TEHAMA sasa ni wajibu, haikwepeki

11Aug 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TEHAMA sasa ni wajibu, haikwepeki

TEKNOLOJIA ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa sasa ni moja ya kigezo kinachotumika kutathmini ubora wa shule za sekondari, lengo likiwa ni kuhamasisha utumiaji wa teknolojia hiyo shuleni.

Kwa maana hiyo, suala la kutumia TEHAMA ni muhimu, hasa kwa shule ambazo walimu wake wamepata mafunzo ya jinsi ya kutumia teknolojia hiyo kwa manufaa ya wanafunzi.

TEHAMA pia haiishii kwenye shule tu bali inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji na uendelezaji wa shughuli mbalimbali, na hutumika katika maeneo mengi yakiwamo ya kibiashara.

Hivyo kutokana na ukuaji wa teknolojia na kuongezeka kwa matumizi ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, imekuwa ni rahisi watu kuwasiliana na hata kufanikisha shughuli zao za kila siku.

Kwa mfano, kutokana na ukuaji wa teknolojia wafanyabiashara wengi wanatafuta masoko kupitia teknolojia ya mawasiliano kama vile mitandao ya kijamii ikiwamo whatsup, facebook na instagram.

Mfanyabiashara anapotumia njia hiyo, anaweza kuuza bidhaa au huduma mtandaoni kwa kuweka bidhaa zake pamoja na taarifa zote muhimu kama bei, mawasiliano na namna gani mteja anaweza kuipata.

Hivyo, kutokana na umuhimu huo wa TEHAMA, wanawake wanaofanya biashara nje ya mikapa ya Tanzania, wanahimizwa kuitumia ili wawafikie wateja wengi kirahisi na tena kwa muda mfupi.

Huo ni ushauri wa Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Mariam Tambwe, kwa wanawake hao wakati akitoa mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

TEHAMA pia inatajwa kutumika katika utunzaji wa kumbukumbu, ambao kwa ujumla wake ni kwamba unamsaidia mtu kuona mwenendo wa biashara yake na kulipia malipo mbalimbali ikiwamo kodi ya mapato ya serikali.

Ukuaji wa teknolojia umerahisisha utunzaji wa kumbukumbu za biashara, kwa kuwa unaweza kufanyika kupitia mfumo maalumu wa kidigitali, ambao unamsaidia mtu kutunza kumbukumbu za biashara yake kwa haraka na kiurahisi.

Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, kupitia teknolojia hiyo mtu anaweza kupata elimu ya biashara kwa kujifunza mambo mengi yahusuyo biashara ingawa kuna changamoto kadhaa ikiwa ujuzi mdogo wa matumizi ya teknolojia hiyo.

Aidha, suala la matumizi mabaya ya teknolojia nalo linatajwa kuchangia upotevu wa muda, kutoelewa lugha ya Kiingereza nalo ni tatizo lingine kwa baadhi ya watu hali ambayo inasababisha wakwepe kuitumia.

Bila kuzingatia ubunifu kwa kutumia TEHAMA, wanaweza kukwama katika biashara zao, kwa vile anasema, baadhi ya wanawake hutumia mitandao kujianika kwa mambo yasiyofaa badala ya kutangaza shughuli zao.

Wote hao wanapaswa kutambua kuwa teknolojia hiyo ni mkombozi kwa wale wanaoitumia inavyotakiwa, hivyo wafanyabiashara wanaotaka kupata mafanikio ni muhimu wachukue hatua za kuitumia kwa usahihi.

Msisitizo zaidi ni kwamba, katika karne hii, TEHAMA haikwepeki, hivyo kinachotakiwa ni kila mwanamke kwenda na wakati kama anavyobainisha Ofisa Programu Msaidizi Idara ya Habari TGNP, Jackson Malangalila.

Anaweka wazi kuwa mitandao ya kijamii inatumiwa na wafanyabiashara kubadilishana mawazo, uzoefu na mambo mengine ya muhimu, kwa ajili ya maendeleo ya shughuli zao za kila siku.

Anakariri taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwamba, asilimia 25 ya Watanzania, wanatumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kuwaunganisha katika shughuli zao mbalimbali.

Hivyo wanawake waliopata mafunzo hawana budi kwenda na wakati, huku TGNP ikiweka milango wazi kwa ajili ya kuwafundisha jinsi ya kufungua barua pepe na namna ya kutumia mitandao ya kijamii.

Kwa kutumia teknolojia hiyo wanawake hao watanufaika na mambo mbalimbali ikiwamo kuboresha huduma kwa wateja, kudhibiti gharama na kuleta mabadiliko katika biashara na soko kwa ujumla.