Tamba uone kama hukutamba…

18Jan 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tamba uone kama hukutamba…

NAAM, “Tamba uone kama hukutamba huna uonacho.” Maana yake zunguka ulimwenguni ujionee mambo usiyoyajua. Hutumiwa kuwahimiza watu wetembee na kujikusanyia maarifa wasiishie kudhani wanayajua yote kumbe hawana wajualo.

Aidha, wahenga walisema: “Gogo la m-buyu si la mvule.” Maana yake pande la m-buyu ambao ni mti mnene si sawa na la mvule ambao ni mgumu na hauliwi na mchwa.”

Methali hii yaweza kupigiwa mfano wa watu wawili tofauti; mmoja mkubwa, lakini asiyeitumia akili; na mdogo ambaye anaitumia akili yake.

Kabla ya mechi ya Simba na Yanga ambayo sasa yaitwa ‘timu ya wananchi’, (kwani Simba ni timu ya wakimbizi?) mchezaji Said Ndemla wa Simba alisema siku chache kabla ya mechi hiyo kwamba: “Yanga hawana ubavu wa kupata pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.”

Akihojiwa na moja ya magazeti ya michezo nchini, mchezaji huyo alisema hawakosi usingizi kwa mchezo huo kwani wamejipanga kuondoka na ushindi.

Akaendelea: “Kwa ujumla kila mchezaji wa kikosi chetu hana hofu na Yanga hata kidogo na matumaini yetu ni ushindi. Tunajiandaa kuifunga Yanga kwa mbinu za kocha wetu Mbelgiji, Sven Vandenbroeck,” Ndemla alinukuliwa kusema hivyo bila kujua kabumbu mara nyingine huwa mchezo wa bahati.

Haieleweki Ndemla alijisikiaje wakati Simba ikiwa mbele ya Yanga kwa mabao mawili bila; lakini Yanga ikasawazisha yote kipindi cha pili na mchezo kumalizika kwa sare ya 2-2.

Haikuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kushangazana. Mara ya kwanza Yanga iliifunga Simba mabao 3-0 ya kipindi cha kwanza, lakini Simba ilirejesha yote kipindi cha pili kuwa 3-3 hata kuufanya uso wa Abdallah Kibadeni aliyekuwa kocha wao ukunjuke baada ya kuwa umetuna kwa wasiwasi!

Mwandishi mwingine wa gazeti ninalolijadili akaandika: “Kwa jeshi hili, wengi watazimia. Kazi ipo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwani benchi la ufundi la Yanga limepanga kufanya ‘surprise’ ya aina yake kwa kupanga jeshi la mauaji litakaloivaa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania.”

Sikumbuki kusikia kuna watu waliozimia Uwanja wa Taifa wakati na baada ya mechi ya Simba na Yanga. Ingekuwa hivyo baada ya Simba kuongoza kwa mabao mawili mpaka kipindi cha pili. Kwa hiyo mashabiki wa Yanga wangezimia kwa kutoamini macho yao!
Kadhalika, ingekuwa hivyo kwa mashabiki wa Simba baada ya Yanga kusawazisha mabao yote mawili kwa muda mfupi na mchezo kumalizika kwa kufungana 2-2. Pengine mwandishi alipatia alipoandika “ … benchi la ufundi la Yanga limepanga kufanya ‘surprise’ (mshangao) ya aina yake …”

Wakati Simba ikiwafunga Yanga mabao mawili, moja katika kila kipindi, Yanga ilifaulu kusawazisha mabao yote mawili kwa muda usiozidi dakika saba kipindi cha pili.

Tumeona au kusikia timu ngumu na maarufu duniani zikifungwa na timu dhaifu na kuwaacha wapenzi wao kwenye mshangao mkubwa. Timu kama Manchester United, Manchester City, Barcelona, Real Madrid n.k. hufungwa na timu zisizotarajiwa na kuwashangaza wengi! Ndio maana husemwa ‘mpira hudunda.’

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza, aliwaambia waandishi wa habari siku mbili kabla ya kupambana na Yanga kuwa mchezo huo utatoa sura ya ubingwa kwao kwani watacheza na timu kubwa ambayo ndio wapinzani wao katika mbio za ubingwa.

Akasema: “Mwaka 2020 tunaanza na Yanga. Ni mchezo mgumu, lakini tunahitaji matokeo mazuri ili tuendelee kupambana kutwaa ubingwa msimu wa 2019/2020. Tukishinda tutakuwa na asilimia kubwa ya kutwaa kombe.”

Kabla ya mechi baina ya Simba na Mtibwa Sugar kugombea Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar, Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema:

“Tuna historia nzuri ya kupata ushindi tunapokutana na Mtibwa, ni timu yenye ushindani, lakini na sisi tunajipanga kukabiliana nayo na kuishinda. Tutapambana kuhakikisha ubingwa unakuwa wetu, hii itatusaidia pia kwenye ligi kuendeleza moto wa mapambano.”

Kichwa cha habari hiyo kiliandikwa: “Matola: Simba ni baba kwa Mtibwa” lakini habari ya paragrafu 10 chini ya kichwa hicho sikusoma popote palipoandikwa Matola kasema ‘Simba ni baba kwa Mtibwa!”

Hata hivyo, Mtibwa Sugar ilipopambana na Yanga jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya Ligi Kuu, Mtibwa ilicheza soka la kufundishwa wakiambaa uwanja mzima kwa pasi za hapa na pale huku wenzao wakitafuta gozi la ng’ombe kwa ‘taa!’

Hakika Mtibwa walikuwa wazuri kimchezo kuliko Yanga hata kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga. Baadhi ya mashabiki wa Yanga wasiokuwa na uvumilivu waliondoka kabla ya mchezo kufikia ukomo huku waliobaki wakijishika matama.

Hii yathibitisha kuwa kila timu iingiapo uwanjani huwa na lengo la ushindi, si kushindwa. Kwa kuwa Ligi Kuu ina timu 20, kila moja inacheza ili kutwaa kombe na kucheza na timu za nje ya nchi.

Pia kila moja inajitahidi kubaki kwenye Ligi Kuu kwani msimu ujao timu zitapunguzwa. Nani asiyetaka kujua nchi mbalimbali za Afrika badala ya kuzisikia tu?

Kabla ya kupambana usitoe maneno ya dharau dhidi ya mwenzako. Ilisemwa “mwenye kelele hana neno.” Maana yake aghalabu mtu anayepiga kelele huwa hana madhara yoyote.

Hutumiwa kutukumbusha kuwa hatupaswi kumwogopa mtu mwenye kelele au fujo kwa kuwa kwa kawaida hana neno.
[email protected]
0784 334 096