Stars ijipime na nchi zilizotuzidi viwango

04Sep 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Stars ijipime na nchi zilizotuzidi viwango

TIMU ya Taifa ‘Taifa Stars’ juzi ilicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Taifa Stars ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku yote yakifungwa na Simon Msuva anayecheza soka la kulipwa nchini Morocco.

Taifa Stars ambayo inashika nafasi ya 120 kwenye viwango vya ubora wa soka vinavyotolewa na Shirikisho la Soka duniani (Fifa), ilicheza na Botswana ambao wenyewe wanashika nafasi ya 140.

Pamoja na Taifa Stars kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo, bado kiuhalisia, Botswana hakikuwa kipimo sahihi cha Taifa Stars kwa mechi hizo zinazotambulika na Fifa kwa kuwa zinaangukia kwenye kalenda ya shirikisho hilo.

Tunahitaji kuona Tanzania ikipanda kwenye viwango vya ubora kutoka hapa tulipo sasa na kusonga mbele zaidi kama tunavyoona kinachotokea kwa majirani zetu, Uganda.

Na hilo ni lengo la Shirikisho la Soka nchini (TFF), chini ya uongozi mpya, ambao unataka kuona Tanzania tukipanda kwenye viwango vya ubora vya Fifa.

Lakini kwa kucheza na timu tulizozidi ubora si kipimo sahihi au daraja sahihi la kutupandisha juu kwenye viwango hivyo.

Ni vyema sasa TFF ikajipanga kwa kutafuta mechi za kirafiki na timu zilizojuu yetu, hususan kutoka nchi za Afrika Magharibi na Afrika Kaskazini ambazo zimetuacha mbali kwenye viwango hivyo.

Kama tutakuwa tunacheza na timu hizo na kupata matokeo mazuri ni wazi tutakuwa tunakusanya pointi nyingi ambazo zinaweza zikatupandisha juu zaidi kwenye viwango vya Fifa.

Ni wazi kuwa kucheza na timu ambazo tumeziacha kwenye viwango vya ubora hakutupi pointi nyingi kama ambavyo tungecheza na timu zilizopo juu katika orodha ya viwango vya ubora na kushinda.

Ni vyema sasa kwa TFF kuliangalia hili kama kweli tunataka kuona tukipanda kwenye viwango vya ubora vya Fifa kama ambavyo kila Mtanzania angependa kuona hilo likitokea.

Lakini pia kwa kasi na uwezo ambao Taifa Stars imeonyesha tangu iliposhiriki michuano ya Cosafa, ni vyema TFF kuhakikisha kila tarehe ya Fifa kwa michezo ya kirafiki inapofika, kapata timu ya kucheza nayo.

Tusikubali kuona tarehe ya Fifa inapita bila kuwapo kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki kwa Taifa Stars. Kwani michezo hii ndio inayotumiwa na Fifa nakupanga viwango vya ubora.

Kutocheza mchezo wowote kwa tarehe hizi kunaifanya nchi yetu kuporomoka kwenye viwango.

Tunataka kuona siku moja Tanzania inakuwa kwenye viwango vya ubora kwenye tarakimu mbili kama ilivyotokea miaka ya nyuma kipindi cha kocha Marcio Maximo wakati akiinoa Taifa Stars.

Tayari kocha wa sasa wa Taifa Stars, Salum Mayanga, ametangaza kikosi chake kitakachocheza mchezo mwingine wa kirafiki Novemba mwaka huu.

TFF ijitahidii kuhakikisha timu tutakayocheza nayo ipo juu zaidi yetu katika viwango vya ubora vinavyotolewa na Fifa ili kujitengenezea mazingira ya kupanda katika viwango hivyo.