Simba, Yanga zahitaji  kauli, umoja thabiti 

20Jan 2018
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga zahitaji  kauli, umoja thabiti 

“CHOMBO hakiendi ikiwa kila mtu anajipigia kasia.” Kasia ni ubao wa kuendeshea chombo cha bahari kama mashua.    

     Ni vigumu kwa chombo cha majini kwenda kama kila mtu anajipigia upondo. Kwa muktadha huu, ‘upondo’ ni mti mrefu au ufito unaotumika kuendeshea na kuelekeza chombo majini, kwa mfano mtumbwi.

    Methali hii yatufunza umuhimu wa kushirikiana tunapofanya kazi. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, walisema wahenga. Twapaswa kutambua umuhimu wa kushirikiana katika mambo tufanyayo.

    Wanachama wa Simba na Yanga wanapaswa kuwa na umoja imara utakaoviwezesha vilabu vyao kuwa na maendeleo. Sitaji mashabiki kwani hao hawana sauti ndani ya vilabu hivyo. 

Maneno yao hayawazuii wanachama kuamua mambo yanayohusu maendeleo ya vilabu vyao. Wahenga walisema “Mwenye kelele hana neno” wakiwa na maana kwamba mtu anayepiga kelele huwa hana madhara yoyote.

Methali hii hutumiwa kutumbusha kuwa hatupaswi kumwogopa mtu mwenye kelele au fujo kwa kuwa kwa kawaida hana neno.

Simba waliingia kwenye mvutano mkubwa wa kuwa na hisa au kuendelea kuwategemea wahisani wanaosaidia kusajili wachezaji na kudai fedha zao baadaye. Kiongozi mmoja wa Baraza la Wazee aliwahi kwenda mahakamani kuzuia mpango wa klabu kuwa na hisa lakini ilishindikana.

Katika yote, Simba sasa imepata mwekezaji mwenye asilimia 49 ya hisa na 51 zilizobaki kuwa za wanachama.Wenzao, Yanga, nao wamo mbioni kuwa klabu yenye hisa. Jambo hili halina shaka kwani limekubaliwa kwa kauli moja na wanachama ingawa kuna mzee aliyeapa kutokubaliana na mpango huo mpaka afe!

Tangu ilipoanzishwa mwaka 1935 Yanga imekuwa tegemezi kwa watu mbalimbali, hasa wa jamii ya Kiasia. Kuna waliotangulia mbele ya haki na waliosalia wameamua kukaa pembeni kimya kimya. Hawa ni watu waliosujudiwa (heshimiwa kupita kiasi) hata kuwafanya kama wafalme.

Walisajili makocha na wachezaji kutoka nnje ya nchi kwa kuwalipa fedha lukuki na mishahara mikubwa ambayo kwa wachezaji wetu ni kama ndoto za Alinacha mpenda spoti! Tunao wachezaji wengi nchini lakini kwa Simba na Yanga ni kutafuta sifa ya kuwa na wachezaji wageni wanaolipwa mishahara mikubwa.

Baadhi yao walidhihirika kutokuwa na uwezo uliotarajiwa, wakafungashiwa virago! 

Ninachosema ni kwamba tabia ya vilabu vyetu kuwategemea ‘wafadhili’ kwa miaka nenda-rudi haitakuwa na maendeleo yoyote si kwao (Simba na Yanga) tu bali kwa nchi (Tanzania) pia. 

Kwa nini? Kwa sababu matokeo yake ni kutokuwa na timu nzuri zenye uwezo wa kuziwakilisha si vilabu tu bali hata taifa kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CECAFA, CAF na FIFA.

Tunazo timu za taifa za vijana, wakubwa na wanawake zinazoiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya kimataifa. Zimefanya nini zaidi ya kuwa washiriki na wasindikizaji tu? Mpaka lini ilhali wachezaji tunao chekwa (kwa wingi)? Aibu iliyoje!   

    Simba wamefanya uamuzi mzuri kuwa na hisa na wanachama wa Yanga wanapaswa kuharakisha kuifanya klabu yao kuwa na hisa kama wenzao ili ifanye mipango yao kwa njia inayoeleweka kuliko ilivyo sasa.

Sidhani kama wenye hisa wataruhusu matumizi mabaya ya fedha kama mambo ya kishirikina ili timu ishinde! Ushindi wa timu hutokana na mafunzo ya walimu na wachezaji kujituma kwa kufuata maelekezo ya walimu. Si vinginevyo.

Hao wanaoukataa mpango wa vilabu kuendeshwa na wenye hisa hawana msaada wowote kwa ila wao ndio wanaofaidika na fedha za vilabu vyao. Hawana uwezo wa kusajili wala kulipa mishahara ya makocha na wachezaji. 

Kwa ufupi hawana mchango wala msaada wowote kwa vilabu zaidi ya kuwa tegemezi kwao na uhodari wa maneno kumbe “maneno ni daraja, hayazuii maji kuteremka.”

    Vilabu vya wenzetu huko nnje vimeendelea kwa sababu vinaendeshwa na wenye hisa waliowekeza fedha nyingi kuviendeleza. Hao ndio wanaobuni miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa hali hiyo hakuna mpango  wa kuomba michango ya wanachama kama tulivyozoea huku kwetu ambayo asilani haikidhi haja.

    Hawa wanaopinga klabu ya Yanga kuwa na wawekezaji watakaonunua hisa, nawafananisha na kile walichosema wahenga kuwa “Mwerevu kanga mwenye kuacha maji akaoga mchanga!”

    Kanga huwa ‘mwerevu’ au ‘mjanja’ kwa kuacha maji na kwenda kujichezesha au ‘kuoga’ mchangani! Methali hii yaweza kutumiwa kwa mtu aliyelipuuza jambo linaloweza kumfaidi au lenye nafuu na kuliandama jingine sililokuwa na faida au la kudharauliwa.

    Tatizo lingine kwa Simba na Yanga ni wenye fedha kusajili wachezaji badala ya makocha na jambo baya zaidi makocha kupangiwa wachezaji wa kucheza mechi fulani fulani! 

Ulaya makocha ndio hupewa fedha za kusajili wachezaji wanaoridhika nao. Kadhalika hawapangiwi wachezaji kama ilivyo huku kwetu na twaona jinsi kabumbu linavyochezwa kwa bidii na ufundi mwingi.

    Huku kwetu ni nadra sana makocha kupewa uhuru wa kuchagua wachezaji. Mara nyingi hupelekewa wachezaji waliosajiliwa na wenye fedha na kama makocha wanaonekana kutokubaliana nao mara kwa mara, huondoshwa haraka!

Ajabu baadhi ya wanaofukuzwa huondoka bila kulipwa stahiki zao. Ushahidi ni baadhi ya makocha na wachezaji walioondoshwa bila kukamilishiwa fedha za usajili na mishahara yao ya miezi kadhaa iliyopita! Kama vilabu vingekuwa vinaendeshwa na wenye hisa, aibu hii [email protected].com0715  334 096 /0622 750 243