TFF imarisheni 'ulinzi' sasa Ligi Kuu

20Mar 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TFF imarisheni 'ulinzi' sasa Ligi Kuu

WAKATI msimu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara unakaribia ukingoni,wasimamizi na watendaji wote muhimu wa mechi hizo wanatakiwa kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao.

Ligi hiyo inayoshiriki klabu 16 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara iko katika raundi ya 24, inamaana kila timu imebakiza michezo sita tu ili kumaliza msimu wa mwaka 2016/17.

Mpaka sasa mbio za kuwania ubingwa huo ziko wazi huku Simba ikiwa inaongoza kwenye msimamo ikiwa na pointi 54 ikifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga ambao wamejikusanyia pointi 52.

Lengo kuu la kuwa makini zaidi katika hatua hii ni kuhakikisha kila timu iliyojiandaa vizuri ndiyo inaibuka na pointi tatu au sare katika mechi hizo zilizobakia.

Hii itasaidia bingwa wa ligi hiyo atakayepatikana awe ametokana na kuonyesha kiwango cha juu ndani ya uwanja (juhudi binafsi) na 'mbeleko' yoyote kutoka kwa waamuzi au wasimamizi wengine wa ligi isipewe nafasi yoyote.

Kutokuwapo kwa vitendo vya timu kubebwa au kupewa upendeleo wa aina yoyote, kutasaidia klabu itakayokuwa bingwa kuendeleza kasi ile ile itakapokwenda kuwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya Klabu Bingwa Afrika au michuano mingine ya Kombe la Shirikisho.

Ni vyema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaanza kuchukua hatua sasa na si kusubiri mechi za mwisho ndiyo itaongeza usimamizi wake. Hii itasaidia yale 'madudu' yaliyotokea kwenye mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza (Polisi Tabora vs JKT Oljoro na Geita Gold Sports vs JKT Kanembwa).

Kujirudia kwa vitendo hivyo, si tu kutafanya bingwa aliye legelege ndiyo apatikane, pia kutaendelea kushusha heshima ya soka hapa nchini na kukimbiza makampuni na taasisi zilizokuwa zinafikiria kudhamini ligi au timu za taifa ambazo bado udhamini wake si mnono.

Klabu na wachezaji nanyi mnapaswa kuipa ushirikiano TFF katika kukomesha vitendo vyote vinavyoshusha heshima ya mchezo huo unaopendwa zaidi duniani kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapoona taratibu zinataka kuvurugwa.

Ni lazima wakati ufike Watanzania tuseme tumechoka kuwa wasindikizaji katika mashindano ya kimataifa kwa kuanza kusema 'hapana' kushabikia au kutochukua hatua kali kwa wale wanaopanga matokeo.

Tukumbuke kuwa 'mafundofundo' ambayo tunayaruhusu kufanyika katika ngazi ya klabu, kunaifanya timu yetu ya Taifa (Taifa Stars) kutokuwa imara kila inapokwenda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Tukiacha kufanya vitendo vya aina hii au hujuma yoyote ile nje ya uwanja, siku moja Tanzania itakuwa na heshima na thamani ya juu katika mchezo wa soka na kuondoa dhana iliyoko ya mataifa makubwa na madogo.

Hakuna kisichowezekana endapo misingi ya kweli itafuatwa na taratibu na kanuni zitaheshimiwa bila kuangalia kosa limefanywa na klabu ipi, yenye mashabiki wengi, yenye uwezo wa kifedha au yenye mashabiki wachache.

TFF ikiweka mkazo sasa, itaepusha kilichotokea katika ligi daraja la kwanza msimu uliopita ambao macho na masikio yalikuwa katika mechi mbili za mwisho.

Tofauti na mbio zilizokuwa katika Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Kuu inaonekana 'biashara' ya kupanga matokeo ndiyo 'hatari' zaidi kwa sababu timu zimegawanyika katika makundi matatu. Lipo kundi la kwanza la timu zinazowania ubingwa ambao wenyewe kila siku utasikia 'afe kipa afe beki ubingwa lazima' au tutafanya kila linawezekana kuhakikisha tunatwaa ubingwa.

Hizi si kauli za kiunamichezo.

Kundi la pili ambalo lenyewe halina cha kupoteza ni zile ambazo haziko kwenye mbio za ubingwa wala hatari ya kushuka, hili ndiyo kundi 'baya' kwa sababu linaweza 'kupindua' matokeo na kuharibu upepo wakati kundi la mwisho ni lile ambalo linataka kujinasua kushuka daraja.

TFF muda bado upo, kwa kushirikisha taasisi husika, mnaweza kusimamia mechi zilizosalia na hatimaye kumaliza ligi kwa ufanisi ili kuvutia wadhamini zaidi katika msimu ujao.

[email protected]