Simba, Yanga: Akutendae mtende!

18Mar 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga: Akutendae mtende!

‘HASIDI’ ni mtu anayetaka heri ya mwenziwe iondoke hata kama hawezi kuipata.

‘Hasimu’ ni neno lenye maana mbili zinazokaribiana. Kwanza ni mtu anayechukiana na mwingine; adui. Pili ni kitendo cha kuepukana baada ya kupita ugomvi. ‘Hasimisha’ ni kitendo cha kugombanisha.

‘Hasira’ ni hisia ya kutofurahishwa na mtu au kitu na kudhihirisha chuki; ghadhabu. ‘Hasiri’ ni kitendo cha kumtia mtu hasara.

Simba na Yanga zaitwa ‘watani wa jadi.’ Maana halisi ya ‘utani’ ni maneno au vitendo vya dhihaka; mzaha. Pia tabia ya watu kufanyiana masihara kwa lengo la kuambiana ukweli na kuimarisha uhusiano wao.

Vilabu hivyo kongwe nchini vyadhihakiana (fanyiana masihara) au vyahasimiana kwa lengo la kuendeleza mfarakano (hali au jambo linalosababisha watu kutoelewana na kuwa mbalimbali)?

Hakuna moja kati yao inayopenda mafanikio ya nyingine. Simba au Yanga inapopambana na timu pinzani ya humu nchini ama kutoka nje ya Tanzania, kuna wanaokwenda uwanjani kuangalia mchezo na kuufurahia.

Kwa mashabiki wengi wa Simba na Yanga mambo ni tofauti. Huenda uwanjani kuiombea mabaya timu ya ‘watani’ ifanye vibaya na hushangilia sana wanapofungwa!

Simba inapocheza na timu ya ndani au ya nje, Yanga huwa ‘mzigoni’ kuhakikisha Simba haishindi. Kadhalika Yanga ichezapo, Simba nao hufanya kila wawezalo ili Yanga ifungwe. Kwa ufupi zote zafanyiana uhasama, eti ili kuwe na ‘utulivu jijini!’

‘Utulivu’ unaosemwa ni upande ulioshindwa kuwa kimya huku mwingine ukitoa maneno mengi ya kuwadhihaki mashabiki wa upande ulioshindwa.

Kwa hali hiyo hakuna utulivu unaosemwa kwani kila upande huwa na zamu ya kutoa maneno ya maudhi dhidi ya mwingine. Wanaoshinda hutamba na kujisifu kwa maneno ya maudhi kuwadharau washindwa.

Mfano wa karibuni ni wakati Yanga ilipokwenda Morogoro kupambana na Mtibwa ya Turiani kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom. Simba walikuwa upande wa Mtibwa na ingawa walitoka suluhu, mashabiki wao walifurahi kwani timu yao iliendelea kuongoza kwenye msimamo wa Ligi.

Yanga ilipocheza na timu ya Ngaya kutoka Comoro na kutangulia kuongoza kwa bao moja dhidi ya Yanga, upande wanaokaa mashabiki wa Simba ulishangilia sana. Yanga iliposawazisha, waliokuwa wakishangilia walitulia tuli.

Mwisho wa mchezo, timu nzima ya Ngaya ilisogea upande wanaokaa mashabiki wa Simba na kuonesha ishara ya kuwashukuru kwa jinsi walivyowashangilia.

Siku Yanga ilipocheza na Zanaco ya Zambia, mashabiki wa Simba walikuwa upande wa Zanaco hata wageni hao waliposawazisha na kuwa 1-1, ungedhani Simba ndiwo walioshinda kwa jinsi walivyoshangilia! Mwisho wa mchezo wachezaji wa Zanaco walikwenda upande wa Simba na kuonesha ishara ya kuwashukuru.

Simba walipokuwa kwenye matayarisho ya kwenda kanda ya Ziwa kupambana na Toto African na Mbao FC jijini Mwanza, yasemekana ‘wajuaji’ wa Yanga walitangulizwa kule kabla Simba hawajapeleka watu wao kwa ‘kazi maalumu!’

Tayari Simba nao wamo katika hekaheka za ‘kuipiga jeki’ Azam ili timu hiyo itakapopambana na Yanga kwenye mechi ya marudiano ya Ligi Kuu, iifunge Yanga, jiji litulie!

Akutendaye mtende, simche akutendaye. Maana yake aliyekutenda ubaya wowote hupaswi kumwogopa; nawe mtende hivyo.

Ndivyo zinavyohasimiana Simba na Yanga kisha zadanganyana eti ni ‘utani!’ Mashabiki wao hufurahi moja inapoanguka kwa kile kisemwacho ‘ubaya ubaya tu.’ Pukachaka (neno lenye kuashiria kutema mate ambalo humaanisha kukidharau kitu kilichotajwa)!
Yanga itaweza kufanya kama ilivyofanya Simba kule Zambia kwa kuifunga Mufulira Wanderers mabao 5-0 kulipiza kisasi cha kufungwa 3-0 jijini Dar es Salaam? Twasubiri jibu leo.

[email protected]
0715/0784 33 40 96