TFF haijiamini, ilete waamuzi kutoka nje

06May 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TFF haijiamini, ilete waamuzi kutoka nje

KWA kawaida, binadamu anatakiwa aishi kwa kujiamini na kufanya kila kitu kwa utashi wake na si kwa kelele au maneno kutoka kwa watu wengine.

Ndiyo maana waswahili wanasema ishi unavyotaka wewe, usiishi wanavyotaka wao.

Nasema hili kwa kulilenga Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi yake ya Ligi na Kamati ya Saa 72.

Inavyoonekana sasa imeanza kuendeshwa na mihemko ya watu kwenye mitandao ya kijamii, kuliko uhalisia.

Na kama ikiendelea hivi basi kuna hatari si soka la Tanzania kuwa la ajabu, lakini pia kuleta hata vurugu viwanjani.

Mara baada ya mechi ya kati ya Simba dhidi ya KMC kumalizika, mitandao ya kijamii ililipuka kuwashutumu waamuzi waliochezesha mechi hiyo, wakiongozwa na Abdallah Kambuzi kwa madai hawakuchezesha kwa haki.

Waamuzi hao walifungiwa si zaidi ya siku moja tu mara baada ya mechi hiyo. Wakati huo huo kuna baadhi ya adhabu au maamuzi yanatakiwa kutolewa mapema, lakini kumekuwa na ucheleshwaji mkubwa, lakini hili limetoka mapema sana kwa muda muafaka.

Sina nia ya kumtetea Kambuzi na wenzake, la hasha, lakini ukiangalia makosa yaliyofanywa kwenye mechi ile, hayatofautiani na makosa yaliyofanywa na waamuzi kwenye mechi zilizofuata kati ya Simba dhidi ya JKT Ruvu, Mbeya City dhidi ya Simba na hata Azam dhidi ya Yanga.

Nadhani hawa waamuzi wamepona kwa sababu mitandao ya kijamii haikulipuka sana kama mechi ile ya Simba dhidi ya KMC, lakini ukiangalia mechi hizo utaona makosa mengi ya wazi ya waamuzi waliochezesha. Sasa unajiuliza kwa nini Kambuzi kaondolewa na wengine wameachwa. Au kwa sababu ni Kambuzi?

Baadhi ya waamuzi wa Tanzania kwa muda mrefu sana wamekuwa na matatizo makubwa kwenye uchezeshaji wa soka na hii haijaanza leo, jana wala juzi.

Na kama TFF kupitia vyombo vyake kama itataka kufuatilia mechi hadi mechi basi inaweza kujikuta inafungia mwamuzi mmoja au wawili kila wiki.

Acha Ligi Kuu, huko kwenye Ligi Daraja la Kwanza ndiyo usiseme, maana hadi timu ya Arusha United imejitoa kwa kulalamikia uonevu.

Kwa maana hiyo ni kwamba kama TFF kupitia Bodi ya Ligi au Kamati ya Saa 72 inataka kukomesha tabia mbaya ya waamuzi basi isisubiri watu walalamike na kucharuka kwenye mitandao ya kijamii, bali ichukue hatua stahiki.

Lakini ikiwa na tabia ya kuacha madudu na kusubiri watu walalamike na kutoa shutuma kwenye mitandao ya kijamii ndiyo wachukue hatua, hizo ni dalili za woga na kutojiamini kwenye majukumu yao.

Kitendo cha kumsimamisha mwamuzi Kambuzi ghafla hivi sasa kimeleta mambo mengi na hata waamuzi hivi sasa wamekuwa wakichezesha kwa woga.

Nimemsikia Kocha Mkuu wa Simba akisema kuwa baada ya mechi ile dhidi ya KMC, waamuzi wamekuwa wakiogopa kuipa haki ya penalti timu yake hata kama ni halali.

TFF na vyombo vyake kama inaona kuna waamuzi wanavurunda kwenye baadhi ya mechi na hawataki kulaumiwa kuwa kuna timu wanaibeba, nadhani sasa imefikia wakati wa kuwaita waamuzi kutoka nje ya nchi kuchezesha baadhi ya mechi kama wanavyofanya wenzetu Misri, Afrika Kusini, Congo DR, Morocco na kwingine.

Nafikiri waamuzi kutokana nje hata kama kutakuwa na makosa, basi mashabiki wataamini kuwa ni ya kibinadamu.