Simba, Yanga zionyeshe ukomavu

16Feb 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Simba, Yanga zionyeshe ukomavu

‘UCHAWI’ ni ufundi wa kutumia dawa au maandishi maalumu ya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe; sihiri. Kitu chochote kinachotumiwa na mganga wa kienyeji kuleta madhara kwa mtu mwingine. Zana zinazotumika kurogea.

‘Ushirikina’ ni tabia ya kuamini uwezo wa kiumbe kingine juu yako badala ya ule wa Mwenyezi Mungu; tabia ya kuamini mambo ya ramli na uchawi.

“Mche Bwana, Mungu wako, ndiye utakayemtumikia … Msifuate miungu mingine.” Wito wa kwanza na dai la haki la Mungu ni kwamba mtu ampokee Yeye na Kumcha. Imeandikwa: “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.”

Amri ya Kwanza ya Mungu inapiga marufuku kuheshimu miungu mingine zaidi ya Bwana mmoja aliyejifunua kwa Taifa lake. Inaharimisha ushirikina na utovu wa dini.

Ushirikina kwa namna fulani huwakilisha upotovu wa dini unaopita kiasi; utovu wa dini ni kasoro ya kutokuwa na fadhila ya kidini. Aidha yalaani ‘dini ya kuabudu miungu mingi.’ Yamtaka mtu kutosadiki na kutoiabudu miungu mingine zaidi ya Mungu mmoja wa kweli.

“Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema. Bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.

“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda.” (Yeremia 17:5-8).

Hapana shaka Simba na Yanga ndizo maarufu zaidi nchini na nnje ya nchi. Ni timu zenye wanachama na mashabiki wengi kuliko timu zingine zote kwani ndizo zilizoanzishwa kwanza mwaka 1935 na 1936 jijini Dar es Salaam. Ni timu zilizoshiriki michezo ya kimataifa mara nyingi zaidi ya timu zingine nchini.

Ushahidi ni wakati huu ambapo Simba imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao, Al Ahly ya Misri na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendeleza mapambano. Twaomba iwe hivyo inshallah!

Timu hizi kongwe nchini zilipaswa kuwa mfano kwa timu zingine, si kwa mchezo mzuri tu, bali pia nidhamu ya mchezo wenyewe na maandalizi yao kabla ya kushindana na timu zingine.

Yasikitisha kuona mambo ni kinyume kabisa kwani zimeweka mbele ushirikina uliokithiri. Matokeo yake timu zingine zote za kandanda, hata zile zinazoitwa za ‘mchangani’ nazo zimefuata mkumbo!

Ushindi husababishwa na mazoezi, kufuata maelekezo ya mwalimu na wachezaji kuwa na nidhamu nnje na ndani ya uwanja. Nidhamu ya nnje maana yake ni kutokuwa walevi wa pombe na dawa za kulevya wala uzinzi (uzinifu, uasherati). Ndani ya uwanja, wachezaji wanatakiwa kucheza kwa nidhamu wakitambua mchezo ni jambo linalofanywa kwa nia ya kuburudisha; sio vita au kulipizana visasi vya nnje na ndani ya uwanja.

Imeandikwa: “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa.

Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” (Mathayo 7:7-11).

Naelekeza kidole cha lawama kwa Shirikisho la Kandanda Nchini (TFF) kwa kutochukua hatua mujarabu (-enye kufaa, mkakati kamili) dhidi ya timu zinazoonesha ushirikina wa waziwazi viwanjani. Kwa mfano, gari la wachezaji linapoingia uwanjani, hukosi kuona vitendo vinavyofanywa na watu wa ‘kamati ya utendaji’ bila kificho kabla ya wachezaji kushuka garini.

Baada ya tukio hilo watu hao wa kamati ya ‘utendaji’ huwaelekeza wachezaji namna ya kushuka wakitanguliwa na mchezaji aliyetayarishwa kufanya hivyo ili anaposhuka afanye nini kabla ya wenzake kushuka na kufanya waliyoam biwa na mwanakamati ya ‘utendaji!’

Wakati mwingine wachezaji hawapitii mlango uliotengwa kwa ajili yao, bali hupitia kwingine. Kadhalika hukataa kuingia kwenye vyumba vyao vya kubadilishia nguo kwa madai kuwa kuna harufu ya dawa iliyopulizwa humo ili wachezaji wa timu pinzani wakivuta hewa ya ndani, walegee wakiwa mchezoni na kuirahisishia timu kupata ushindi kwa urahisi!

Yote hayo hufanyika mbele ya viongozi wa TFF lakini hakuna ufuatiliaji wala hatua yoyote inayochukuliwa dhidi yao. Twajua kuwa viwanja vya mpira hulindwa usiku kucha ili kuzuia wachawi kuingia na kufanya ulozi (tendo la kumpatia mtu shida au hasara kwa uchawi, tendo la kuroga) dhidi ya timu pinzani.

Twataka mwamuzi wa mchezo wa Simba na Yanga aamue haki huku timu zikicheza kiungwana na atakayeshindwa akubali matokeo kwani “Asiyekiri ushinde hakuwa mshindani.”

[email protected]
0784 334 096