TFF imeshindwa sakata la Kakolanya?

15Apr 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TFF imeshindwa sakata la Kakolanya?

ZAIDI ya miezi sita sasa kumekuwa na msuguano kati ya Klabu ya Yanga na kipa wao, Beno Kakolanya.

Pamoja na mambo mengine, Kakolanya aliandika barua kuomba kuvunjwa mkataba wake kwenye klabu hiyo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutotimiziwa maslahi yake waliyokubaliana.

Msuguano huo ulisababisha Kakolanya kusuasua kwenda mazoezini kiasi cha kumkasirikia Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera.

Alichofanya ni kumtimua Kakolanya katika kikosi cha Yanga wakati akiwa bado na mkataba mpaka mwaka 2020 kwa madai kuwa ni msaliti kutokana na kugoma kuitumikia timu hiyo akishinikiza kulipwa madai yake.

Kipa huyo wa zamani wa timu ya Tanzania, Taifa Stars, akaandika barua kwa waajiri wake, lakini bila majibu, hivyo akawa halipwi, hatakiwi kwenye kikosi na hata hakuna makubaliano yoyote angalau ya pande zote mbili kuachana kwa amani ili kila mmoja afanye mambo yake.

Hali ilipozidi meneja wake, Selemani Haroub, aliandika barua kupeleka Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi. Hata yeye mwenyewe anashangaa hadi leo suala hilo limekuwa na kigugumizi.

“Tulilipeleka TFF kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi, lakini mpaka sasa bado," anasema meneja huyo.

Anasema mpaka sasa kipa huyo hajui msimu ujao atakuwa na timu gani kutokana na TFF kushindwa kulipatia ufumbuzi suala lake hilo na Yanga.

Utata unaanzia hapa. Kwa nini TFF ambayo pamoja na kwamba inaongoza soka, lakini pia ni mpatanishi wa klabu na wachezaji haiwaweki pamoja ili kumalizana?

Kwa nini TFF kupitia kamati zake haiwaiti Yanga pamoja na Kakolanya mwenyewe ili kuwaweka sawa na wakipatana arudi kundini?

Na kama ikishindikana kwa nini haitumii sheria na kanuni ili kuangalia tatizo lilipoanzia hadi lilipoishia na kubaini nani amevunja vipengele vya mkataba ili yeyote katika pande hizo mbili amlipe mwenzie ili kila mmoja achukue hamsini zake maisha yaendelee?

Hivi TFF kukaa kimya huku mchezaji akiwa hachezi ni kuua kipaji chake ikichukuliwa kuwa alikuwa kipa wa timu ya taifa, lakini kwa sasa ameachwa kwa sababu hajacheza muda mrefu?

TFF haidhani kuwa kitendo cha Yanga kuwa kimya ni kama vile kumkomoa mchezaji, huku na yenyewe pia ikiwa kimya ni kutomtendea haki mchezaji kwa sababu anayeumia hapo ni Kakolanya na si klabu?

Cha ajabu ni kwamba hata Chama cha Wachezaji nchini (Sputanza) kimekaa kimya kwenye hili, huku mchezaji akiwa hajui hatima yake wakati wakiwa wakali sana kwenye masuala ya mikataba inapohusu wachezaji wengine.

Mimi nadhani imefika wakati sasa TFF kufanya maamuzi kwenye hili kwa sababu limechosha masikioni mwa mashabiki wa soka nchini, huku mchezaji akiwa haelewi hatima yake.

Soka ni ajira kwa sasa na si kukomoana na ndiyo maana hata Shirikisho la Soka nchini (Fifa) huwa linatoa kibali cha miezi sita kuitumikia klabu nyingine kwa mchezaji ambaye anaonekana ana matatizo ya kimkataba au kimaslahi na klabu yake mpaka hapo utata wa tatizo lake litakapotatulia.

Fifa wanafanya hivyo kwa kusudi la kulinda kipaji cha mchezaji na kufanya maishi yaendelee.

Nashauri kama TFF haiwezi kufanya hivyo, basi imsaidia mchezaji huyo ili suala lake liende Fifa ambao wao wataamua bila woga, badala ya kuheshimu mihemko au kuogopa siasa za soka nchini.