Stars ijipange kwa Lesotho ikikumbuka ya Tico-Tico

22Oct 2018
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Stars ijipange kwa Lesotho ikikumbuka ya Tico-Tico

BINADAMU hujifunza kutokana na makosa. Kufanya kosa ni asili ya binadamu. Lakini mara nyingi binadamu anafundishwa jinsi gani ya kutorudia kufanya kosa lile lile alilolifanya mwanzo.

Iwapo litakuwa likirudiwa mara kwa mara, basi inakuwa si kosa la bahati mbaya bali ni uzembe, kutokuwa na umakini au vyote kwa pamoja.

Tanzania imefufua matumaini ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon kufuata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa Kundi L. Ushindi huo wa kwanza kwenye mashindano haya, unaifanya Taifa Stars ijisogeze hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili.

Tanzania inahitaji kushinda mechi mbili tu zilizobaki ili kufuzu bila kuangalia matokeo ya mechi nyingine.

Wakati Watanzania wote akili na ndoto zao ziko Cameroon mwakani, nawatahadhalisha kuwa bado shughuli ni pevu katika Kundi L na huu si wakati wa kuanza shangwe, sherehe, maandalizi ya kushiriki AFCON ambayo hatujafuzu.

Bali huu ni wakati wa kuweka mipango ya kukusanya pointi katika mechi mbili zijazo, tukifikiria ugumu uliopo mbele yetu.

Leo hii Watanzania wengi wanaona au wanaamini wana kazi nyepesi sana kuelelea AFCON baada ya kushinda mechi moja tu, wakati hao Uganda walioshinda mechi tatu wanaihisi shughuli pevu iliyopo mbele yao na bado wanajipanga kisawasawa.

Tunaona ni kazi nyepesi kuifunga Lesotho kule Maseru, tu kwa sababu imefungwa na Uganda pale pale, lakini hatujiulizi hiyo ndiyo timu ambayo tulishindwa kuifunga hapa nyumbani kwetu.

Mawazo kama haya ndiyo yalitufanya tukafungwa 3-0 na Cape Verde katika mechi ambayo tungeweza japo kupata sare kama tungecheza kwa nidhamu iliyostahili.

Kujiamini kupita kiasi na kuona kama kazi imekamilika, ndiko kulikoifanya Stars ishindwe kufuzu AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana.

Ilikuwa ni Septemba 8, 2007 wiki moja tu baada ya Uwanja wa Taifa kufunguliwa ikawa siku ya majonzi kwa Watanzania tuliposhindwa kufuzu, baada ya kufungwa nyumbani bao 1-0 na timu ya Taifa ya Msumbiji, bao likifungwa na Manuel Bucuane maarufu kama Tico-Tico dakika ya nane tu na kuwaacha Wabongo na kilio na kumbukumbu isiyofutika hadi leo kwa sababu ilihitajika sare tu ili Stars ifuzu.

Kwa maana hiyo Watanzania hasa wachezaji, makocha na hata viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ni wakati wa kuwa makini mno, ili lisijirudie tena jinamizi kama la wakati ule.

Ndiyo maana mwanzo nilisema kuwa kufanya kosa si kosa ila kosa ni kurudia kosa.