Timu zijipange Ligi Kuu, itakuwa ngumu mno

05Aug 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Timu zijipange Ligi Kuu, itakuwa ngumu mno

KILA timu kwa sasa imejichimbia kambini kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 23, mwaka huu.

Makocha wapo kwenye hekaheka za kuwaweka fiti wachezaji pamoja na kuwapa ufundi ili ligi ikianza waanze kukifanya kile ambacho waliwaagiza.

Ni kipindi kinachohitaji utulivu na umakini wa hali ya juu, kwani mara nyingi tunaona ligi ikianza makocha wanakuwa na ama na vipindi vifupi, au hawana kabisa muda wa kuwafundisha tena wachezaji hao, zaidi ya kurekebisha tu makosa madogo madogo kutokana na ratiba kubana.

Kinachotakiwa sasa kwa makocha na wachezaji, huu ndiyo wakati wa kujiandaa kwa usahihi na ukamilifu kwani inavyoelekea msimu huu ligi itakuwa ngumu zaidi kuliko hata ya msimu uliopita.

Tuliona Ligi Kuu msimu uliopita ilivyokuwa ngumu, Simba, Yanga na Azam zilivyokuwa zikikimbizana kuusaka ubingwa. Ilipofika katikati, tuliona Azam pumzi ikianza kukata, Yanga ikizidi kupepea kileleni.

Lakini Simba ilipotoka kwenye mechi za kimataifa iliingia na gia mpya, na wakati huo Yanga nayo ilionekana kuishiwa pumzi na kuwafanya Wekundu wa Msimbazi kutwaa ubingwa.

Hata hivyo, timu zote tatu za juu zimepata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, huku KMC, bila kujijua, ikifanikiwa kupata 'zari', la kucheza Kombe la Shirikisho baada ya kukamata nafasi ya nne. Nafasi hizi zilitangazwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) wakati ligi imeshamalizika.

Na hii ilitokana na uwakilishi mzuri wa Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa kiasi cha kufika robo fainali. Nina uhakika, kama Caf ingeitangazia mapema TFF kuwa nafasi za uwakilishi wa michuano ya kimataifa zimeongezeka, ligi ingeweza kuwa ngumu zaidi ya ilivyokuwa.

Kwa sasa timu zote 20 zinajua kuwa kuna nafasi tatu za moja kwa moja za kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa. Kutokana na hali hiyo, hakuna timu itakayokubali kupoteza mechi kirahisi kama ambavyo tulikuwa tukishuhudia huko nyuma, baadhi ya timu zikishaona nafasi za juu kuna timu ambazo zina pointi nyingi ambazo haziwezi kufika, basi zinaamua kufa moyo na kupoteza kirahisi.

Timu zitakuwa zikipambana kutafuta nafasi ya kwanza, pili ya tatu mpaka ya nne, maana lolote linaweza kutokea.

Kwa maana hiyo hata timu iliyokuwa chini, nayo itakuwa ikipambana ipate hata nafasi ya nne, kwa sababu moja inaweza kutokea kama ilivyotokea kwa Azam, timu ya tatu kutwaa Kombe la FA na kupata nafasi ya moja kwa moja kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho, hivyo anayeshika nafasi ya nne akaikwaa kiulaini kama ilivyokuwa kwa KMC.

Nafasi kutoka moja tu ya bingwa kuwakilisha nchi, hadi tatu, mpaka nne zitaifanya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20 kuwa ngumu na isiyotabirika kwa sababu kila timu sasa itataka kuwa ndani ya nafasi hizo.

Kinachotakiwa sasa timu zote ni kufanya maandalizi kabambe, na kila timu ikitegemea upinzani mkali kutoka kwa nyingine na hatutarajii kuona malalamiko yasiyo ya msingi wala mashiko.

Ni timu zilizojipanga vema kwa maandalizi ndizo zitakazofanya vizuri kama waamuzi watakuwa wakichezesha kwa haki.