Suala la taulo za mabinti, tuzame kujua ya shuleni

13Mar 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Suala la taulo za mabinti, tuzame kujua ya shuleni

MTOTO wa kike anakumbana na changamoto ambazo zinaanzia nyumbani au shule. Ni hali inayochangia hata kushindwa kusoma vizuri au kutohudhuria vipindi darasani.

Ni changamoto inayoweza kumkuta mtoto wa kike, anatumikishwa kazi nyingo pasipo kuwa na fursa ya kupumzika, hali inayochangia asiweze kujisomea kwa usahihi, sababu kuu ni kukosa muda sahihi wa kufanya hayo muhimu katika talauma, ndani ya muda muafaka.

Iko bayana, kuwapo changamoto nyingine inayohusiana na hilo, ni binti anapokuwa kwenye hedhi, anaweza akawa amepatiwa taulo la kujisitiri, lakini shule anayosoma haina maji au inakosa chumba maalumu cha kumhudumia.

Ni hali inayoyosababisha mtoto kushindwa kuhudhuria masomo, kutokana na kukosa chumba au maji na anapokuwa katika siku hedhi, analazimika kubaki nyumbani, ili aweze kujihudumia vizuri na anaporejea hali ya kawaida, anarudi shuleni kuendelea na masomo kama kawaida.

Imo katika kinachosababisha watoto wasihudhurie masomo, kwa kukosa maji au kutokuwapo vyumba vya kujisitiri katika shule zao.

Katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, asasi ya TGNP Mtandao iliandaa maadhimisho kwa kushirikiana na vituo 14 vya Taarifa na Maarifa vilivyopo katika Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Hapo, baadhi ya wanafunzi walishiriki katika maadhimisho na walitumia nafasi husika kutoa yao ya moyoni.

Walisema kwa nyakati tofauti kuwa, wanakumbana na changamoto ya kushindwa kuhudhuria masomo kutokana na shule zao kutokuwa na miundombinu ya maji.

Anasema, mmoja wa wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Mabibo jijini Dar es Salaam, kuwa shule yao haina maji ya uhakika na watoto wa kike wanapoingia katika hedhi, wanakosa maji, ni sababu inayomfanya ashindwe kuhudhuria masomo.

Niseme kuwa ni jambo jema mabinti hao wanapewa taulo, lakini kuna sura ya pili, bado tatizo lipo katika suala la upatikanaji maji. Kwa kweli, ni changamoto!

Ushauri wake ni kwamba, kinachotakiwa sasa kuangaliwa ni umuhimu wa shule zikawa na maji ya kutosha, ili wasichana hao wanapokuwa katika hedhi, iwepo huduma kwao ya kiafya na utetezi wa nafsi binafsi

Husna Said, ni mwanafunzi wa chuo kimoja akipata mafunzo ya ufundi umeme, jijini Dar es Salaam, anasema katika kumtambua mwanamke masomoni, pia wakumbukwe wasichana walio nje ya shule.

Anasema kuwa, wapo wasichana wanaoishia darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo, lakini wanapokumbana na changamoto, matatizo yao wanabaki njia panda, nani wa kumwambia?

Kwa mujibu wa Husna, haki mara nyingi inapigiwa kelele kwa mabinti walio masomoni na kuwaacha njia panda, walio nje ya masomo, hawana mwelekeo kamili, upande upi atapaza sauti yake.

Anasema watoto wengi wanapotea kimaisha, kupitia changamoto zinazoanzia majumbani. Ni aina ya mtazamo inaoibua haja ya utetezi kutoka kwa watoto, unaoweza kufanywa, ingawa najua katika baadhi ya maeneo umeanza, watembelewe mitaa,wasikilize na kutatuliwa kero zao, hiyo ndio sehemu ya utekelezaji sahihi wa haki ya mwanamke.