Tanesco, hakuna siri huu ni mgawo 

03Dec 2017
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
NAWAZA KWA SAUTI
Tanesco, hakuna siri huu ni mgawo 

ILI nchi iwe na uzalishaji bora pamoja na mambo mengine ni lazima kuwa na umeme wa uhakika.

Hilo ni tofauti kwa Tanzania kwa kuwa umeme umekuwa ni kitendawili kilichokosa mteguaji, kwa vile  kwa sasa zipo dalili za wazi za kuwapo kwa mgawo wa umeme wa siri au wa chinichini.

Tangazo la Tanesco la hivi karibuni lilieleza kuwa kuna tatizo kwenye gridi ya taifa na wananchi wanaotegemea umeme kutoka njia hiyo kukosa nishati hiyo kwa takribani siku tatu.

Kabla ya kutangazwa kuwapo kwa tatizo katika gridi ya taifa, umeme umekuwa ukikatika kila mara na hivyo kusababisha hasara wa wateja wa nyumbani hadi viwandani.

Kutokana na umeme kukatika bila taarifa na kurejea ukiwa na nguvu kubwa wapo wananchi wanaolia kuunguliwa vifaa vyao na hivyo kupata hasara ambayo kiuhalisia haina wa kufidia.

Tatizo la umeme nchini si la jana wala juzi, limekuwa sugu, kwa kuwa siku za karibuni tena ilitokea, umeme ulikosekana siku mbili serikali iliingilia kati na kuwataka wahusika kuhakikisha unarejea huku akichukua hatua za kinidhamu dhidi ya baadhi ya watumishi wa shirika la umeme (Tanesco).

 

Najiuliza wakati ule hatua za kinidhamu zilichukuliwa ikiwamo kusimamishwa kazi baadhi ya watumishi ikielezwa kuwa wao ndiyo chanzo cha kutotengemaa kwa umeme wa uhakika, lakini kwa sasa tena tatizo lile lile limerudi jambo linalotufanya tuwaze kwa sauti kwamba kuna suala kubwa  zaidi ya hilo lililotatuliwa.

Wakati hali iko hivyo, nchi ilishahakikishiwa kuwa mgawo wa umeme utakuwa historia, na kwa sasa kuna chanzo zaidi ya kimoja cha kupata nishati.

Kwa sasa upo umeme unaotokana na gesi, maji na mafuta lakini bado shida ya upatikanaji wake iko pale pale, na zile ahadi za kuwa mgawo utabaki kuwa historia zimeshindikana kutekelezwa.

Serikali ya awamu ya tano imejinasibu vyema kuwa inakwenda kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, na tayari jitihada mbalimbali zimefanyika na wawekezaji wamejitokeza kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Lakini kukosekana kwa umeme wa uhakika kunatia doa suala la ukuaji wa viwanda na hivyo kurudisha nyuma jitihada hizo, kwanza hakuna taarifa za kukatika kwa umeme zinazotolewa mapema, lakini hutolewa baada ya umeme kukatika jambo ambalo litaathiri sana uzalishaji.

 

Wapo wazalishaji wadogo wadogo waliojiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali wanashindwa kuendelea na kazi kwa kuwa hakuna umeme, lakini bei ya bidhaa na huduma inapanda kwa kuwa wanaotumia jenereta wanaongeza bei ili mzigo wa mafuta ya jenereta uende kwa mlaji.

 Ni vyema sasa serikali ikafikiri upya juu ya uimara na uwezo wa Tanesco, kwamba kuwe na shirika jingine la kuzalisha umeme kuliko kutegemea umeme kutoka eneo moja tu ambalo miaka yote limeshindwa kuwa na utatuzi wa kudumu.

Kama nchi ina gesi, maji na mafuta na bado kuna tatizo la mgawo wa umeme, ipo haja ya kuchimba kwa ndani kujua tatizo ni nini?na kwa vyovyote lipo tatizo ambalo halijawekwa hadharani na siyo ajabu wahusika wanaumia nalo vifuani.

Huwezi kuleta maendeleo kwa taifa lolote ikiwa tu umeme wako siyo wa uhakika, kwa mazingira haya ni kwamba viwanda havitazalisha saa 24, watu hawataajirika wala kujiajiri kwa kuwa shughuli zinazotegemea umeme haziwezi kufanyika. Lakini si hivyo tu  nchi itakosa mapato na wananchi watakosa kipato.

Siku zote linapotokea tatizo lolote ni lazima ziandaliwe njia mbalimbali za kulitatua na kuangalia uzuri na ubaya wa kila njia ya utatuzi, hivyo ni wakati mwafaka kwa serikali na Tanesco kwa ujumla kutafuta suluhisho la kudumu.

Haitoshi kila wakati kutoa tangazo kueleza kuwa umeme utakatika, na iwe ndiyo kawaida lakini bado tatizo la msingi halijaelezwa, na mgawo katika baadhi ya maeneo ukiendelea kimya kimya.

Kwa saa ni kawaida umeme kukatwa usiku au mchana na kukaa kutwa au usiku wote bila umeme na hakukuwa na taarifa yoyote ya kuwepo kwa mgawo husika, na wakati mwingine umeme kuwa mdogo au kukata na kurudi kila baada ya sekunde kadhaa na hivyo kusababisha majanga kwa wateja.

Tanesco tafuteni suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa umeme nchini, ili shughuli za uzalishaji ziendelee na hivyo kuleta maendeleo ya taifa.

Tafakarini!