Tatizo Stars si kocha, wachezaji ni mfumo

23Jan 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tatizo Stars si kocha, wachezaji ni mfumo

UMEKUWA ni kama utamaduni wa baadhi ya mashabiki wa soka hapa nchini kwa sasa kuwa kila Timu ya Taifa (Taifa Stars), inapofanya vibaya, basi 'jumba bovu' linamwangukia kocha mkuu wa timu hiyo.

Tangu timu hiyo ilipokuwa chini ya Marcio Maximo, mambo ni yale yale. Hadi alipokuja Emmanuel Amunike hali iliendelea kuwa hivyo hivyo na hata sasa ambapo inafundishwa na Etienne Ndayiragije hakuna kilichobadilika.

Maximo, ambaye ni Mbrazil aliipeleka Stars kwa mara ya kwanza katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), mwaka 2009 zilizochezwa nchini Ivory Coast, lakini baadaye alionekana hafai, akaondolewa.

Walikuja makocha wengi baadaye ambao nao waliondoka kwa mtindo unaofanana na huo, hadi alipokuja Mnigeria, Amunike.

Huyu naye alifanikiwa kuipeleka Tanzania kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zilizochezwa nchini Misri, mwaka juzi. Baadaye naye hakudumu akatimuliwa.

Sisemi kuwa kocha ambaye ameipatia mafanikio timu asifukuzwe, lakini Watanzania kuwa tabia ya kuwaondoa makocha kwa namna ambayo wanaonekana kama vile hakuna kitu walichofanya.

Sasa hivi ukiangalia kwenye mitandao ya kijamii na mijadala inayoendelea kwenye baadhi ya vipindi vya michezo kuhusu Ndayiragije utashangaa.

Ni kocha huyu huyu ambaye kwa kuteua wachezaji ambao si vipenzi kwa mashabiki wa soka nchini, alifanikiwa kuipeleka Stars kwenye michuano ya CHAN ambayo kwa sasa inaendelea nchini Cameroon.

Hata jinsi Stars ilivyofanikiwa kuingia fainali hizo, utagundua kuwa ni juhudi binafsi za kocha huyo kuchagua wachezaji wenye vipaji ambavyo vinaweza kumsaidia huku akimjumuisha golikipa mkongwe na mzoefu, Juma Kaseja.

Lengo lake la muda mfupi lilikuwa ni Stars ifuzu. Alijua amchukue nani na nani ili atimize lengo. Na kweli alifanikiwa.

Kwa sasa anaonekana kama vile haiwezi Stars, afukuzwe na kutafutwa kocha mwingine. Mimi sikatai Ndayiragije kufukuzwa kwa sababu hatokaa milele. Lakini kumpa lawama kuwa ndiyo sababu ya Stars kutofanya vyema katika mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia, ndiyo napoona hakuna uhalisia.

Kwa baadhi ya Wabongo walivyo, leo kama Stars ikiifunga Namibia, zile kelele zote za Ndayiragije zitapungua na kama itapita kwenye hatua ya makundi, basi kelele na malalamiko yanayoendelea sasa yataisha kabisa.

Zinaweza kuibuka pale timu itakaposhindwa kuchukua Kombe la CHAN. Bado kuna baadhi ya Watanzania wanaamini kuwa Stars ina uwezo mkubwa kisoka kiasi cha kuchukua kombe la michuano hiyo na kama likikosekana tatizo linakuwa ni kocha.

Si kweli. Labda ingekuwa ile Stars ya miaka ya 1970 hadi mwishoni mwa 1980. Baada ya hapo soka la Tanzania lilishuka sana na sasa ndiyo limeanza kupanda tena taratibu, bado hata Stars ikichukua CHAN siyo kwamba itakuwa soka lake liko juu sana.

Hapo miaka ya katikati kuna sehemu tulikosea. Misingi ya kuzalisha wachezaji wapya ilikiukwa. Hatukupata wachezaji bora tena kama kina Mohamed Rishard Adolf, Peter Tino, Mohamed Salim, Juma Mkambi, Charles Boniface Mkwasa, Thuwein Ally na wengineo.

Mashindano ya soka yalianzia shuleni, vyuoni na hata kwenye mashirika ya umma, kampuni na hata sekta binafsi.

Zamani kila kona ya nchi kulikuwa na viwanja vya kuchezea watoto, lakini baadaye vilipigwa bei na kuwa gereji,

kujengwa nyumba, ndiyo maana tunaona wachezaji wengi wa Kibongo hata kwenye CHAN, 'kukontroo' mpira tu inakuwa tatizo. Wachezaji wengi wa Kitanzania wana tatizo la kumiliki mpira na kutulia, huu ndiyo msingi mkubwa wa soka ambao mchezaji anafundishwa utotoni.

Badala yake tunaona wachezaji wetu wakiwa na mpira, utafikiri chini au mpira wenyewe una moto.

Hata wachezaji vipenzi vya mashabiki ambao mashabiki wengi wa soka walitaka kocha awaite, walishawahi kuitwa huko nyuma tatizo ni hilo hilo na hakuna walichofanya.

Ukiona mchezaji wa Kitanzania ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, hicho ni kipaji binafsi tu.

Nadhani ifike wakati tuwaache makocha wafanye kazi yao kwa uhuru na Watanzania kurudi kwenye mfumo sahihi wa kutengeneza wachezaji bora tangu utotoni.