Tamko la Maalim Seif na hatari iliyopo Zanzibar

13Apr 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Tamko la Maalim Seif na hatari iliyopo Zanzibar

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetoa tamko linalojiekeleza katika `msimamo mkuu’ wa chama hicho baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20.

Likisomwa na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyewania Urais wa Zanzibar na kuamini (hata sasa) kwamba alishinda, tamko hilo linajijenga katika ‘sura’ tatu.

Moja ni kwamba linawahimiza Watanzania wa Zanzibar kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kuwapo nchini, licha ya ‘kuporwa’ kwa ushindi anaoamini kuupata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

Pili ni tamko linalofungua mlango kwa wanaoamini kuwa Maalim Seif na CUF ilishinda katika uchaguzi huo, lakini ‘wakaporwa’ kwa hila zilizoongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, waanze kudai haki yao.

Tatu ni kuhimiza mamlaka za kikanda na kimataifa, kuwadhibiti viongozi wa serikali ya Dk. Shein, ikiwamo kuzuiliwa kusafiri nje (bila shaka ni katika nchi za Magharibi) na kukaguliwa kwa akaunti zinazodaiwa kuwa nje ya nchi.

Akijifungamanisha na matamko 13 ya Baraza Kuu la CUF, Maalim Seif akasema hiyo ni sehemu ya mikakati madhubuti ya kutekeleza kwa kutumia njia za amani, demokrasia na kikatiba ili kuwafikisha katika malengo ya kuona uamuzi wa Wazanzibar unaheshimiwa.

Uamuzi anaouzungumzia Maalif Seif na kwamba unapaswa kuheshimiwa ni `ushindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana’.

Sitaki kuingia kwa undani kuhusu maazimio 13 ya Baraza Kuu la CUF, lakini kama kuna mtu ninayeweza kumshangaa, ni yule atakayeamini kwamba licha ya tamko hilo, Zanzibar itaendele kuwa katika amani na utulivu wa kweli.

Sitaki kuamini hivyo kwa maana tamko la Maalim Seif limetangulizwa mbele ya maelfu ya wanachama na wafuasi wa chama hicho chenye nguvu kubwa ya kisiasa Zanzibar, licha ya kususia kwake uchaguzi wa marudio.

CUF ni chama kilichojijenga kwa mifumo tofauti inayokifanya kiendeshe shughuli zake kwa kadri inavyokusudiwa, huku kikitambua umuhimu na msingi wa kuweka mbele maslahi ya taifa.

Ndivyo ilivyo kwa vyama vingine vinavyoaminika na kuungwa mkono kama CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi na vingine vilivyo kwenye orodha ya msajili wa vyama vya siasa nchini.

Lakini inapotokea CUF kupitia kwa Maalim Seif kikaanza mkakati wa kuwahamasisha wananchi kushiriki mikakati ya kudai ‘haki ya Oktoba 25, mwaka huu’, Taifa halipaswi kupuuza. Tujadili.

Wakati huo dunia ikitambua kwamba tayari `matokeo ya Machi 20, mwaka huu’ yalitumika kumuapisha Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, hali inayoashiria kuibuka kwa upinzani usiokuwa na tija visiwani Zanzibar.

Wakati wa mzozo kuhusu kurejewa ama kutorejewa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, niliwahi kuandika makala, nikitahadharisha kwamba eneo hilo la Muungano lisiachwe mithili ya shamba la nafasi lililotelekezwa wanapopatikana nyani.

Kwa maana nyani wanapoachiwa shamba la namna hiyo, mathalani mahindi, wakiachwa kwa muda, basi kitakachofuatia ni kuokota mabua, mahindi yatakuwa yameliwa isivyostahili.

Tafsiri yake kubwa ilikuwa ni kuhumiza umuhimu wa kuwaleta pamoja Watanzania katika kujadili na kupata suluhu ya kudumu na yenye tija katika mzozo wa kisiasa ulioanza kujitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, mwaka jana.

Sasa baada ya tahadhali hiyo iliyojenga hoja kwa kuzielekea pande zote hasa za CCM na CUF wanaoungwa mkono na sehemu kubwa ya kizazi cha Zanzibar, hali haikuwa hivyo.

Vikao vilivyofanyika havikufikia maelewano isipokuwa tangazo ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio uliomuwezesha Rais Shein kuweka historia inayoweza kuishi miaka mingi kwa kupata ushindi wa asilimia 91.4.

Ni ushindi unaopingwa na baadhi ya watu wakiuona kwamba ‘ulipikwa’, dhana ambayo ipo kwa baadhi ya mataifa makubwa yaliyo washirika wa maendeleo wa Tanzania. Katikati ya hali hiyo, Watanzania wa Zanzibar wanahimizwa kushiriki mikakati ya kudai haki yao.

Kwa namna yoyote ni kutaka matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana yawe kigezo cha kumpata Rais watakayemtambua, licha ya ukweli usiopingika kwamba kwa mujibu wa Katibu, Rais ameshapatikana, ndiye Dk. Shein.

Ikimbukwe kwamba tafsiri ya kudai haki kwa njia za kidemokrasia na amani zimekuwa chanzo cha kuibuka kwa vurugu katika mataifa mengi hususani Afrika, Tanzania ikiwamo.

Mara kadhaa wapinzani wamekuwa wakitafsiri kwa namna inayotofautiana na watawala kuhusu mahitaji ya kidemokrasia na amani, hivyo kuyafanya mataifa kutoepuka vurugu zinazoweza kusababisha umwagaji damu.

Kwa namna iwayo yote, sitaki kuamini kama CUF wanaweza kujipanga kwenda msituni kudai matokeo ya Oktoba 25, mwaka jana. Wataingia msitu upi katika Zanzibar ama Tanzania Bara? Bila shaka suala hilo halipo.

Isipokuwa uzoefu unatoa ubashiri wa namna pekee ya ushiriki huo ni pamoja na kupitia maandamano yasiyo na ukomo ambayo kwa wapinzani na jumuiya za kimataifa, huchukuliwa kuwa ni njia muafaka ya kidemokrasia katika kuelezea hisia na matakwa ya watu.

Lakini maandamano yamekuwa wakipingwa na watawala kwa maana, pamoja na mambo mengine, yanasimamisha shughuli nyingi za uzalishaji, kuhatarisha amani kutoka kwa wasiokuwa na nia njema na hata kusababisha nchi ‘isitawalike’.

Ni kwa hali hiyo, nitaitazama Zanzibar katika hatari hiyo ambayo haipaswi kuachwa itokee, bali idhibitiwe kwa namna ambayo itaungwa mkono na jamii nzima.

Kuidhibiti hali hiyo kwa namna nyingine hasa yenye kuigawa jamii katika sehemu mbili zinazopingana kutakuwa na athari kubwa kwa nchi na watu wake.

Lakini kama nilivyowahi kuandika awali, hata sasa ninahimiza wadau na mamlaka zinazohusika zinapaswa kukaa meza moja na kuileta nchi pamoja.

Ni kama alivyowahi kutamka Rais mstaafu Jakaya Kikwete, tunaijenga nyumba moja, hakuna haja ya kugombania fito.

Mashaka Mgeta ni Mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kupitia namba +255 754691540, 0716635612 ama barua pepe:[email protected] au [email protected].