Tikiti ni moto wa kwanza

06Jul 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tikiti ni moto wa kwanza

TIKITI huiva vizuri kutokana na moto wa kwanza. Methali hii hutumiwa kutunasihi kwamba tuyatakapo mambo yetu yafanikiwe lazima tuyashughulikie mapema bila ya kupoteza wakati.

Ni dhahiri kuwa timu zetu za kandanda nchini zimekuwa kama watu wanaosindikiza wengine kwenye mafanikio kisha wasindikizaji kurejea nyumbani mikono mitupu. Hufanywa kama ‘viwanja’ vya kufanyia mazoezi na wachezaji wetu huwa watalii! Kwa ufupi timu haziandaliwi ipasavyo.

Nalilaumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuruhusu vilabu vyetu kusajili wachezaji 10 kutoka nje ya Tanzania. Kwa maana hiyo, timu zaruhusiwa kusajili wachezaji 10 wazawa na 10 kutoka nnje ya nchi. Kwa utaratibu wa mchezo wa kandanda duniani, wachezaji wanaocheza uwanjani ni 11. Kwa hiyo timu ikipanga wachezaji nane wa kigeni, waliobaki ni watatu tu wazawa!

Wahenga walisema “Chako ni chako, cha mwenzako si chako.” Maana yake kitu unachokiita chako ni kizuri na huweza kukufaa na una uhuru nacho. Methali hii yatufunza tuvitegemee vitu vyetu wala sio vya watu wengine. Pia yatukumbusha kuvithamini vitu vyetu ingawa sio vizuri kama vya watu wengine.

    Ni kweli kuwa wachezaji wetu wengi hawakidhi haja ya vilabu vyetu ndo sababu ya TFF kuruhusu usajili wa wachezaji 10 wageni ili kunogesha mchezo wa kandanda nchini. Matokeo ya ruhusa hiyo kumeifanya Tanzania kutokuwa na wachezaji mahiri wanaoweza kupambana kwenye michezo ya kimataifa na kuiletea Tanzania sifa.    

Kama wachezaji 10 wanaosajiliwa kutoka nje watakuwa bora zaidi kuliko wetu, ni dhahiri timu za nyumbani zitakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kupambana na timu ngeni na hivyo kuzifanya hata timu za taifa kuwa dhaifu. Inapokuwa hivyo, mchezo wa kandanda unapoteza hamu ya kuutazama na matokeo yake ni idadi ya watazamaji kupungua viwanjani!

  “Usijivunie cha mwenzako.” Maana yake usijivunie kitu ambacho si chako. Hutumiwa kutukumbusha kuwa hatupaswi kuvionea fahari vitu visivyokuwa vyetu; tuvionee fahari vitu vyetu wenyewe.

    Wachezaji wanaosajiliwa kutoka nje, tena kwa gharama kubwa kuliko wachezaji wetu, yatokeapo mashindano makubwa, huenda makwao kuzipa nguvu timu zao za taifa na kutuacha na wachezaji wetu wasiokuwa na uzoefu wala uhodari wa kucheza na timu za nje.

Mara ya mwisho Tanzania kushiriki mashindano ya Afrika ilikuwa miaka 39 iliyopita timu ikiwa na Watanzania watupu bila mchezaji hata mmoja kutoka nnje. Kwa nini? Kwa sababu wakati ule hakukuwa na utaratibu wa kusajili wachezaji kutoka nchi za nnje.

Tatizo letu ni kuwa na maneno mengi kuliko vitendo. TFF inaridhika na hali hii? Nionavyo, jibu la swali hili ni ‘NDIO!’ Kwa nini? Kwa sababu hakuna juhudi zinazofanywa na TFF kuwa na timu bora kama za wenzetu. Kwa mfano, ukubwa wa maeneo ya nchi za Burundi na Rwanda ni kama baadhi ya mikoa yetu kwa ukubwa.

TFF hailioni jambo hili? Au macho yao yanaziangalia Simba na Yanga tu? Zimefanya nini mpaka sasa? Mara ya mwisho timu hizo kutwaa Kombe la Kagame ni mwaka gani? Kwetu sisi kusherehekea Simba kufikia hatua ya pili kuelekea fainali ya Kombe la Afrika (ingawa ilitolewa), twaisifu utadhani imetwaa Kombe!

Je, Simba ingetwaa Kombe ingekuwaje? TFF ingejinasibu kuwa imeisaidia Simba?  Kwa lipi hasa? TFF haistahiki sifa kwani ilipofikia Simba ni juhudi za viongozi wake wala TFF haina cha kujivunia. Hakuna juhudi zozote muhimu zilizofanywa na zinazofanywa  na TFF kuzinufaisha vilabu vyetu zaidi ya kuwa “Domo kaya samli kwa mwenye ng’ombe.”

Katika moja ya makala zangu za michezo kuna wakati nilipendekeza kutumia muda huo kuzijenga timu za taifa (Taifa Stars, Serengeti Boys, Ngorongoro Heroes n.k.)

Timu hizo zitajengwaje? TFF iwe na shule maalum ya mchezo wa kandanda itakayokuwa na walimu wenye utaalamu wa kutoka nchi za nje. Baada ya hapo iunde timu ya walimu (makocha) wa kandanda watakaozunguka nchi nzima kuchagua wachezaji vijana kutoka timu mbalimbali za mikoani. Wote wawekwe kwenye shule maalum itakayowapa maarifa ya mchezo huo.

“Ukipanda upepo, utavuna tufani (dhoruba).” Maana yake ukipanda upepo utaishia kuvuna kimbunga. Methali hii huweza kutumiwa kwa mtu anayepuuza mashauri anayopewa na kuishia kupatwa na matatizo mengi sana. TFF zindukeni. Au bado mpo usingizini?

[email protected]

0784  334 096