kutokuwa na wachezaji wengi wa Kitanzania wenye uwezo wa kupambana na wachezaji wa klabu za nje ambazo nazo pia zinakuwa zimesheheni wageni kutoka nje ya nchi zao.

Ukilifutilia kwa undani pendekezo la Azam lina mantiki kwa upande mmoja. Ni kweli kwa dunia tunayokwenda nayo si rahisi kuacha kusajili wachezaji wa kigeni.

Hata klabu kubwa barani Afrika ukiziangalia, utakuta zina baadhi ya wachezaji toka nje ya nchini zao.

Hata klabu za nchi kama Misri, Algeria, Nigeria, Cameroon, Ghana, Congo, pamoja na kwamba ziko juu kimpira, lakini zina wachezaji wengi kutoka nje ya nchi zao.

Hii yote ni kuongeza ladha na vionjo vya soka kutoka kona mbalimbali za Afrika, ili kukabiliana na aina zote za timu zinazokutana nazo kutoka pande zote.

Lakini pamoja kwa upande wa pili nina wasiwasi na hilo na hasa ubora wa wachezaji wenyewe.

Napenda kuwaambia Azam kuwa tatizo lililopo kwenye timu yao si idadi ya wachezaji wa kigeni, ila ni ubora wa wachezaji hao.
Kwa misimu michache iliyopita, Azam imekuwa haina wachezaji wengi bora wa kigeni.

Badala yake imekuwa ikibebwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji wawili tu ambao ni Kipre Tchetche na Paschal Wawa.

Ukiondoa hao, waliobaki watano ni wachezaji wa kawaida sana ambao hata hapa nchini wanapatikana.

Nina uhakika kama Azam ingekuwa na wachezaji saba bora kabisa na wenye viwango vya hali juu, ilikuwa kwenye nafasi kubwa msimu huu kuitoa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) timu ya Esperance ya Tunisia ambayo iliondolewa kwenye mechi ya marudiano.

Hii ilitokana na kutokuwa na wachezaji wa kigeni wenye viwango vya hali ya juu, ambao wangeweza kuwapa changamoto kali wachezaji wa Kitanzania na kuifanya timu kuwa imara.

Ugonjwa huo wa Azam ndiyo ambao inao Simba kwa misimu hii michache.Haikuwa na wachezaji wengi wa kigeni wenye uwezo wa hali ya juu na badala yake ilisajili 'makapi', tena ni afadhali hata wa Azam.

Tukiangalia mfano wa Yanga ambayo imetinga hatua ya makundi, imebebwa zaidi na wachezaji wa kigeni kila Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Mbuyu Twite, Vicent Bossou, Haruna Niyonzima na Amissi Tambwe.

Hawa waliwaongoza wachezaji wa Kibongo kuifanya Yanga kuwa ya kutisha msimu huu kiasi cha kufanya vema hata kwenye mechi za kimataifa ambako sasa iko katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwenye soka ukipata wachezaji wengi ambao wana uwezo wa juu, huwa wana uwezo hata wa kuficha mapungufu ya wachezaji wengine.Ndivyo ilivyo Yanga kwa sasa. Imejitahidi sana kusajili wachezaji hasa wa kigeni wenye uwezo mkubwa.

Hata Simba iliyofanya vema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2012 kiasi cha kuitoa timu ngumu ya ES Setif, ilibebwa zaidi na wachezaji watatu tu wa kigeni ambao ni marehemu Patrick Mafisango, Emmanuel Okwi na Felix Sunzu.

Wachezaji hawa watatu walikuwa mhimili mkubwa wa Simba, wakiwaongoza wachezaji wengine wa Kitanzania kuunda timu ambayo ilikuwa ya kuogopeka ndani na nje ya nchi.
Simba haikuwa na wachezaji wengi wa kigeni kiasi hicho, lakini ilifanya vema hata kwenye mechi za kimataifa, na hii inathibitisha kuwa idadi si tatizo, ila kinachotakiwa ni uwezo wa wachezaji hao.

Wala siwashauri Shirikisho la Soka Nchini (TFF) wakatae kuruhusu idadi hiyo ya wachezaji, au wakubali, vyovyote watakavyoamua ni sawa, ila tu nataka kuiambia Azam na timu nyingine zenye mawazo kama hayo kuwa kinachotakiwa ni uwezo wa wachezaji na si idadi.

TFF inaweza kuamua kuruhusu wachezaji 10, lakini kama klabu za Simba, Yanga na nyingine zitaendelea na tabia ya kuleta nchini wachezaji wasio na viwango, basi wanaweza kuonekana ni wachache na kuomba tena kuongezwa.

Ni kwa sababu bado hawatokidhi mahitaji ya timu.Lakini inawekana kabisa kama idadi ya wachezaji hawa hawa saba kama nafasi hizo zingetumiwa kusajili vizuri 'maproo' wala kusingeonekana mapungufu.

Nionavyo mimi mapungufu yaliyoonekana kwenye klabu za Simba na Azam ni kwa sababu tu ya kutosajili wachezaji wenye viwango, na wala si idadi ndogo.
Ndiyo maana klabu ya Yanga haijapeleka mapendekezo ya kutaka kuongezwa wachezaji wa kigeni kufikia 10.

Wamezitumia vizuri nafasi zao za usajili kwa kusajili 'vifaa' na sasa wanataka kuitumia nafasi moja ya kigeni ya Soffou Boubacar ambaye ndiye pekee anayoonekana kuwa amechemka, kusajili kifaa kingine ambacho kinaweza kuleta tija ndani ya kikosi hicho.

Azam badala ya kuomba idadi ya wachezaji wa kigeni waongezwe, kwanza ingejifunga kibwebwe na kushusha 'vifaa vinne au vitano' vya nguvu toka pembe mbalimbali za Afrika ambavyo sina shaka vingeibadilisha kabisa timu hiyo, ambavyo msimu huu ilionekana kuwa ya kawaida tu na ilitumia zaidi uzoefu kuliko uwezo.

Ni suala la kuamua tu kwanza wala sina shaka na pesa za usajili kwa klabu hiyo.Kwa upande wa Simba nayo kama inataka ubingwa na kurudi tena kucheza mechi za kimataifa, ifanye usajili wa maana hasa kwa wachezaji wa kigeni.

Idadi ya wachezaji saba tu wa maana inatosha kabisa kuzibadilisha timu hizo kama ambavyo Yanga inavyobebwa na idadi ya wachezaji sita tu na wala si 10.
Cha maana ni ubora na si idadi ya wageni.