Tatizo la fangasi, matibabu yake

20Mar 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Tatizo la fangasi, matibabu yake

FANGASI ni vimelea au viumbe vinavyosababisha madhara mwilini. Mara nyingi uvamizi au madhara haya huletwa na aina ya fangasi wajulikanao kama Candida albicans.

Katika hali ya kawaida, ngozi ya binadamu huhifadhi kiasi kidogo cha fangasi hawa huzinufaisha pande mbili ambazo ni mhusika pamoja na wadudu wenyewe kila upande unapata faida kutoka kwa mwenzake. Lakini madhara hutokea wakati mwingine kama fangasi watazaliana na kuongezeka zaidi.

Wapo fangasi wa aina nyingi lakini kwenye mashambulizi mengi Candida albicans ndiyo huhusika zaidi.
Madhara ya fangasi yanatibika na kupona ikiwa matibabu sahihi yatapatikana kwa wakati. Hata hivyo, fangasi wasipotibiwa huongezeka na kuwa tishio kwa maisha ya mgonjwa hasa kwa wenye upungufu wa kinga mwilini.

KINACHOSABABISHA
Maambukizi ya fangasi hutokea sehemu yoyote mwilini lakini mara nyingi huvamia zaidi aneo ambalo nyama zinakutana au kwenye mikunjo, wakati mwingine nyama zinaposuguana. Sehemu hizo ni kama kwapani, tumbo linapokutana na sehemu ya juu ya paja na maeneo ya kati kati ya vidole vya mikono na miguu.

Vimelea hivi hukua na kustawi zaidi sehemu zenye joto, unyevu na nyakati za kutoka jasho kwa wingi.

Katika hali ya kawaida ngozi ni ngao huzuia mwili usivamiwe na viumbe wavamizi wanaopenya na kuingia mwilini.

Inapotokea mkato au mpasuko wowote katika sehemu ya juu ya ngozi unaoruhusu kuwa na uwazi. eneo ndani yake huwa wazi na kusababisha fangasi kupenya na kuleta madhara.

MAZINGIRA
Fangasi wanapopata mazingira mazuri ya kuishi. huvutiwa na joto, unyevu, uchafu wa mwili au uvaaji wa mavazi yanayobana. Mambo au mazingira zaidi ya haya yanayoweza kusababisha uvamizi wa fangasi ni kama umri (watoto au wazee), uzito kupita kiasi, kisukari, kufanya kazi mazingira ya majimaji au unyevu na upungufu wa kinga kimwilini.

Lakini pia baadhi ya matibabu hasa matumizi ya dawa husababisha uvamizi wa fangasi kama vile ukitumia vidonge au tiba nyingine kwa muda mrefu.

Dawa hizo ni kama za kuua bakteria (antibiotics) na dawa za kupanga uzazi. Unapotumia dawa hizi ni vema kufuatilia kwa karibu hali ya ngozi yako ili kubaini uvamizi wa fangasi.

DALILI
Uvamizi wa fangasi una dalili mbalimbali kulingana na sehemu ya mwili iliyoathirika ambazo ni pamoja na kutokwa vipele (vinavyowasha na kuwa na wekundu kwenye ngozi), mabaka mekundu, kutokwa vumbi jeupe sehemu iliyoathirika.

Wakati mwingine kutokwa magamba, ngozi kupasukapasuka, maumivu na ukomavu wa misuli, utando mweupe na mbabuko, pamoja na na vidonda vyeupe au vyekundu midomoni.

KUGUNDUA TATIZO,TIBA
Ugunduzi wa tatizo hufahamika baada ya uchunguzi wa daktari kwa kuangalia sehemu iliyoathirika au kupitia kipimo.
Sehemu ndogo ya ngozi, kucha au maeneo ya chini ya nywele katika sehemu iliyoathirika huchukuliwa na kufanyiwa kipimo maabara. Mara baada ya tatizo kugundulika daktari huchunguza zaidi ili kufahamu chanzo cha fangasi kwa mhusika.

Vyanzo ambavyo vinahusika ni kama mabadiliko ya hali ya usafi wa mwili au kisukari na utunzanji wa ngozi.

Matibabu ya fangasi wa ngozi huwa ni rahisi mgonjwa anatumia dawa za kukausha ngozi, krimu za fangasi, mafuta, au losheni ili kupaka sehemu iliyoathirika. Iwapo madhara ya fangasi ni makubwa au hayajapona kwa dawa za awali basi daktari humpatia mgonjwa dawa zaidi kwa njia ya mdomo au sindano.

KUJIKINGA
Zipo njia mbalimbali za kujikinga dhidi ya uvamizi wa fangasi ambazo ni pamoja na uvaaji wa nguo zilizokauka kikamilifu zinazoweza kunyonya unyevu wa ngozi yako.

Hakikisha hali ya usafi sehemu zinazokuza fangasi kama kwapani, sehemu kati tumbo na paja, katikati ya vidole na sehemu nyingine zote zinazojulikana kwa kukuza fangasi.

Pia ni vyema kukausha sehemu zote za mwili zenye mikunjo haswa kwa watu wanene, kuoga na kujikausha vizuri kila baada ya kazi zilizokutoa jasho, kuvaa viatu vya wazi nyakati za joto na kubadili soksi na nguo za ndani mara kwa mara.

Kwa watu wazima fangasi sio tatizo kubwa la kutishia uhai kwani hutibiwa zikapona. Maambukizi ya fangasi ni hatari zaidi kwa wazee na watoto wadogo pamoja na wenye upungufu wa kinga mwilini.

Linakuwa tatizo kubwa kwa makundi haya kwa vile madhara husambaa sehemu nyingine za mwili ikiwamo koromeo, valvu za moyo, tumboni, ini na kwenye mapafu. Ni muhimu kuwahi matibabu mapema pale unapogundua ugonjwa kwani kadri unapowahi kutibu ndivyo unavyopona mapema.

Iwapo hali ya muwasho inaambatana na maumivu ya tumbo au homa kali basi wahi haraka hospitalini.