Simba, Yanga zinavyolia ukata wajanja wakicheka

14May 2018
Somoe Ng'itu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga zinavyolia ukata wajanja wakicheka

TIMU kongwe za soka nchini Simba na Yanga ambazo zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kila kukicha zimekuwa zinalia kukosa fedha za kujiendesha kutokana na kiasi kidogo cha pesa wanazoingiza.

Klabu hizi zenye makao yake makuu katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, mapato yake makuu kwa sasa ni fedha za wadhamini wakuu wa Ligi ambao ni Vodacom, Kampuni ya Kubashiriki Matokeo Michezoni ya SportPesa na Azam TV.

Chanzo chao kingine ni fedha zinazotokana na viingilio vya milangoni ambavyo kwa madai yao ndani ya misimu mitatu sasa vimeshuka kutokana na mashabiki kukaa kwenye televisheni kuangalia na kupungua kwenda viwanjani.

Lakini jambo la kushangaza ambalo limekuwa likipigiwa kelele kila siku ni klabu hizo kushindwa kutumia haki miliki ya nembo zao kujiingizia fedha kama wanavyofanya wenzao wa nchi zilizoendelea.

Sio Simba na Yanga peke yao ndio wanaumia katika kudhibiti ‘wajanja’ kutumia nembo kujiingizia fedha, hata Azam FC na Lipuli FC ambao wamerejea kwenye Ligi Kuu kwa mara nyingine, nao pia bidhaa zenye nembo ya klabu na hawazitambui wamekuwa wanaziona zikiuzwa na "wafabiashara haramu" wakiendelea kufaidika.

Baada ya Alhamisi, Simba ya Dar es Salaam kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa msimu wa 2017/18, tayari ‘wajanja’ hao wameingia kwenye viwanda vyao ‘bubu’ na kutengeneza bidhaa mbalimbali kama fulana na skafu wakiziuza na kujipatia kipato huku klabu ikiwa haipati kiasi chochote cha fedha katika mauzo hayo.

Huu ndio wakati wa kuamka kwa Simba na klabu nyingine na kuacha kulia pembeni kuhusu kuhujumiwa huko wakati mnahitaji fedha za usajili na maandalizi mengine yenye uhakika kwa ajili ya msimu ujao.

Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha viongozi wa klabu zote za hapa nchini kuchukua hatua kwa vitendo, ili kujikwamua katika kulia njaa kupitia miradi mbalimbali ambayo imewanyanyua wenzenu kama Barcelona na Man United ambayo licha ya kutotwaa ubingwa, tayari wameshaanza kutangaza jezi zao za msimu ujao na naamini zitaingia sokoni mapema.

Ilielezwa kuwa, mauzo ya Neymar aliyetokea Barcelona ambaye yuko Paris St. Germain ya Ufaransa yaliweza kurudisha fedha za usajili alionunuliwa na hivyo klabu kufaidika uwanjani na nje ya uwanja.

Umefika wakati tuone klabu za hapa nchini zinafaidika kwa jasho ambalo wamelitumikia na kumaliza vitendo vya hujuma ambazo kiuhalisia vinawaumiza wachezaji na familia zao ambao huwa katika wakati mgumu na kupitia changamoto mbalimbali pale wanapokaa muda mrefu bila kulipwa mishahara na posho zao.

Ugonjwa huu usiishie katika ngazi za klabu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nao wanatakiwa kuamka na kuhakikisha bidhaa mbalimbali zenye nembo yake au timu zake za Taifa zinawaingizia fedha kikamilifu, ili kusaidia kupunguza makali ya kuhudumia timu hizo.

Fedha za wadhamini hazijawahi kutosha, mahitaji na gharama za kuhudumia timu kila siku huongezeka, viongozi kama hamtaamka na kuwa wakali kwenye uuzaji wa bidhaa tutaendelea kushuhudia kauli za ukata zikitolewa hadharani kutoka kwa wachezaji, wanachama na mashabiki.

Inasikitisha kuona wajanja wanafaidika na wachezaji wanaishi maisha ya kubahatisha hadi baadhi yao wanadaiwa kugoma kucheza kwa sababu ya klabu zao kushindwa kuwalipa mishahara, tuondoke katika dunia hii na kufanya kama yale yaliyowafanya wengine wakapiga hatua.

Ni changamoto lakini hakuna kisichowezekana, klabu zikiungana na kushikilia suala hili mambo yanaweza kuwa tofauti katika msimu ujao, ili ligi iwe bora ni lazima wachezaji wawe tayari kupambana na hatimaye kupata bingwa aliyestahili ambaye atakwenda kupeperusha vyema bendera ya nchini katika mashindano ya kimataifa.

Napenda kumaliza kwa kuipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa ikiwa bado na mechi mkononi, lakini kuzitakia klabu nyingine kuimaliza ligi kwa heshima na nidhamu wakati huu tunaosubiri kuona nani anashuka daraja na kuzipisha KMC, JKT Tanzania, African Lyon, Coastal Union, Alliance FC na Biashara United zitakazocheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.