Tanzania inavyopendeza kielimu miaka 60 Uhuru

07Dec 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tanzania inavyopendeza kielimu miaka 60 Uhuru

TANGU mwaka 1961 Tanzania ilipopata Uhuru, yapo maendeleo mengi ambayo taifa limeyafikia, katika nyanja mbalimbali kutokana na mapambano dhidi ya maadui watatu waliotangaziwa vita mara tu baada ya uhuru.

Ni ujinga, maradhi na umaskini adui waliokuwa vikwazo kwa maendeleo ya Watanzania, Rais wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere, alianza nao kwa kuwekeza katika elimu ili kuwamaliza wengine wawili waliobakia yaani umaskini na maradhi.

Lengo la kufanya hivyo, lilikuwa ni kuachana na elimu ya kikoloni ambayo ilikuwa na ubaguzi na haikuwahakikishia Watanzania fursa za kuelimika.

Hatua ya kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja, ilichochangia kufanikisha harakati za kupambana na maadui kwa kumwezesha kila mmoja kwenye eneo lake kushiriki katika vita iliyokuwa inamlenga adui ujinga na sasa tunapoadhimisha miaka 60 ya uhuru, matunda yake tunayaona.

Mojawapo ya matunda hayo ni elimu, takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, zinaonyesha kuwa, wakati nchi inapata uhuru, ilikuwa na shule za msingi 3,270 zilizosajiliwa.

Leo taifa linapoadhimisha miaka 60 ya uhuru, kuna shule 18,546, huku 16,656 kati ya hizo zikiwa ni za serikali na 1,890 za binafsi, jambo ambalo ni la kujivunia kwa Watanzania.

Mafanikio mengine ya kujivunia katika elimu, ni uwingi wa shule za sekondari, kwa kuwa wakati nchi inapata uhuru, zilikuwapo 41 pekee huku mbili kati ya hizo zikiwa za binafsi sasa zimefikia 5,460.

Sekondari za serikali kati ya hizo ni 3,983, za binafsi zikiwa ni 1,287, na kuongezeka kwa shule hizo, kunakwenda sambamba na uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya sekondari kuongezeka.

Historia inaonyesha, wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 1961 walikuwa ni 4,432, na kwamba mwaka huu wameandikishwa 803,085, idadi  inakwenda sambamba na ongezeko la watu, lakini uelewa wa umuhimu wa elimu.

Vilevile kwa mujibu wa Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako, vyuo vikuu vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum vimeongezeka kutoka Chuo Kikuu kimoja cha Dar es Salaam mwaka 1961 hadi vyuo vikuu 11 mwaka 2021.

Kwa hatua ambazo nchi imefikia katika maendeleo ya elimu, ninadhani ni muhimu Watanzania kushirikiana zaidi na serikali kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya elimu kwa watoto wote.

Msisitizo unaoelezwa na serikali katika kuimarisha elimu, ni zaidi katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Sayansi, Ujasiriamali na stadi za kazi mtambuka, huku kukiwa na fani za kimkakati.

Fani hizo za kimkakati miongoni mwake ni uhandisi, kilimo, udaktari, kwamba zinapewa kipaumbele, huku serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule, ili kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike na wa kiume.

Hivyo, ni vyema wazazi na walezi nao wakahakikisha watoto wao wanapata elimu bila ubaguzi au upendeleo ili hatimaye kila mmoja wao awe na mchango kwa maendeleo yake na ya taifa kwa kutumia elimu aliyopata.

Miaka 60 elimu imetoka kule sasa ipo hapa, kilichobaki ni kuendelea kuboresha zaidi mazingira ya shule ili yawe rafiki hata kwa watoto wa kike ambao wamekuwa wakikumbana na matatizo mengi.

Katika juhudi za kutatua changamoto za watoto wa kike, serikali imeshaanza kujenga shule 274 za kutwa, huku 10 zikiwa ni za wasichana.

Hivi karibuni imetoa Shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo na kukamilisha kazi hiyo.