TRC itupie macho upungufu huu kuboresha zaidi huduma

14May 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TRC itupie macho upungufu huu kuboresha zaidi huduma

YUMKINI huduma zinazidi kutengemaa kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa treni au abiria kama ilivyokuwa inafahamika kwa baadhi ya wakazi wa Kanda ya Ziwa nyakati hizo.

Ninazungumzia nyakati za miaka ya 1980 na mwanzoni ya miaka ya 1990 kwa wale waliokuwa wakitumia usafiri wa vyombo vya Shirika la Reli nchini (TRC) nyakati hizo.

Kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa, treni au garimoshi lilijulikana pia kama abiria, nyakati ambazo mbali na kung’aa katika eneo la usafirishaji mizigo, ni usafiri ambao ulitegemewa na wengi katika safari zao.

Si kutokana na bei ya nauli ambayo wengi waliimudu, lakini pia uwezo wa kuchukua abiria wengi kwa wakati mmoja, katika kipindi ambacho usafiri huo ulipatikana karibu kila siku ya wiki.

Ni kipindi ambacho si tu kilirahisisha gharama za usafiri kwa wananchi na wafanyakazi wa serikali, lakini pia kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari nchini, wengi wakiwa wanasoma mbali na makwao.

Muungwana anasema kwamba kuna mambo ambayo yanazidi kuboreshwa katika usafiri wa treni za shirika hilo lililopitia misukosuko mingi ya utoaji huduma kwenye miaka ya katikati ya 1990 hadi ya 2010, baada ya kuwa ameutumia usafiri huo.

Ilikuwa ni mwezi Machi mwaka huu aliposafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mpanda mkoani Katavi, kwa ajili ya kusalimia ndugu na jamaa.

Hiyo ni safari yake ya kwanza akitumia treni kutoka mwaka 1995, na moja ya sababu zilizosababisha kutotumia usafiri huo ilitokana na uduni wa huduma uliojitokeza katika kipindi hicho, kujaza abiria kupita kiasi ikiwa ni sababu mojawapo.

Moja ya mambo yaliyomvutia Muungwana ni utaratibu mpya wa kufanya malipo ya tiketi katika Stesheni ya Dar es Salaam ambapo mkatisha tiketi hagusi fedha ya msafiri.

Kutokana na uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kwamba malipo yote ya serikali pamoja na  mashirika yake yatumie mfumo wa kielektroniki kufanya malipo, TRC nao wameshaanza kutumia mfumo huo.

Kwa uzoefu alioupitia Muungwana, anaona utaratibu huo pamoja na mengine umepunguza suala la ulanguzi wa tiketi kwani msafiri anatakiwa kuwa na kitambulisho ili aweze kuhudumiwa.

Si hilo tu la kununua tiketi lililoboreshwa, bali hata suala la eneo la kujihifadhi abiria katika Stesheni ya Reli Dar es Salaam pia limeboreshwa likiwa na huduma zote zinazohitajika kwa abiria muda wote anapokuwa pale.

Aidha, suala la kutoa taarifa ya sababu za treni kuchelewa kuondoka au kunapokuwa na dharura ambalo ni la msingi kwa abiria kujua nalo linafanyika kama ilivyotokea kwa Muungwana siku aliposafiri, ambapo ilibidi achelewe kuondoka kwa saa tisa.

Hiyo ilitokana na mazonge yaliyojitokeza njiani kwa treni iliyokuwa ikitokea Mwanza na Kigoma kuja Dar es Salaam.

Hata hivyo, Muungwana alibaini baadhi ya mapungufu katika safari yake ambayo TRC inaweza kuyafanyia kazi kwa sababu hayahitaji uwekezaji mkubwa ama msaada kutoka nje ya nchi.

Mojawapo ya mapungufu hayo ni kukosekana kwa maji kwenye vyoo kwa muda mwingi wa safari.

Wakati stesheni ya treni jijini ina maji ya kutosha, Muungwana alishangaa ni kwa nini maji hayakuwekwa katika vyoo kiasi cha mmoja wa wafanyakazi wa treni hiyo kushauri abiria wa moja ya mabehewa ya daraja la tatu, kula vyakula vikavu ili kuepuka suala la kwenda chooni mara kwa mara.

Ni mpaka treni ilipofika Tabora, ndipo Ofisi ya Stesheni Tabora ilipowataka wahudumu wa mabehewa kuhakikisha kwamba mabehewa na vyoo vyote vina maji na ikafanyika hivyo.

Upungufu mwingine ambao TRC inaweza kuurekebisha ni wa baadhi ya abiria na hasa wa njiani kukatiwa tiketi ya kusimama, ambao pia Muungwana aliushuhudia.

Ni rai ya Muungwana kwa TRC kurekebisha mapungufu haya ili kuendelea kuboresha huduma za usafiri huo.