Stars kutofuzu AFCON, mengi yamechangia

29Mar 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Stars kutofuzu AFCON, mengi yamechangia

HIVI sasa kila mmoja anazungumza lake juu ya timu ya Taifa ya Tanzania kushindwa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON). Ni michuano inayotarajiwa kuchezwa Januari hadi Februari mwakani nchini Cameroon.

Alhamisi iliyopita, Taifa Stars ilizima ndoto za kutaka kucheza fainali hizo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuchapwa mabao 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea ikiwa ugenini.

Tanzania ilifuzu kucheza michuano hiyo mwaka 2019 ilipocheza fainali hizo nchini Misri baada ya miaka 40.

Kwenye Kundi la J, Stars ilikuwa pamoja na Tunisia na Equatorial Guinea ambazo zimefuzu huku yenyewe na Libya ndoto zao zikiyeyuka. Hata hivyo kushindwa kufuzu AFCON kwa Stars kumepokelea kwa hisia tofauti na mashabiki wa soka nchini.

Lakini baadhi yao wanaonekana kushangaza kwa kile ambacho wao wanaona kimesababisha Stars ishindwe kusonga mbele. Kuna wanaosema uchaguzi wa wachezaji wa timu ya taifa haukuwa mzuri.

Pia wapo wanaodai kuna baadhi ya wachezaji ambao wana uwezo wa kuichezea timu ya taifa hawakuitwa na badala yake wakachukuliwa baadhi ya wachezaji ambao uwezo wao ni wa kawaida tu, au unaotia shaka.

Wengine wanadai kuwa mfumo uliotumika kwenye mechi hiyo haukuwa rafiki kwa wachezaji. Mashabiki wengine wamewatuhumu nahodha Mbwana Samatta na mwenzake Simon Msuva ambao ndiyo tegemeo kwenye kikosi cha Taifa Stars kuwa hawakuwa kwenye viwango vya bora vilivyozoeleka, wakieleza walicheza chini ya kiwango.

Watanzania wengine wanadai hakukuwa na muunganiko baina ya viungo washambuliaji na washambuliaji. Ilijaza viungo wakabaji wengi, Mzamiri Yassin, Jonas Mkude na Feisal Salum, wote wakiwa na tabia ya kukaba, na hakuna yeyote aliyekuwa anawalisha washambuliaji.

Wapo walioenda mbali zaidi na kudai eti Stars imefungwa kwa sababu tu ilijaza wachezaji wengi wa klabu ya Simba. Ili mradi tu kila mmoja anasema lake. Lakini ukweli unabaki pale pale tu, Taifa Stars haina hati miliki ya kucheza Fainali za AFCON.

Kuna nchi au mataifa makubwa ambayo yako juu kimpira, lakini yameshindwa kutinga fainali hizo, achilia mbali Tanzania. Timu ya taifa, ina matatizo mengi mno ya msingi na wala hakuna hata moja kati ya hilo ambalo mashabiki wamekuwa wakidai.

Ni maoni yao na mawazo yao, lazima yaheshimiwe, lakini ukirudi nyuma ni kwamba Watanzania tuna matatizo ya msingi kwenye soka letu, lakini tumekuwa na tabia ya kulaumu tunakoangukia tu.

Kuna nchi ambazo zimetuzidi soka na hata viwango zimeshindwa kufuzu kama DR Congo, Angola, Togo na hata Zambia, zote hizi zimeambulia patupu. Cha kusangaza nchi kama Comoro ambayo ilikuwa inafungwa mabao mpaka 15-0 na Tanzania miaka ya 1990, imefuzu AFCON.

Tatizo letu kubwa ni kwamba hatuna mipango mizuri ya uzalishaji vijana, pamoja na mafuzo ya uhakika kwa wachezaji wadogo tangu awali. Ndiyo maana wachezaji wa Kitanzania ili uwaone wanacheza vizuri ni lazima wawe wamezungukwa na nyota wa kigeni. Wakibaki wenyewe ndicho hicho kinachoonekana.

Matatizo mengine yapo nje kabisa ya uwezo wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), na hata benchi la ufundi.

Nchi kama Equtorial Guinea ilikuwa na wachezaji wengi wanaocheza ligi mbalimbali Hispania na wenye uraia wa nchi mbili, Hispania na Equatorial Guinea. Hata Comoro imekuwa juu kwa sasa kwa sababu wachezaji wao wengi ni raia wa Comoro na Ufaransa, wakicheza ligi mbalimbali za huko.

Watanzania tuna wachezaji wengi nchi za nje ambao wazazi wao wamezaliwa Bongo, kina Yusuph Poulsen wa Denmark na wengine wengi wanaotaka kuichezea Stars, lakini wanatatizwa tu na kutokuwapo kwa uraia wa nchi mbili.

Nchi nyingi za Afrika kwa sasa wanatumia hilo ili kuwapata wachezaji wenye asili yao waliopo nje na wamekuwa wakizisaidia sana.

Tanzania tusipobadilika na kufanya hivyo, angalau kwa wanamichezo tu, basi tutaendelea kushikana uchawi, kufukuza makocha, kutiana vidole vya macho na kusutana, huku ukweli tukiwa tumeuweka mfukoni.