Simba, Mtibwa zifanye hivi kukamilisha kazi

03Dec 2018
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Mtibwa zifanye hivi kukamilisha kazi

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, Simba na Mtibwa Sugar kesho zinatupa karata zao za mwisho kwenye mechi za awali za michuano hiyo.

Timu zote zitakuwa ugenini zikiwa na kazi moja tu ya kukamilisha kazi ambazo walizianza wiki iliyopita.

Simba inayoiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika  itakuwa nchini Swaziland kurudiana na Mbabane Swallows kwenye  mechi ambayo itakuwa ngumu, kwani wenyeji watakuwa na kazi ya kutafuta mabao 3-0 ili kusonga mbele.

Kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa nchini, Simba ikishinda mabao  4-1 na kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga kwenye raundi ya kwanza.

Kwa upande wa Mtibwa inayowakilisha nchi kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho, itarudiana na Northern Dynamo ya Shelisheli ugenini, huku kibindoni ikiwa na mtaji mnono wa mabao 4-0 iliyoyapata Jumanne iliyopita nchini Tanzania.

Pamoja na kwamba inaonekana imeshatinga hatua nyingine, timu ya Mtibwa haitakiwi kubweteka kwani inatakiwa kuendelea kuthibitisha ubora wake.

Haitakiwi tena kucheza kwa masihara kwa sababu wapinzani wao wanaonekana ni vibonde au kuona mabao manne ni mengi yasiyoweza  kurudishwa, badala yake kama kushinda tena kwa idadi hiyo ya mabao wafanye hivyo.

Simba ndiyo inayoonekana ina kibarua kizito kwani wapinzani wao si timu ya mchezo. Kwenye mechi hii wachezaji wa Simba wanachotakiwa kufanya ili mechi iwe rahisi mno kwao ni kusaka bao moja tu la ugenini ambalo litawakatisha kabisa tamaa wapinzani wao,  kwani watakuwa wanahitaji kufunga mabao matano ili kusonga mbele kitu ambacho kitakuwa ni kigumu.

Wachezaji wa Simba watatakiwa kucheze kana kwamba hawajashinda  kwenye mechi ya mwanzo na si vinginevyo.

Kwanza kabisa mabeki wanatakiwa kuwa makini kutofanya makosa ya kiufundi, lakini pia kutoweka mpira nyuma bila sababu za msingi ili  kutowapa nafasi ya kupata bao kiurahisi.

Kwenye mechi hiyo, wachezaji wote wa Simba ikiwamo hata  washambuliaji wacheze kwa kujituma na kukaba ili kuwabughudhi na kushindwa kukaa na mpira muda mrefu au kupiga pasi zinazotakiwa  kufika eneo husika.

Simba ihakikishe pia inatawala eneo la kati ili kuwapoteza wapinzani wao ambao wanaonekana nao ni wazuri mno eneo hilo.

Washambuliaji nao watatakiwa kuwa makini kutumia nafasi  wanazozipata kupata mabao yatakayorahisisha mechi kwao na kuwa ngumu kwa wageni. Wakumbuke kuweka mpira ndani ya nyavu tu ndiyo kutawaweka salama Simba na kuimaliza mechi yote.

Ninazitakiwa kila la kheri timu zote za Tanzania kwenye michuano hiyo.