Stars iungwe mkono kwa matokeo yoyote inayopata

24Jun 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Stars iungwe mkono kwa matokeo yoyote inayopata

JANA Taifa Stars ilitupa karata yake ya kwanza kwenye michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, dhidi ya Senegal katika mechi iliyochezwa saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Timu hiyo ya Tanzania itakuwa na mechi zingine mbili dhidi ya Algeria na Kenya kwenye fainali hizo za Afcon zinazoendelea nchini Misri.

Na kama Stars ikifanya vizuri kwenye mechi hizo, basi itafuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa ngazi ya timu za taifa barani Afrika.

Wala nisipepese macho kusema kuwa Watanzania wengi hasa unapopita mitaani na kwenye mitandao ya kijamii wamegawanyika kuhusu timu yao ya taifa. Wa kwanza ni wale wazalendo ambao wao hawajali kama timu inapewa kipaumbele kushinda au la.

Wao ni Tanzania kwanza, wanachoishangilia ni timu yao ya taifa kwa hali na mali, na kwa matokeo yoyote yale yatakayotokea wao wako na timu yao tu. Ikifuzu watashangilia na kama haikufuzu wala hawatoona vibaya kwa sababu ni timu yao.

Kundi la pili ni wale wenye nongwa. Hawa wanachotaka au kuombea ni Stars kufungwa ili waanze kumnanga kocha Emmanuel Amunike kwa sababu zao tu za kuacha wachezaji ambao wao waliona wanafaa kuichezea, au wachezaji wanaowapenda wao.

Kundi la tatu ni wale ambao hawana uhakika na timu ya Tanzania kama inaweza kufanya vizuri au la.

Wanachofanya kwanza ni kuangalia kama itashinda na ikiwa hivyo basi watashangilia na kujifanya wao ndiyo mashabiki namba moja. Lakini kama timu ikipoteza basi wao ndiyo watakaoanza kutoa lawama kwa makocha, wachezaji na kila mtu ambaye wanaona anahusika kwenye kikosi hicho cha Taifa Stars. Hata hivyo makundi haya yote ni mashabiki wa timu ya taifa na ni Watanzania.

Ukiangalia katika makundi haya matatu, kundi linalotakiwa kuwa mfano wa kuigwa ni lile la kwanza. Kundi la pili na la tatu, wote wanatakiwa kuiga mfano wa kundi la kwanza la kuwa Watanzania kwanza.

Kama ni Mtanzania huwezi kuwa chochote kile zaidi ya hicho. Hata kama timu haitofanya vema basi kinachotakiwa ni kusikitika, lakini ukiendelea kuwa Mtanzania na si kuanza kulaumu na kutupia lawama watu.

Nasema hili kwa sababu mara nyingi kuna mazoea yamejengeka kuwa Stars ikishinda timu inakuwa ni ya wote. Ni ya Watanzania wote, huku kila mmoja akijiona ni mhusika wa mafanikio hayo.

Pongezi kwenda kwa wachezaji, makocha na hata Shirikisho la Soka nchini (TFF), zinakuwa hafifu, badala yake watu wanashangilia tu kana kwamba ushindi umeletwa hivi hivi. Inapokuwa kinyume chake sasa, mzigo anatupiwa kocha, wachezaji wa TFF.

Si kama kusiwe na ukosoaji kama timu inafanya vibaya. Ni lazima watu waseme tatizo liko wapi. Tatizo ni pale ukosoaji huo hauwi wa kujenga, bali ni kama kusuta, kushutumu na kuhukumu.

Binafsi, kwa hapa Stars ilipofikia ni mafanikio makubwa kwenye soka la nchi yetu, kwani baada ya miaka 39, timu hiyo imefuzu na inacheza michuano hiyo baada ya miaka 40.

Kwa maana hiyo naona kuingia kwa mara ya kwanza baada ya miaka hiyo ni kwenda kusaka uzoefu na si kuwaweka wachezaji roho juu na kujiaminisha kuwa wanatakiwa kulitwaa kombe hilo au kufika nusu fainali.

Ni kama Klabu ya Simba ilivyofanya mwaka huu kuwa lengo lake ilikuwa ni kutinga makundi, hivyo kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa ni kuvuka malengo waliyojiwekea.

Stars nayo ni hivyo hivyo, lengo lilikuwa ni kufuzu AFCON na tayari imefanya hivyo, hivyo hakuna sababu ya kuihukumu pale kwa bahati mbaya itakaposhindwa kufuzu kwenda hatua inayofuata.

Na kama ikifanikiwa basi itakuwa imevuka malengo na hakuna haja ya kumshika mtu uchawi.

Kwa sasa Watanzania wote wapenzi wa soka wanatakiwa kuungana na kuwa kitu kimoja kuiombea Taifa Stars ifanye vema, lakini pia kukubali matokeo yoyote yale yatakayotokea bila kushusha lawama zisizo na msingi. Ikishinda tufurahi wote na ikifungwa tuhuzunike wote.