TFF iwe makini Ligi Daraja la Kwanza

09Jan 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
TFF iwe makini Ligi Daraja la Kwanza

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara umeanza. Huu ukiwa ndiyo msimu mgumu zaidi kwenye ligi hiyo kutokana na siasa za soka la Tanzania.

Ndiyo msimu ambao baadhi ya viongozi wa serikali, vyama vya mikoa na klabu zinaungana kuhakikisha kuwa timu zao zinashinda kwa gharama yoyote ile.

Na ni hao hao ambao huzitelekeza timu hizo zinapokuwa Ligi Kuu na kuanza kutembeza bakuli. Lakini zinaposhuka daraja hufanya kila njia hata za haramu kuhakikisha zinapanda.

Zile vurugu na upangaji wote wa matokeo huwa unatokea wakati huu. Timu zinapokuwa nyumbani hufanya hila yoyote ile ili kupata ushindi.

Hata baadhi ya waamuzi hawako nyuma kwenye hatua kama hii, kutokana na rushwa, au maagizo kutoka kwa 'wakubwa zao.'

Mimi siyo mtabiri, lakini mzunguko huu kama tusipoangalia vizuri tunaweza kushuhudia vurugu kwenye viwanja mbalimbali, kwa sababu tu kuna timu zinatafutiwa mbeleko ili zicheze Ligi Kuu, hata kama hazina uwezo huo.

Si hilo tu, hata tukaona kujirudia kwa sakata kama la JKT Kanembwa na Geita Gold pamoja na Polisi Tabora na JKT Oljoro ambalo lilichafua taswira ya soka la Tanzania na kusababisha baadhi ya maafisa wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuburuzwa mahakamani kutokana na tuhuma za kuomba rushwa ili kupanga matokeo.

Mwaka juzi pia kulikuwa na mechi iliyovunjika. Ilikuwa ni baina ya Majimaji na Friends Ranger mjini Songea. Friends ilisusia mechi hiyo kwa madai ya uonevu.

Haya ni matukio ambayo TFF na bodi yake ya ligi sasa inaonekana kama inataka kuyafanya kuwa maisha ya kawaida kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Kwa mbali, tayari nimeshaanza kusikia harufu ya kile kinachotokea misimu kadhaa.

Mechi kati ya Lipuli ya Iringa na Mshikamano ya Dar es Salaam iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Samora, imeshaanza kulalamikiwa na baadhi ya wadau.

Inadaiwa kuwa baadhi ya wachezaji wa Mshikamano wamepigwa hadi kujeruhiwa kwenye mchezo huo, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni uzalendo.

Sisemi kama hili lililotokea lina ukweli au la. Ila vyovyote itakavyokuwa kati ya hayo mawili, bado inaonekana kuwa dalili za vurugu kwenye mechi hizo.

Kwanza kabisa Bodi ya Ligi, inapaswa kuanza na hili la Iringa ambalo tayari limeshaanza kuwa gumzo kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Ifanye uchunguzi kujua kuwa kama kuna ukweli wowote endapo wachezaji wa Mshikamano walifanyiwa vurugu kwenye mechi hiyo.

Lakini pia sasa, kutokana na historia ya ligi yenyewe jinsi ilivyo, inabidi iamke na kupeleka watu ambao watakuwa wanaangalia matukio na kuyaripoti moja kwa moja ili kujua mazingira ya mechi zinavyokuwa mikoani, ambako baadhi ya mechi zinakuwa na uzalendo wa kupindukia, huku mkoa mzima ukihusika.

Hili litapunguza tabia ya baadhi ya watu wanaotaka kulazimisha timu zao zipande Ligi Kuu wakati hazina uwezo huo.

Ligi Kuu Tanzania Bara inahitaji kuwa na timu bora zinazopigana kiukweli kuingia huko ili zikatoe ushindani na si kupanda kiujanja na baadaye kuwa jamvi la wageni na kuleta matatizo mengi.

Bodi ya Ligi ikumbuke kuwa wachezaji wa Ligi Kuu ndiyo hao hao wanaunda timu ya taifa, hivyo hatuwezi kuwa na wachezaji wazuri wa Taifa Stars wakati hatuna ligi bora, badala yake timu nyingi zinaingia tu kwa mipango, halafu hazileti changamoto yoyote zaidi ya kupigania kushuka daraja tu kila msimu.

Lakini haya yote yatafanikiwa kama tu baadhi ya viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi hawamo kwenye mipango ya kutaka timu fulani zipande Ligi Kuu kwa sababu mbalimbali, ikiwamo uswahiba, rushwa au kupata kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.