Tanzania ichukue hatua zaidi kufikia makubaliano ya Paris

19Jun 2019
Jenifer Julius
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tanzania ichukue hatua zaidi kufikia makubaliano ya Paris

KATIKA makubaliano ya Paris, mataifa yamewekewa malengo ya kuzuia hali ya ongezeko la joto la kimataifa kufikia nyuzi joto 1.5.

Kwa hatua hiyo mataifa hasa yanayoendelea yapo katika mapambano kuhakikisha kuwa lengo hilo linatimia na hasa wakati huu ambapo hali inazidi kuwa mbaya kadri muda unavyokwenda.

Mojawapo ya mataifa ambayo yanahitaji kukaza buti ipasavyo ni Tanzania, kutokana na kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zinaiathiri kwa kasi nchi hii iliyo Afrika Mashariki.

Na miongoni mwa athari zilizopo wazi ni kutotabirika kwa majira, hali inayoyumbisha uchumi.

Mfano kwa mwaka huu, baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wakulima wamepata hasara ya kurudia kupanda mbegu kwa sababu zile za awali ziliozea ardhini, kutokana na mvua kutonyesha kwa wakati uliotegemewa.

Kwa mantiki hiyo wapo baadhi ya wakulima hawakurudia kupanda mbegu kwa kukata tamaa au kukosa pesa.

Katika Mkutano wa Mabadiliko ya tabianchi unaoendelea jijini Bonn, nchini Ujerumani, mjadala wa jinsi gani mataifa yanaweza kuzuia ongezeko hilo la joto ili kufikia makubaliano ya Paris ni miongoni mwa mingi.

Muungwana ana maoni kwamba kuna mambo yaliyojadiliwa ambayo ni muhimu Tanzania ikajifunza ili kuendana na kasi ya makubaliano ya Paris.

Na mojawapo ya mambo hayo ni yale yanayochangia ukataji wa miti na jinsi ya kupambana nayo.

Kutokuwa na sheria kali inayosimamia biashara ya miti ni baadhi ya mambo yanayotajwa kuchangia ukataji wa misitu holela.

Kwamba sheria ipo lakini haitekelezwi ipasavyo na watu wanajikatia miti bila woga.

Ujasiri wao unatoa taswira kwamba yupo mtu nyuma ya pazia anayewalinda.

Katika mahojiano na Nipashe Dk. Dil Raj Khanal kutoka Shirikisho la Jamii ya Watumiaji Misitu (Federation of Community Forest Users, (FECOFUN) nchini Nepal, anasema ni wakati sasa mataifa kusimamia utekelezaji wa sheria za biashara ya miti ili kuhifadhi hewa ukaa ya kutosha.

Sababu nyingine inayotajwa kuchangia uharibifu wa mazingira ni mwingiliano wa shughuli za kilimo, hasa kilimo kisichokuwa na mpangilio.

Hii ina maana kwamba shughuli za kilimo wakati mwingine zinasababisha ukataji wa miti kwa kiasi kikubwa.

Katika maandalizi ya shamba, mkulima analazimika kukata miti au kuchoma moto shamba ili aweze kupanda mbegu.

Kitendo cha kuteketeza hekari za maeneo yenye miti kwa ajili ya kilimo kwa nchi kama Tanzania kwa hali iliyonayo kwa sasa ni hatari.

Aidha, moto unaoteketeza hekari za mashamba hutoa moshi kwa wingi ambao wote huishia kuziba tabaka la ozoni.

Dk. Khanal anashauri ni wakati sasa wa mataifa kuzuia uchomaji wa moto mashamba na kutoa elimu kwa wakulima ya njia nzuri za kuandaa mashamba.

Vilevile anashauri mataifa kuzuia ukataji wa miti kwa ajili ya kilimo.

Uhamaji wa watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine pia imetajwa kama chanzo cha uharibifu wa mazingira.

Kwamba jamii inapohamia eneo lingine hasa katika maeneo ya vijijini, inalazimika kukata miti ipate eneo la kujenga nyumba, lakini pia miti ya kujengea nyumba.

Jamii haina budi kuheshimu na kutangaza sheria za taifa za misitu.

Lakini pia elimu ya umuhimu wa misitu kwa jamii itolewe ikiambatana na uhamasishaji juu ya upandaji wa misitu ili kama taifa tufikie malengo tuliojiwekea kupitia Mkataba wa Makubaliano ya Paris ya kuzuia ongezeko la joto la dunia kwa kiwango cha nyuzi 1.5, na hivyo kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaonekana wazi.