Simba itacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers ya Uganda, wakati Yanga Jumatano itakuwa kwenye uwanja huo huo wa Benjamin Mkapa, kumenyana na Real Bamako kwenye Kombe la Shirikisho la Soka barani Afrika.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi kupita, tunashuhudia klabu mbili kubwa zikiwa kwenye michuano hii mikubwa na kila moja ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kupata ushindi.
Ukitazama ratiba ya michuano hii ilivyopangwa kwa timu zote mbili, unaona kabisa kuwa kitakachofanya zisisonge mbele kwenye hatua ya robo fainali ni uwezo tu wa uwanjani na wala si kitu kingine chochote.
Ratiba ya michuano hii tangu mwanzo imeonekana si kuzipendelea ila kuzibeba timu za Tanzania. Zote zimeanzia ugenini na kwa bahati mbaya zikafungwa. Simba ikafungwa dhidi ya Horoya ya Guinea bao 1-0 na Yanga mabao 2-0 dhidi ya Monastir ya Tunisia.
Zikarudi nyumbani, Yanga ikashinda 3-1 dhidi ya TP Mazembe, lakini Simba kwa bahati mbaya ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca.
Halafu zote zikatoka kusafiri tena ugenini, Yanga ikalazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Real Bamako ya Mali, Simba ikashinda bao 1-0 dhidi ya Vipers ya Uganda.
Ushindi wa Simba ugenini, ukaua mechi iliyopoteza nyumbani dhidi ya Raja Casablanca. Ratiba ikaendelea kuwa rafiki kwa Watanzania kwani zote mbili sasa zinarejea nyumbani kucheza na timu zile zile ambazo zimecheza nazo awali ugenini, tena ikionekana inazimudu.
Ingawa mpira una matokeo matatu, lakini kutokana na mechi za awali ambazo Simba na Yanga zimecheza, kama zikicheza kwa kiwango kile tulichokiona, zina uwezo mkubwa wa kushinda nyumbani.
Mechi za kesho na Jumatano ndizo kwa kiasi kikubwa zitaamua hatma ya timu hizi kimataifa. Pamoja na kwamba zinaweza zisifanye vema, halafu yakatokea matokeo mengine yasiyotarajiwa yakawarudisha kwenye mchezo, ila mechi hizi ndizo zitatoa mwanga halisi na nini zinakwenda kufanya kwenye mechi zijazo.
Kama nilivyosema, ratiba hii iko rafiki, tena kwa timu zote za Tanzania, baada ya mechi hizi, timu hizo bado zitakuwa na mechi zingine hapa hapa nchini. Simba itacheza dhidi ya Horoya Machi 18 na Yanga dhidi ya Monastir Machi 19, mwaka huu.
Hapa utaona kuwa robo fainali ya michuano ya kimataifa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ipo miguuni mwa wachezaji wenyewe wa timu hizo. Kama watapambana kucheza kufa au kupona na kushinda mechi zote mbili ambazo zitacheza hapa nchini kila moja, basi zinaweza kujikuta zinakwenda kucheza mechi za mwisho zikiwa tayari zimeshatinga robo fainali.
Kwa wachezaji hizi siyo mechi za kucheza 'pira biriani', ni mechi za kucheza bila kuremba, badala yake ni pira la kutafuta nafasi ya kwenda robo fainali ambapo wanapaswa kucheza kwa ari, kupambana na kasi.
Kwa kutumia vitu hivyo vitatu ndivyo vinaweza kukupa matokeo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kusonga mbele kwenye mechi hizi zilizopo na si kingine.
Tunaziombea timu zetu ziweze angalau tu kuvuka hatua hii ya makundi ili ziweze kutengeneza pointi ambazo zinaweza kuifanya Tanzania kwa miaka miwili kuweza kupeleka timu nne kwenye michuano ya kimataifa bila tatizo lolote.
Kwa msimu ujao inaonekana ni kama tayari nchi imefanikiwa, kwani kinachotakiwa ni timu yoyote ile kati ya Simba au Yanga imalize nafasi ya tatu kwenye kundi, hapo itakuwa moja kwa moja Tanzania imejiweka sehemu salama bila kujali nchi zingine ambazo nazo zina timu zake hatua ya makundi kwenye michuano hiyo.
Zikivuka hatua hii ina maana tayari zitakiwa zimeshajiwekea akiba ya pointi kwa msimu kwa mwingine baada ya ujao, kwani zitahitaji pointi chache tu ili kufikia malengo.