Simba mwenda pole ndiye mla nyama

19Apr 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Simba mwenda pole ndiye mla nyama

“RUFANI ya kesi ya utakatishaji fedha na kugushi inayomkabili wakili maarufu nchini, Median Mwale na wenzake watatu jana imeshindwa kusomwa na majaji watatu wa Mahakama Kuu, baada ya jaji mmoja kuamua kujitoa.”

Sentensi hiyo ina makosa matatu. Kwanza ni neno ‘gushi’ lisilo la Kiswahili; pili kushindwa kuchanganua wakati uliopita na ulipo; tatu ni ‘kesi imeshindwa kusomwa.’

Badala ya ‘gushi’ neno sahihi ni ‘ghushi’ lenye maana mbili. i) iga saini au maandishi ya mtu kwa nia ya kudanganya; bini, changanya vitu. ii) kamili, isiyozidi wala kupungua. Kwa muktadha huu twazungumzia maana ya kwanza.

Katika sentensi hiyo, mwandishi atwambia “… jana imeshindwa kusomwa …” Inaposemwa ‘jana,’ maana yake ni siku kabla ya leo hivyo neno linalofuata haliwekwi katika wakati uliopo. Vilevile kesi ‘haishindwi kusomwa’ bali yashindikana kusomwa kwa sababu …

Ingeandikwa: “Rufani ya kesi ya utakatishaji fedha na kughushi inayomkabili wakili maarufu nchini, Median Mwale na wenzake watatu, jana ilishindikana (kitendo cha jambo kutoweza kutekelezwa kutokana na sababu fulani) kusomwa kutokana na jaji mmoja kati ya watatu kujitoa.”

Mwalimu rafiki yangu Mohamed Sharif alinitumia ujumbe huu kuhusu wananokosea kuandika Kiswahili fasaha: “Kwa vile Tanzania ina makabila mengi na yote yana haki ya Kiswahili, basi la msingi ni kuzingatia kanuni. “Akiandika ‘hichi’ ifuatie ‘chifungu.’ Kwani huoni kuwa twasomewa ‘Taalifa ya Habali’ kwenye TV zetu.

Kuhusu kuchanganya maneno ya Kiingereza na Kiswahili, msomaji Vincent Kalinga wa Iringa alinitumia ujumbe usemao: “Nakubaliana nawe Bakita likemee upotoshwaji wa maneno pia likemee matangazo ya biashara ya mitandao kwa kuleta maneno kama ‘Wagiftishe’, ‘smatifonika,’ ‘deilee,’ n.k.”

Stanslaus wa Morogoro aliandika: “Nakubaliana na wewe kuhusu matumizi ya Kiswahili.”
Msomaji mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, anasema: “Hali yako mzee. Leo katika safu ya Muungwana Lazima Nilingo, Bw. Gwamaka anauliza ‘Imekuwaje Mchina katushinda mtihani wa Kiswahili kidato cha nne?’

“Kiswahili ni somo kama jingine na Mchina kapata A yote? 2. Kuna maprofesa wa Kkiswahilii duniani hawajakanyaga ardhi yoyote ya nchi ya Kiswahili?”

Msomaji mwingine akaniandikia kuhusu waandishi wachafuzi wa lugha ya Kiswahili, aliandika hivi: “Bora mauzo yanapanda, nani atajali matamshi na fasaha?”

Katika moja ya vituo vyetu vya runinga, kuna tangazo litolewalo mara kwa mara kukaribisha watangazaji kwamba watapata nafasi kubwa kuliko ya matangazo …Isemwapo ‘nafasi kubwa kuliko ya matangazo’ ina maana gani?

‘Kuliko’ lina maana mbili: kwenye: i) kiwakilishi cha mahali kusikodhihirika: kuliko na ngoma ni wapi? ii) kuzidi, zaidi ya; mnazi ni mrefu kuliko mchungwa; twiga ni mrefu kuliko wanyama wote.

Msomaji mwingine anayefuatilia safu hii aliniandikia: “Hongera kwa kuwakosoa waandishi kwa kutumia lugha za mitaani katika vyombo rasmi. Pamoja na uandishi kuna pia matamshi yasiyo sahihi. Mfano: hiko ‘kitu’ badala ya hicho ‘kitu.’”

“Kamusoko, Niyonzima pasi za mabao hadi aibu” ni kichwa cha moja ya magazeti ya michezo ikifuatiwa na habari kuwa “Viungo washambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na Mnyarwanda Haruna Niyonzima wamefunika kwa kuwa viungo vinara wa kupiga pasi za mwisho zilizozaa mabao msimu huu.”

Kama ni vinara wa kutoa pasi za mwisho zilizosababisha mabao, ‘aibu’ inayosemwa ni ipi? ‘Aibu’ ni jambo la kumvunjia mtu heshima; dosari katika kitu, mtu au jambo.

“Bia hii ambayo ni ya kupimwa kuanzia glasi ya Sh 500 hupendwa na vijana ambao husema kuwa wanajiunga kivurushi cha gharama nafuu.” Sipati maana ya ‘kivurushi’ ila hapana shaka mwandishi alikusudia neno ‘kifurushi’ lenye maana ya kitu kidogo kilichofungashwa kwenye karatasi.

“Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupitia kwa maafisa uvuvi wake, imekamata na kutekeleza mzigo wa samaki aina ya magege wenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 2.5 ulioingizwa nchini kinyemela.”

Neno ‘kutekeleza’ mzigo ndilo liliharibu mtiririko wa sentensi. Maana ya ‘tekeleza’ ni tenda kama ilivyotakiwa; kamilisha. ‘Telekeza’ ni acha kuendelea na jambo au shughuli uliyokwisha ianza; acha kutunza mtu au watu wanaokutegemea, tupa watoto.

‘Teketeza’ ni unguza kitu kwa moto hadi kwisha kabisa; haribu kabisa kwa moto au joto. Kwa hiyo samaki waliokamatwa Mbeya ‘hawakutekelezwa’ bali waliteketezwa.
Methali: Ukipanda upepo, utavuna tufani.
[email protected]
0715/0784 33 40 96