Simba, Yanga ziache ujinga huu

09Feb 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga ziache ujinga huu

‘KISASI’ ni tendo analofanya mtu kwa mwingine kulipiza ubaya aliofanyiwa. Dhamiri ya mtu kumfanyia mwingine ubaya kulipiza uovu aliofanyiwa yeye kabla.

Simba ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam ndio klabu pekee ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.

Imekuwa hivyo ilipoipokonya Yanga ubingwa msimu uliopita baada ya kuusotea kwa miaka minne mfululizo. Mengi yamesemwa baada ya klabu hiyo kufungwa mabao 5-0 na AS Vita ya Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na idadi kama hiyo dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Mashabiki wa Simba na Yanga wana tabia za kijinga sana. Timu ngeni inapokuja nchini kushindana na Simba au Yanga, hushangiliwa sana na mashabiki wa moja ya timu nilizotaja.

Ukiwauliza mashabiki wa pande zote mbili watakwambia wanalipa kisasi kwani hata timu yao (Simba au Yanga) inapofungwa na timu za ughaibuni (nchi zilizo nnje ya Tanzania) walichekwa sana na mashabiki wa upande mwingine. Tabia hiyo ya kijinga huwanufaisha wageni kwa kiasi fulani kama nilivyoeleza katika moja ya makala zangu hivi karibuni kwenye gazeti hili.

Timu yoyote ya Tanzania inapocheza mechi ya kimataifa na timu kutoka nnje ya nchi, bendera zinazopeperushwa uwanjani ni za nchi mbili – nchi mwenyeji na ngeni.

Sababu zitolewazo na mashabiki wa Simba na Yanga kuhusu kuzishangilia timu ngeni, eti timu ya nyumbani ikishinda, maneno yatakuwa mengi mitaani na kujitapa kwingi dhidi ya upande mwingine (Msimbazi au Jangwani) hivyo wanawafunga midomo na kulipiza kisasi!

Hiyo imekuwa ni kawaida kwa mashabiki wa Simba na Yanga. Ni sawa na wale waliokuwa wakipinga majeshi yetu ya ulinzi kupambana na wavamizi wa Uganda walioivamia Tanzania kupitia mkoa wa Kagera na kutwaa sehemu ya ardhi yetu wakidai eti ni ‘eneo lao.’

Chondechonde tuache tabia hii ya kijinga ya kumcheka nduguyo anapopigwa na mgeni kisha kufurahia na kushangilia anavyopigwa huku ukimshangilia mgeni anavyompiga nduguyo! Ni dhahiri tutadharauliwa na kufananishwa na majununi (watu wanaopungukiwa na akili).

Kuchekana na kuzomeana iwe kwa timu za nyumbani tu yaani sisi kwa sisi lakini chuki zetu tusiwaonyeshe watu wa nje ya Tanzania kwani tunajiumbua wenyewe. Imeandikwa: “Pendo lisiwe la unafiki; lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu.” (Warumi 12:9-10).

Simba inapocheza na timu kutoka nnje ya Tanzania, ishangiliwe na watazamaji walio nnje na ndani ya uwanja. Vivyo hivyo Yanga inapocheza na timu ngeni ishangiliwe na watazamaji wote walio nnje na ndani ya uwanja kwa sababu ni timu ya nyumbani.

Kama kuna watu wasiopenda utaratibu huu, kinachowapeleka uwanjani ni kitu gani? Kwenda kumshangilia adui anayemwadhibu nduguyo (timu ya nyumbani)? Hebu tuondokane na chuki (hisia ya kutopenda kitu au jambo) kwani tunajidhuru (kitendo cha kusababisha uharibifu, hasara, athari mbaya au maafa) wenyewe.

Jambo lingine linalokera ni wanachama na mashabiki wa Y|anga kutokuwa na shauku (hamu kubwa ya kutaka kufanya jambo) ya kuishangilia timu yao wakati wanapoona timu ikiwa katika hali mbaya ya fedha na kuhofia timu kufanya vibaya. Ikumbukwe kuwa kadiri timu inavyoshangiliwa uwanjani ndivyo wachezaji wanavyopandisha mori (hima, ari na hamasa ya kutenda jambo) wa kucheza kwa bidii.

Mashabiki na wanachama wa Simba huwa na mori sana timu yao inapocheza uwanjani lakini wa Yanga ni tofauti kubwa. Kwa wanaonifahamu watadhani labda nimegeukia upande wa pili, kwamba nimejiunga na Simba, hasha (sivyo kabisa)! Nawapa ukweli wenzangu kwani wahenga walisema: “Kweli ingawa chungu niambie sinifiche.” Maana yake niambie ukweli hata kama una uchungu. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuwa na tabia ya kuusema ukweli au kuwa watu wausemao ukweli.

Mwenzako anapoteleza katika jambo fulani ni vizuri kumwambia ukweli hata kama utamchoma moyo kwani “Kweli ndio fimbo ya kukamata.” Maana yake kweli ni silaha nzuri maishani. Methali hii yatukumbusha umuhimu wa kuusema ukweli hata kama kwa kufanya hivyo tutaishia kuchukiwa na wenzetu.

Aidha ilisemwa: “Kweli ikidhihiri, uongo hujitenga.” Maana yake ukweli unapojulikana uongo unajitenga. Methali hii yatukumbusha kwamba ukweli wa jambo fulani utokeapo, uongo unaolihusu hautambuliwi tena au hauna nafasi tena. Huweza kutumiwa kumnasihi mtu anayejaribu kusema uongo wa waziwazi.
[email protected]