Taifa Stars moja, makocha milioni moja!

25Jan 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Taifa Stars moja, makocha milioni moja!

AFADHALI sasa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, atapumua na kupumzika kutoka kwenye midomo ya baadhi ya watu ambao walikuwa wanataka atimuliwe.

Hii ni baada ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia kwenye mechi ya kwanza ya Kundi D, ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zinazoendelea nchini Cameroon.

Ushindi wa bao 1-0 ilioupata dhidi ya Namibia Jumamosi usiku, umeifanya timu hiyo si tu kujizolea pointi tatu na kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali, lakini yamewafanya wale wote ambao walikuwa wameshaanza kumnyooshea kidole cha shahada kocha huyo, sasa kunyamaza.

Baada ya kipigo, baadhi ya mashabiki, waandishi wa habari za michezo, na wachambuzi, walishaanza kusema kuwa kocha huyo hafai.

Ni kocha huyu huyu ambaye ndiye ameipeleka Stars kwenye fainali za CHAN ndiye leo anaambiwa hafai. Na ukisikiliza sababu unaambiwa kuwa hakuchagua kikosi kizuri cha kwenda nacho CHAN. Wengine wanasema ana kikosi kizuri, lakini anakosea kukipanga na wapo ambao hawana hata sababu, wao wanasema tu hafai.

Kuna mashabiki wako tofauti na Ndayiragije kwa sababu tu hakuwachagua baadhi ya wachezaji ambao wao wanaona wanafaa kuichezea timu ya taifa. Hili ndilo tatizo la baadhi ya mashabiki wa soka Tanzania na wachambuzi wa masuala ya michezo.

Taifa Stars inapofungwa mara nyingi hazitolewi sababu za kitaalam, au za msingi kabisa za soka letu, badala yake zinakuwa ni za kishabiki na kisiasa zaidi. Wakati mwingine Stars inaweza kufungwa tu kwa sababu imezidiwa kwa kukutana na timu bora au kwa siku hiyo imekuwa bora kuliko Stars, lakini watu hawataki kukubali ukweli huo.

Sidhani kama leo Watanzania tumekuwa na timu imara ambayo haitakiwi kufungwa kwenye michuano yoyote ile.

Na hata kama Stars ikishinda, basi si kwamba tuna timu imara sana, ila wakati mwingine mbinu za benchi la ufundi kwa siku hiyo zimefanya kazi nzuri, au tumekutana na timu ambayo tumeizidi kiwango kwa siku hiyo.

Hakuna sababu yoyote ya Stars kufungwa basi tatizo liwe kwa kocha Ndayiragije. Stars imefundishwa na makocha wengi sana na wameondoka, lakini bado matatizo ni yale yale. Hakuna kocha yeyote atakayekuja na kuleta miujiza kama Stars itakuwa na aina ya wachezaji wale wale ambao leo wanacheza vema, lakini kesho wanacheza vibaya.

Mashabiki wengi wa Tanzania wanakwepa sababu za msingi kuwa wachezaji wetu hawajaandaliwa kuwa wanasoka, hasa wa kulipwa, ndiyo maana mchezaji wa Ligi Kuu wakati mwingine hata kutuliza mpira anashindwa, lakini pia baadhi wanashindwa hata kulinda viwango vyao.

Mara nyingi sababu za Watanzania utasikia kocha mbaya, kocha anabagua wachezaji, hawezi kupanga kikosi, hajaita wachezaji fulani. Na wengine wanakwenda mbali kabisa na kusema ili Tanzania iwe na timu nzuri ya taifa ni lazima wapunguzwe wachezaji wa kigeni nchini.

Hata hivyo, ukiangalia mechi zote mbili za Stars, utaona kwa kiasi kikubwa wachezaji wa Kitanzania wameshaondoa hofu ya kucheza na wachezaji wageni kwa sababu kwenye ligi yao kuna wachezaji wengi kutoka mataifa tofauti.

Kwa maana hiyo, kuwapo kwa wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu, kunawafanya wachezaji wetu sasa wacheze kwa kujiamini.

Tatizo ni moja tu, wakati mwingine wanazidiwa uwezo tu wa mchezaji mmoja mmoja na wachezaji wa timu zingine. Inawezekana wakosoaji wakaibuka tena Jumatano kwenye mechi dhidi ya Guinea, ingawa hatuombei hilo litokee.

Hapa nataka kusema mambo ya ufundi tumuachie kocha mwenyewe. Stars ina kocha mmoja tu ambaye ni Ndayiragije, wengine wote tubaki kuwa washangiliaji na timu ikipata matokeo ya aina yoyote tuwe tumefungwa wote na si kumtupia lawama kocha, kwa sababu wachezaji Stars ni hawa hawa, hakuna wengine wenye viwango vya juu zaidi hapa Tanzania kuliko hawa waliokuwapo.