Simba tutoeni kimasomaso

23Mar 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba tutoeni kimasomaso

MAANA ya ‘kimasomaso’ ni aibu, haya au tahayuri ambayo mtu ataka kuikwepa; tendo la kujiondoa katika haya; jitoa katika aibu. Hili ndilo Watanzania kwa ujumla wetu twapaswa kuiombea timu ya Simba katika mbio zake za Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Mgema akisifiwa, tembo hulitia maji.” Kwa kawaida mgema apewapo sifa kutokana na tembo lake, badala ya kutengeneza tembo zuri hulitia maji na kuliharibu. Ni methali ya kutumiwa kuwanasihi watu kutomsifu mtu sana asije kufura kichwa na kuharibika. Pia hutumiwa kwa mtu ambaye asifiwapo huishia kujivuna.

Hii ni maalumu kwa viongozi, wanachama, mashabiki na zaidi sana wachezaji wa Simba. Ni dhahiri kuwa Simba imefanya vizuri katika michuano ya kimataifa baada ya kuingia kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu zingine zilizoingia hatua hiyo ni TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Esparance Sportive de Tunis ya Tunisia, ambayo imetwaa ubingwa nchi yao mara 28. Nyingine ni Wydad Athletic Club.

Esperance Sportive de Tunis ni timu pekee iliyomaliza mechi zake bila kupoteza mchezo wowote na kupata alama 14. Imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu na kuwa katika nafasi ya pili mara nne miaka ya 1999, 2000, 2010 na 2018.

Kwa ufupi, timu zote hizo zina uzoefu mkubwa kuliko Simba yetu. Kwa hiyo si timu za kubezwa kama idhaniwavyo na wengi. Kwa sababu hii, badala ya viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba kujinasibu kuwa watapata ushindi kirahisi ni muhimu kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili watambue timu watakazokutana nazo zina uzoefu zaidi katika mashindano hayo kuliko Simba yetu.

Wachezaji wanatakiwa kuwa makini na kutokuwa na uwoga kwa kuwa timu zote zina wachezaji 11 kila mmoja akiwa na miguu miwili kama walivyo Simba. Muhimu ni kuwa na nidhamu ya mchezo na kucheza kwa ari kwa kuwa hakuna kubwa lisiloshindwa, chambilecho wahenga.

Maneno haya hutumiwa kumhimiza mtu anayekabiliana na hali ngumu kuwa lazima atafanikiwa. Wachezaji wa Simba wanapaswa kutambua kuwa penye nia pana njia. Hii ni methali ya kuwakumbusha wachezaji wetu kuwa wakiwa na nia ya ushindi ni lazima watafanikiwa.

Wahenga walisema: “Simba mwenda pole (kimya) ndiye mla nyama.” Maana yake Simba aendaye taratibu bila ya kujitambulisha ndiye awezaye kuwagwia (kuwakamata) wanyama bila shida. Hii ni methali ya kuwanasihi wachezaji wa Simba wawe na umakini na utaratibu katika uchezaji wao, wasipapie mambo na mwisho watafanikiwa, Inshallah (apendapo Mwenyezi Mungu)!

Kwanza nijitambulishe kwa wana Yanga wenzangu. Nilijiunga na Yanga tarehe 2 Desemba, 1966 na kupewa kadi ya kwanza yenye namba 447. Kadi zilipobadilishwa mwaka 1976, nikapewa kadi namba 01868 kisha kadi namba 0340 ya mwaka 1993 na ya sasa ni namba 007887 iliyotolewa mwaka 2008. Wakati wote nitakuwa mkweli kwa klabu yangu.

Ni ukweli usiopingika kuwa ingawa Yanga tumetwaa ubingwa mara nyingi zaidi kuliko timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu, wakiwamo watani zetu, Simba, tumeshindwa kuiwakilisha vema Tanzania kwenye mechi za kimataifa ipasavyo. Simba wamekuwa mabingwa wa Tanzania mara chache lakini wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mechi za kimataifa kuliko Yanga. Sasa ndiwo wanaoiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Afrika.

Simba ilikuwa timu ya kwanza Tanzania kucheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1993 jijini Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-0 mbele ya Rais wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kwenye Uwanja wa Taifa (siku hizi Uhuru) jijini Dar es Salaam.

Rais Mwinyi aliwaasa watazamaji waliojaa uwanja ule kuwa waache tofauti zao za kiitikadi na waishangilie Simba kwa kuwa ilikuwa inaiwakilisha Tanzania. Tukaombwa tuonyeshe uzalendo wetu.

Kweli ilikuwa hivyo hata pale Simba ilipofungwa bao la kwanza kwani uwanja ulikuwa kimya; lakini ilipofungwa la pili, uzalendo ukawashinda watazamaji wa upande ulee … wakaimba “Uzalendo umetushinda … uzalendo umetushinda …” wakifurahia Simba kushindwa! Wageni wakaondoka na kombe lao na kutuacha Watanzania tukikodoa wakati wageni wakikabidhiwa kombe lao kwenye uwanja wetu. Ilikuwa fedheha iliyoje!

Baada ya hapo kulikuwa na maneno ya chini chini kuwa eti kuna fedha zilizotumika kuwapa baadhi ya wachezaji muhimu wa Simba ili timu ishindwe! Eti kuna tajiri wao fulani alifanya hivyo ili kuepuka kutoa mamilioni ya fedha alizowaahidi wachezaji kama wangeshinda! Kama kuna ukweli ama la, Allahu ya aalam (Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua zaidi).

Leo Taifa Stars itapambana na Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Twende kwa wingi ili kuujaza Uwanja wa Taifa pomoni (katika hali ya kujaa au kwa wingi) tukiwa na mavazi yanayolandana na bendera ya taifa letu, mavuvuzela, ngoma na nyimbo za kuwatia mori (hima, ari na hamasa ya kutenda jambo) wachezaji wetu ili kuwakatisha tamaa Waganda.

[email protected]

0715 334 096