Tuanze kujipanga kufikia 50/50 mwaka 2030

22Mar 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuanze kujipanga kufikia 50/50 mwaka 2030

MAPEMA mwezi huu, Tanzania iliungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mwanamke duniani.
Katika maadhimisho hayo, kaulimbiu ilikuwa inasema 50/50 ifikapo 2030 tuongeze jitihada.

Kaulimbiu hiyo ililenga kuelimisha serikali na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa sera na mipango inayowekwa kwa kuzingatia haki za wanawake.

Nyingine ni kutoa fursa maalum kwa taifa, mikoa, wilaya, mashirika ya dini, vyama vya siasa na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa kimaendeleo na kubainisha changamoto mbalimbali zilizopo katika kufikia azma ya ukombozi na maendeleo kwa mwanamke nchini.

Katika kuadhimisha siku hii ya mwanamke kila Machi 8 kila mwaka, ipo haja ya kuangalia wapi tulipotoka, wapi tulipo na wapi tunakwenda katika kufanikisha maendeleo ya mwanamke.

Kadhalika, tunahitaji kutafakari kama yapo mafanikio yaliyofikiwa ama bado kuna mapungufu ambayo bado yanahitajika kufanyiwa kazi zaidi.

Hii si tu kwa serikali, bali pia kwa jamii, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, taasisi za dini na wadau wengine.
Katika miaka ya nyuma kundi la wanawake lilikuwa limewekwa nyuma sana katika masuala mbalimbali ikiwamo kutopatiwa haki zao za msingi, kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vya kikatili na kuchangia kukwamisha maendeleo yao.

Pamoja na jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali katika kuhakikisha usawa unapatikana baina ya mtoto wa kike na wa kiume, lakini bado kuna changamoto ndogondogo ambazo zinapaswa kushughulikiwa.

Kama ambavyo kaulimbiu ya mwaka huu inasema, ipo haja kuongeza juhudi zaidi ya pale zilipofikia kuhakikisha vikwazo kwa watoto wa kike shuleni, kazini na katika ngazi za familia vinaondolewa ili kufikia 50/50 katika ngazi zote za maamuzi ifikapo mwaka 2030.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), ni miongoni mwa taasisi zilizojitokeza kudhamini maadhimisho ya siku ya mwanamke wilaya ya Kisarawe, nao wanasema kwamba pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau za kumkomboa mwanamke kuhakikisha anapata haki zake, lakini bado wanakiri kuwapo kwa vikwazo vinavyoweza kusababisha kukwamisha lengo la kaulimbiu hiyo.

Katika maadhimisho hayo, Tamwa walitaja baadhi ya vikwazo kwamba ni pamoja kuendelea kuwapo kwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au kwa amri ya mahakama na hivyo kukosa haki zake za msingi ikiwamo fursa ya kupata elimu.

Nyingine walisema ni kuendelea kukumbatia baadhi ya mila na desturi kwa baadhi ya makabila kwa kutokumruhusu mwanamke kushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali zikiwamo za kisiasa pamoja na kupewa kipaumbele katika elimu.

Kama ambavyo tumekuwa tukielezwa kwamba ukimuelimisha mwanamke mmoja umeelimisha jamii nzima. Mimi pia ninaamini zaidi katika uwezo wa mwanamke pale anapopatiwa nafasi.

Ikumbukwe kwamba kama mwanamke huyo ameweza kusimamia familia yake vizuri, kuongoza watoto, mume, ikiwamo kupanga bajeti, naamini kwamba hakuna jambo lolote linaloweza kumshinda hata katika ngazi nyingine.

Kikubwa zaidi anachohitaji ni kuhakikisha anapata fursa sawa na mwanamume ya kupata elimu na ujuzi ya kumuongoza katika kutekeleza majukumu yake ya kazi na kuondolewa vikwazo vingine vyote.