Siyo dhambi klabu  zingine zikiiga Simba

04Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Mjadala
Siyo dhambi klabu  zingine zikiiga Simba

JANA klabu ya Simba ilifanya mkutano wake mkuu wa dharura ukiwa na ajenda kuu moja ya kupokea ripoti ya kamati ya zabuni ya klabu hiyo.

Kamati hiyo ambayo ilikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Thomas Mihayo, iliyokuwa na kazi ya  kupokea na kutangaza zabuni ya wanachama wa klabu hiyo ambao walijitokeza kununua hisa za klabu hiyo.

Mkutano huo wa kihistoria ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa zamani wa klabu hiyo, pamoja na viongozi wa serikali ambao mgeni rasmi Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe, aliwakilishwa na Msajili wa Vyama vya Michezo na klabu, Ibrahimu Mkwawa.

Kimsingi jambo ambalo limefanywa na klabu hiyo kongwe nchini linapaswa kuigwa na klabu zingine ili kulipeleka soka letu kwenye mafanikio.

Kuiga jambo jema na lenye mafanikio si dhambi, hivyo kwa klabu nyingine kuiga yale ambayo Simba wameyafanya ni suala la wivu wa maendeleo, ambalo linapendeza zaidi kwa manufaa ya soka letu.

Akisoma hotuba yake kwa niaba ya Waziri Mwakyembe, Mkwawa, alisema serikali haina tatizo na mabadiliko ya klabu hiyo na kusema mambo ambayo yanafanywa na klabu hiyo yanapaswa kuigwa.

Kwa namna mchakato huu wa mabadiliko ya uwendeshwaji wa klabu hii ulivyoendeshwa ni wazi klabu nyingine zinapaswa kuiga kama ilivyosemwa na serikali kuiga jambo jema si dhambi.

Kimsingi Simba imepiga hatua moja kubwa katika kuifanya timu hiyo kujiendesha kisasa na kuipa maendeleo stahiki, hakuna ubishi kuwa maendeleo kisoka yameiacha klabu hii yenye umri wa zaidi ya miaka 80 mbali sana.

Kwa umri wa klabu ya Simba, ilipaswa kuwa mbali kimaendeleo kama zilivyo timu nyingine kubwa barani Afrika; TP Mazembe, Kaizer Chief au Zamaleki, lakini kwa bahati mbaya klabu hii kama zilivyo zingine kongwe nchini zimechelewa kutokana na wachache kulenga kujinufaisha wenyewe.

Lalini si mbaya kuchelewa, cha msingi ni kufika hatua hiyo muhimu pamoja na kuona imechelewa kufikia maendeleo, bado imeendelea kupambaana na kujikongoja katika safari hiyo ndefu, na sasa mwanga wa kufika zilipo klabu kubwa Ulaya umeanza kuonekana.

Hakika Simba ilipofikia, imeonyesha kweli ina nia ya kufika kwenye mafanikio, nia hiyo imeonekana si kwa viongozi pekee bali pia kwa wanachama wa klabu hiyo ambao walijotokeza kwa wingi katika mkutano wa Agosti 8, mwaka huu pamoja na huo wa  jana wa kutangazwa mshindi wa zabuni.

Kilichofanywa na Simba kinapaswa kuigwa na klabu zingine, soka la sasa linaendeshwa kisasa na hakuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio.

Suala linalofanywa sasa na uongozi na wanachama wa klabu ya Simba, tayari wenzetu waliopo juu kwenye maendeleo ya soka wameyafanya miaka mingi iliyopita.

Sio jambo baya wengine kuiga mchakato huu uliofanywa na Simba mpaka kufikia sehemu ya kupata mwekezaji wake ambaye atasaidia kuiendesha timu hii katika misingi ya kisasa.

Mafanikio ya soka kwa taifa lolote hutokana na uimara mkubwa wa klabu za ndani ya nchi, kuendeshwa kisasa.Simba inastahili pongezi kwa uthubutu wake na kujaribu kufanya mabadiliko ya uwendeshwaji mpya wa klabu hiyo ambao jana ulifikia kilele kwa kutangazwa mshindi wa tenda ya kununua hisa za klabu hiyo, mfanyabiashara Mohamed Dewji maarufu kama "MO".