TEHAMA inakupa taarifa, lakini changamoto hudhalilisha

03Nov 2020
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TEHAMA inakupa taarifa, lakini changamoto hudhalilisha

TEKNOLOJIA ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), licha ya kukua kwa kasi imeleta mapinduzi ya upatikanaji taarifa mahali popote kwa urahisi duniani lakini, zikiibuka changamoto lukuki hasa wizi na udhalilishaji kinamama.

Aidha, inawezesha habari kupatikana kwa gharama nafuu kupitia simu za mikononi, zinazowawezesha watumiaji kupokea taarifa kutoka eneo lolote duniani baada ya kujiunga na kampuni tofauti za simu.

Mkuu wa kitengo cha usimamiaji, utekelezaji wa masharti ya leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Dk. Philip Filikunjombe, anasema TEHAMA imebadili mfumo wa mawasiliano katika sekta ya habari.

“Habari imekuwa jambo rahisi na mitandao ya kijamii inafikisha habari kiurahisi. Wasikilizaji wanaongezeka kupitia redio na hata mtandaoni ingawa changamoto kubwa ni habari za picha za udhalilishaji wanawake,” anasema Filikunjombe.

“Habari imefanya jambo jepesi na mitandao ya kijamii inasaidia kuzisambaza kwa urahisi. Wasikilizaji wanaongezeka ingawa changamoto ni udhalilishaji huku wanawake wakiathiriwa zaidi,” anasema Filikunjombe.

Kukua kwa TEHAMA kunasababisha changamoto ikiwamo ongezeko la kesi za aina tofauti hasa za udhalilishaji kwenye kitengo cha huduma kwa wateja cha mamalaka hiyo.

Anasema changamoto nyingine ni kukua kwa habari feki, uhalifu mtandaoni zinazoletwa na kukosekana udhibiti wa mitandaoni ya kijamii.

Kitaaluma, picha isiyo na maadili haitumiwi, lakini mitandao ya kijamii mwanamama akikaa vibaya kwenye sherehe hiyo ndiyo inakuwa habari wanaipiga na kuisambaza mtandaoni,” anasema Filikunjombe.

Filikunjombe anasema kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018, zinasaidia kujua watuma taarifa mtandaoni wanafahamika pia kuwawajibisha inapotakiwa au kuwataka wafanye marekebisho.

Kanuni hizo zinawahimiza wananchi kuwa kukiwa na uvunjifu wa kanuni waende polisi na si TCRA. Lakini masuala ya maudhui yanamtaka mtuma taarifa kuwalinda watoto pia kuwa na nywila kwenye akaunti za mitandao ya kijamii na simu za mikononi au kompyuta.

Ni wazi kuwa simu isiyo na nywila au neno la siri ikiibwa ni rahisi kufanyiwa uhalifu na kosa hilo adhabu yake ni faini isiyopungua Shilingi 5,000,000 au kifungo kisichopungua miezi 12.

Filikunjombe anasema kwenye dunia ya teknolojia kunaweza kuwa na kitendo kimoja na kuleta madhara tofauti kwa mfano mtu alipita nyumbani kwa jirani akakata waya na umeme ukakosekana.

Aidha, mwingine alikata waya kama huo hospitalini nayo ikakosa umeme, huduma za dharura na muhimu zikasimama, wawili hao wakikamatwa nani atapewa adhabu kubwa? Sheria inatoa maelekezo.

Anataja makosa mengine mtandaoni ni kuonyesha mbinu za kihalifu kama wizi, kutoroka gerezani, kuweka picha za mtoto mtandaoni, kukutwa na picha za utupu.

Filikunjombe anakumbusha kuwa ni marufuku kutumia habari za media nyingine bila idhini, lakini ni kosa.

Ofisa Mwandamizi Semu Mwakyanjala, anasema sekta ya habari na mawasiliano nchini, imeleta baadhi ya changamoto zikiwamo wizi wa mtandao na udhalilishaji wa kijinsia na kwamba ukuaji huo unahitaji usimamizi madhubuti ili isiwe hatari nchini.

Anasema vyombo vya habari katika mfumo wa kidigitali ikiwamo vya mtandaoni zinaelimisha ingawa zipo changamoto lakini zina mchango muhimu katika ujenzi wa taifa.

Anakumbusha kuwa kabla ya uhuru kulikuwa na vyombo vichache, lakini sasa kuna redio 183 kutoka moja baada ya uhuru na kwamba ni chanzo cha ajira kwa Watanzania.

Zipo televisheni 47 nchini na aidha, mfumo wa kutuma na kupokea pesa ni kitu kilichosambaa nchini na hivi sasa Watanzania milioni 27 wana akaunti benki kupitia mfumo wa mtandaoni na simu za mkononi.