Tasaf iimulike kaya hii maskini bado inateseka

03Jan 2020
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tasaf iimulike kaya hii maskini bado inateseka

MPANGO wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), unaotekelezwa chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, unatajwa unalenga kuzifikia jumla ya kaya milioni 1.2, ambazo ni wastani wa watu milioni sita wanaoishi katika hali ya umaskini kwa Tanzania Bara na Visiwani.

Kuna vigezo vilivyowekwa kuzibaini na kuziorodhesha kaya hizo maskini, ili chini ya mkakati wa uhawilishaji fedha, zijengewe uwezo wa kujikomboa kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Hata hivyo, kuna haja ya kumulika vigezo vinavyotumika katika kubaini kaya hizo, kutokana na ukweli kwamba kuna dai la ‘figisu’ zinazosababisha mateso kwa walengwa.

Rais Dk. John Magufuli, kuna wakati alinyooshea vidole dhidi ya ufanisi kwenye mfuko huo, baada ya kubainika kashfa ya kaya hewa nyingi sana.

Ni vitendo vya baadhi ya watendaji wa serikali, hivyo ni wazi mfuko huo unapaswa kumulikwa kwa kila mara ili wanufaika wabaki kuwa walengwa.

Vivyo hivyo, kuna malalamiko kadhaa yamekuwa yakiibuka kutoka kwa baadhi ya kaya maskini kuenguliwa kwa vigezo visivyoainishwa vyema na Tasaf.

Kaya ya Abdallah Rashidi, inaweza kuingia katika orodha ya walalamikaji walioenguliwa kwenye mpango huo, hali inayosababisha wawe katika maisha magumu kiasi cha kushindwa kumwezesha mtoto wao mlemavu kupata huduma za matibabu.

Sakina Sadick, ni mama mzazi wa mtoto huyo, anayebainisha kuwa yuko katika wakati mgumu kumhudumia mtoto wao, Munira Rashid (12), sababu kuu ni pengo katika kipato chao.

Mtoto huyo ni mlemavu wa viungo, anayeishi na wazazi wake Saranga, wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam. Ni miaka miwili imepita tangu alipotakiwa kupimwa kichwa kwa kipimo cha CT- Scan, ikiwa ni hatua za awali kumsaidia kutibu tatizo ya kutoona alilolipata baada ya kuugua homa kali akiwa na umri wa miaka 9.

Mama huyo anawaomba wasamaria wema wajitokeze kumsaidia mtoto apate huduma ya tiba ya kipimo hicho, ili atibiwe macho, kwani analalama kusota tangu alipoandikiwa apimwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamekwama gharama za malipo.

Sakina anabainisha kuwa awali walijitahidi kutafuta fedha hizo ambazo zilikuwa ni Sh. 160,000 wakapata nusu yake, (Sh. 80,000) ambazo baada ya muda, walijikuta wanazitumia kwa mahitaji mengine, pindi walipokwama kupata za kuongezea.

“Mwanangu Mnira nilimzaa mwaka 2008 akiwa mzima, lakini baada ya miezi minne ndipo nikabaini jambo tofauti mwilini mwake, kichwa kilianza kuwa kikubwa kwa kasi, tukampeleka CCBRT ambako alitibiwa na kufanyiwa upasuaji mara mbili, lakini hakurejea katika hali ya kawaida.

Anasema, Munira awali alikuwa anaona, lakini alipopatwa na homa kali akiwa na umri wa miaka 9, alilazwa katika Hospitali ya Mwananyamala, na baada ya hapo alianza kupoteza uwezo wa kuona na ndio imekuwa hali yake hadi sasa.

Ni hatua ndio inayoleta hitaji ya CT-Scan kwa ajili ya uchunguzi utakaomwezesha atibiwe. Mzazi huyo anasema, walishawahi kujiandikisha kutaka kuwa wanufaika wa Tasaf, lakini hawakukubaliwa.

Munira ni mtoto mwenye uwezo mzuri wa kujieleza na anasema, tamanio lake ni aende shule kusoma, lakini hawezi kutembea na alijifunza kuhesabu kwa kutumia ‘visoda’ nyumbani kwao.

Rashid Abdallah, baba mzazi wa mtoto huyo, anasema awali alikuwa akifanya kazi kwenye kituo cha mafuta, lakini alipunguzwa, hivyo amekuwa akitafuta kipato cha familia kwa kufanya vibarua, ikiwamo kusaidia mafundi kwenye ujenzi.

Anasema, Munira kwa sasa ni mkubwa na inakuwa kazi nzito kumbeba, hivyo anaamini iwapo watasaidiwa baiskeli, itawarahishia kumhudumia. Ombi lake ni wanajamii wamsaidie kwa kuwasiliana naye kwa namba ya simu: 0654728106.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Saranga Godwin Muro, anakiri na kuunga mkono hitaji la kaya hiyo kupatiwa msaada, akibainisha kuwa aliwaandikisha kuwa wahitaji wa Tasaf, lakini cha kushangaza, jina liliondolewa, kwa majibu wanasaidiwa watoto wanaosoma.

Kwa hali inayoikabili familia hiyo, ni wazi kuna haja ya mtu mmoja mmoja au kikundi, hata ofisi za kiserikali zijitokeze kuwasaidia, maana ninarejesha imani kwamba Tasaf wakati wote iko kwa ajili ya maslahi ya umma.

Ni jambo linalotia moyo kwamba zipo kaya kadhaa tayari zimeshanufaika kupitia mpango huo, kupitia kuungwa mkono na serikali, katika kuhakikisha unasimamiwa vyema kufanikisha malengo.

Zipo kaya kadhaa masikini zimeshatoa shuhuda za jinsi ruzuku hizo zilivyowapunguzia umaskini wa kipato na kuwawezeshwa kupata huduma na mahitaji muhimu, ikiwamo malipo ya ada za shule, huduma za afya na kuboresha makazi yao.
Barua pepe: [email protected]