Simba, Yanga zinavyowindana

23May 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga zinavyowindana

‘UTANI’ ni desturi za kimila zinazowafanya watu wanaojuana waweze kuambiana au kutengeneza jambo lolote la mzaha bila ya kuleta chuki au kero; maneno ya dhihaka. Tabia ya watu kufanyiana masihara kwa lengo la kuambiana kweli na kuimarisha uhusiano wao.

Kwa Simba na Yanga hakuna mambo kama hayo ila ni chuki, yaani hali ya kutokuwapo upendo; hali ya kuwa na roho mbaya, kuwa na kinyongo na kutotaka maendeleo ya mwingine. Kwa ufupi, kwa sasa, Simba na Yanga si watani wa jadi kama isemwavyo, bali ni maadui. Wanaobisha wabishe tu, lakini huo ndio ukweli wenyewe.

Kwa sababu hiyo, kila moja huiombea nyingine mambo mabaya badala ya mazuri na mema. Kile kisemwacho ‘watani wa jadi’ si kweli ila ni maneno tu! Watani hawachokozani ili kufanyiana ubaya, kuzomeana na kuchekana bali husaidiana wakati wa shida, tena kwa hali na mali.

Ukitaka kuthibitisha hali hii, subiri wakati wa kipindi cha usajili uone jinsi zinavyochimbana. Kila upande hujitahidi kuwashawishi baadhi ya wachezaji wa upande mwingine ili kuwasajili. Itokeapo upande wa Msimbazi au Jangwani umepata fununu ya mwingine kumsajili mchezaji muhimu, lazima kuwe na tafrani ya aina yake.

Mchezaji huyo huandamwa kwa kila hali, kwa kuahidiwa fedha nyingi na mambo mazuri kuliko aliyoahidiwa na upande mwingine! Hali kama hii yataka mchezaji anayegombewa awe mtulivu na kufanya tafakuri itakayomwezesha kufanya uamuzi sahihi. Aidha anapaswa kuwa makini kwa watu anaowaomba ushauri.

Wanapata nafasi za kucheza au huwekwa kando na kuwa wachezaji wa akiba? Katika hali kama hiyo lazima wapime uwezo wao kama wanawazidi waliopo ama la. Vinginevyo wasikubali kughilibiwa.

Wachezaji waweke wazi kuwa mikataba watakayotia saini zao iwe na kifungu kinachowapa haki na uhuru wa kwenda kufanya majaribio na timu za ughaibuni iwapo watatakiwa. Itazinufaisha vilabu vyetu kwa kuwauza wachezaji wao nnje ya nchi.

Pia wawe waangalifu na mameneja wanaowatafutia timu kwani wanaweza kupewa hela na timu zinazotafuta wachezaji ili kuwaghilibu walipwe hela kiduchu na wakati huo huo kuchukua hela kwa wachezaji wanaotafutiwa timu.

Wahenga walisema “Fedha ilivunja nguu, milima ikalala.” Maana yake pesa zina uwezo wa kuvunja milima na vilima. Hii ni methali ya kupigia mfano uwezo wa fedha. Mtu akiwa na pesa anaweza kufanikiwa kufanya mambo ambayo asingeweza kuyafanya wala kudhania kuyafanya.

Kuna chama kilichoundwa na wachezaji wa zamani ili kutetea stahiki (kitendo cha mtu kuwa na haki ya kupata kitu fulani kutokana na ufanisi aliopata) za wachezaji wa sasa. Wachezaji wa zamani ambao sasa waitwa ‘zilipendwa’ enzi zao walifanya kandanda kama mchezo wa kuwafurahisha watazamaji na wakati huohuo kuimarisha afya zao. Hawakulipwa mishahara kama walivyo wachezaji wa sasa.

Wachezaji hao wanajua matatizo waliyokumbana nao wakati ule. Nadhani ndo sababu ya kuunda chama cha wachezaji ili walipwe mishahara na stahiki nyinginezo, kuwatetea wanapodhulumiwa au kunyimwa haki zao.

Kwa hali yoyote iwayo, chama cha wacheza kandanda hakitakuwa na nguvu bila hela kwani kuna wakati itabidi kuwatumia wanasheria ili kuwatetea wachezaji waliopunjwa/wanaopunjwa stahiki zao na wanaoachwa na vilabu vyao dakika za mwisho na kuwakosesha timu za kuwasajili!

Twaambiwa “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.” Je, wacheza kandanda wamejiunga na chama chao na kulipa ada za kila mwezi au mpaka wanapopatwa na matatizo ndio wanakumbuka kuwa kuna chama chao cha kuwatetea?

Hata hivyo, ni kama chama cha wacheza kandanda kingali kwenye usingizi mzito kwani hatujaona makucha yake pale wachezaji wanapopunjwa au hata kunyimwa stahiki zao! Hatujasikia kuwaita wanachama (wachezaji) wao kuwaeleza na kuwakumbusha wajibu wao kwa vilabu. Kama chama hicho kipo, mbona hatujasikia hekaheka zake dhidi ya vilabu vinavyowaonea au kuwadhulumu wachezaji wao?

Kwa upande mwingine wachezaji wanapaswa kutambua kuna leo na kesho. Hapana shaka wamesikia au kuona jinsi wachezaji wenzao wanavyohangaika pindi wanapodai fedha za usajili na malimbikizo ya mishahara yao mpaka kupelekana TFF, CAF na FIFA. Kwa hali hiyo wanapaswa kuzinduka na kuona umuhimu wa kujiunga na chama chao.

“Ujinga wa kuuza si ubaradhuli wa kununua.” ‘Ubaradhuli’ ni upumbavu. Ni heri kuwa mjinga wa kuuza kuliko kuwa mjinga wa kununua. Methali hii hutumiwa kuwakumbusha watu umuhimu wa kuwa makini na kutahadhari wakinunuapo au wanapopendezwa na kitu fulani.

[email protected]
0784 334 096