Tatizo la mawe kwenye mfuko wa nyongo -2

17Jul 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Tatizo la mawe kwenye mfuko wa nyongo -2

WIKI hii tunaendelea na fululizo wa makala zinazozungumzia mawe kwenye figo na ndani ya mfuko wa nyongo.

Makala iliyopita tulimalizia safu hii kwa kutizama masuala yanayomweka mtu kwenye hatari ya kupata tatizo hilo ambayo ni kama ujauzito, matumizi ya dawa za kupunguza kiwango cha lehemu na umri. Leo tunatizama namna ya kugundua mawe ya mfuko wa nyongo.

Zipo aina mbalimbali za vipimo ambavyo hutumika kubaini tatizo hilo. Kwanza vipimo hufanyika kwa kupata picha ya ndani ya tumbo taratibu mbalimbali zikihusishwa.

ULTRASOUND:
Mgonjwa hufanyiwa kipimo hicho kupata picha ndani ya tumbo.Njia hii hupendekezwa ili kubaini uwepo wa mawe hayo ndani ya mfuko wa nyongo.

CT SCAN:
Kipimo hiki hutumika ili kupata picha ya ndani ya ini pamoja na sehemu zingine za tumbo.

KUPIMA DAMU:
Kipimo hiki hutumika kufahamu kiwango cha kemikali ya ‘bilirubin’ kwenye damu. Aidha husaidia pia kubainisha hali ya afya ya figo.

MATIBABU
Mawe ya mfuko wa nyongo huonekana kwenye kipimo japokuwa mara nyingi hayaonyeshi dalili. Wakati mwingine hayahitaji matibabu ya aina yoyote.

Daktari humshauri mhusika kuwa makini na dalili ambazo hujitokeza baadaye ambazo ni pamoja na maumivu kuoongezeka sehemu ya juu ya tumbo karibu na mbavu upande wa kulia.

Iwapo dalili zitajitokeza baadaye baada ya mtu kugundulika kuwa na mawe ya mfuko wa nyongo huhitaji kupatiwa matibabu. Japokuwa watu wengi wenye mawe ya mfuko wa nyongo yasiyo na dalili hawahitaji matibabu kabisa.

UPASUAJI:
Mara nyingi matibabu kwa njia ya upasuaji ndiyo njia ya kwanza kutibu mawe ya mfuko wa nyongo . Iwapo mgonjwa anapata dalili.

Matibabu haya hufanywa ili kuondoa mfuko wa nyongo. Baada ya mtu kuondolewa kiungo hicho nyongo ambayo hutengenezwa kwenye ini husafiri moja kwa moja kuingia ndani ya utumbo mwembamba bila kuhifadhiwa kwenye mfuko kabla ya kumwagwa ndani ya utumbo mwembamba.

Mgonjwa anaweza kuishi bila kuwa na mfuko huo kwani hauathiri uwezo wa kumeng’enya chakula japo hali ya kutokuwa na mfuko wa nyongo inaweza kusababisha matatizo ya muda mfupi.

TIBA YA DAWA:
Iwapo chanzo cha mawe ya mfuko wa nyongo kwa mgonjwa kimesababishwa na wingi wa lehemu basi mgonjwa hupewa dawa maalum ambazo husaidia kuyeyusha helemu iyoganda.

Hata hivyo, matibabu ya dawa huchukua kipindi cha miezi kadhaa hadi miaka mingi kwa mawe haya kuyeyuka.

Wakati mwingine matibabu haya hayayushi mawe, hivyo hayatumiki mara nyingi na hutumiwa pale ambapo mgonjwa hawezi kufanyiwa upasuaji.

MADHARA
Kuwepo mawe kwenye mfuko wa nyongo huleta madhara kama kuvimba ‘inflammation’ kwenye shingo ya mfuko wa hali ambayo huambatana na maumivu makali pamoja na homa.

Huleta pia kuziba kwa mrija wa kupitisha nyongo. Wakati mwingine mawe haya huziba mirija ambayo hupitisha nyongo kutoka kwenye ini au mfuko wa nyongo kwenda kwenye utumbo mdogo.

Hali hii husababisha umanjano ‘jaundice’ au maambukizi kwenye mirija hiyo.Saratani ya mfuko wa nyongo inaweza pia kutokea.Watu wenye historia ya tatizo la mawe kwenye mfuko wa nyongo huwa katika uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya mfuko wa nyongo japokuwa aina hii ya saratani hutokea mara chache sana.

KUZIBA MRIJA WA KONGOSHO:
Mrija wa kongosho ‘pancreatic duct’ ni mrija ambao huanzia kwenye kongosho hadi kwenye mrija wa kupitisha nyongo na ambao kazi yake ni kupitisha kimeng’enyo maalum ‘pancreatic juice’ ambacho husaidia kumeng’enya chakula.

Mawe ya mfuko wa nyongo huweza kusababisha kuziba kwa mrija huu wa kongosho hali ambayo husababisha kuvimba kwa kongosho kitaalam ikijulikana kama ‘pancreatitis’. Hali hii ya kuvimba husababisha maumivu makali sehemu ya tumbo na mara nyingi huhitaji matibabu ya haraka.

USHAURI:
Kuzuia uwezekano wa kupata mawe ya mfuko wa nyongo ni pamoja na kula mlo kamili, kutoruka milo ikimaanisha kuwa unakula milo yote kwa siku, kuwa na uzito sahihi, kunywa maji kiasi cha kutosha kila siku na kuhakikisha mwili unakuwa na maji ya kutosha muda wote na pia iwapo una mpango wa kupungua punguza uzito taratibu kwa kuwa upunguaji uzito wa haraka huongeza uwezekano wa kupata mawe ya mfuko wa nyongo na matatizo mengine ya kiafya.