Tubadili Mfumo Wetu wa Utumishi wa Umma

29Nov 2020
Nkwazi Mhango
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Tubadili Mfumo Wetu wa Utumishi wa Umma

PAMOJA kupata uhuru takriban miaka zaidi ya 60 iliyopita, nchi nyingi za kiafrika kama si zote zilisahau, au tuseme, makusudi, hazikubadili mifumo yake ya uendeshaji wa serikali zake.

Kimsingi, nchi hizi zilirithi mfumo wa kikoloni na kuendelea hata kuung’ang’ania kwa manufaa ya watu wachache wenye nguvu katika jamii. Kutokana na mfumo huu wa kikoloni na kinyonyaji, nchi zote za kiafrika zilibakia maskini pamoja na nyingi kujaliwa utajiri wa rasilimali.

Kuna msemo kuwa Afrika ina utajiri wa maliasili, lakini ikikaliwa na watu maskini hata kuliko wa nchi nyingi za Magharibi zisizo na rasilimali za kutosha ikilinganishwa na ilizojaliwa Afrika.

Katika safu ya leo, tutaangazia baadhi ya maeneo au mambo tunayopaswa kuyabidili haraka ili kuendelea na kuwawezesha wananchi wetu kufaidi utajiri mwingi waliojaliwa na Mungu. Yafuatayo ni mambo husika:

Ni bahati mbaya kuwa baadhi ya wazito wetu wanaosimamia rasilimali zetu wanaishi maisha sawa na yale ya waliowang’atua, kuwatimua na kuwarithi ama kwa makusudi au kwa kutojua ukiachia mbali kunogewa na utamu wa hali na mifumo hii.

Ni hatari kuwa ni wachache wanaoliona na kulidurusu hili. Kutokana na mfumo huu zandiki, nchi za kiafrika zimekuwa zikipoteza fedha nyingi za walipa kodi kwa matumizi mabaya ya watu wachache badhirifu na fisadi. Ndiyo maana Rais John Pombe Magufuli alipoingia madarakani, alijaribu kuuteketeza mfumo huu pale alipofumua baadhi ya mambo kama vile ajira hewa, wanafunzi hewa na matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma bila kusahau rushwa huku akianzisha ubanaji matumizi yaliyolenga kuwakomboa wanyonge. Hii ndiyo siri ya Tanzania kupiga maendeleo haraka na kuweza kuwa kwenye kundi la nchi za kipato cha kati ndani ya miaka mitano; jambo ambalo halijawahi kufanywa na nchi yoyote.

Leo nitatoa baadhi ya mifano kuhusu namna Afrika inapaswa kuanza kuangalia upya mifumo yake ya uongozi na matumizi yasiyo ya lazima. Hivi, katika karne ya 21, kuna haja ya baadhi ya watendaji wetu kuwa na ma-bodyguard (walinzi) au madereva wakati hawana tishio lolote na kuwatumikia wananchi kama kweli wanawatumikia wananchi au kuweza kufanya kama vile kuendesha magari yao kwenda na kurudi kazini? Hapa Kanada, wazito wengi huendesha magari yao na hawana ma-bodyguard au madereva na kuwahudumia waliowachagua vilivyo.

Je, hawa wetu wanamuogopa nani kama kweli wanawahudumia mabosi wao ambao ni wale wanaowawakilisha? Je, ni fedha kiasi gani tunapoteza na ukale wa mfumo huu wa kikoloni? Wakoloni walihitaji madereva kwa vile hawakujua nchi zetu. Walihitaji ma-bodyguard kwa vile walikuwa wakitunyanyasa na kutunyonya. Ukiondoa viongozi wa kitaifa ambao wanahitaji ulinzi kama huu, hawa wadogo kama vile wakuu wa mikoa, wilaya na wengine wanahitaji kwa mfano madereva na wasaidizi wakati ni watumishi wa kawaida?

Hapa Kanada majaji, na wakuu wengine hujiendesha wenyewe. Chukulia mfano majaji. Kama wanahitaji madereva ili wasichoke, inakuwaje maprofesa wanaowaandaa hawa majaji au madaktari wanaookoa maisha ya watu wanajiendesha na hakuna kinachoharibika?

 

Kimsingi, wenzetu wa nchi za Magharibi walioanzisha mifumo fujaji na nyonyaji kwa makusudi mazima. Mfano, wakuu wa kila idara walilindwa kwa hofu ya kudhuriwa na wale waliokuwa wakiwatawala kimabavu na bila faida.

Hakika, tunapaswa kuanza kutoza kodi viongozi au watumishi wa umma wanaopata mishahara mikubwa na huduma za bure kama hizi za madereva na wasaidizi wasiohitajika. Ukiachia mbali watumishi wa umma, huku si rahisi kuwa na wasichana wa kazi kama ilivyo nyumbani. Hii ni kwa sababu hakuna mwenye uwezo wa kuwalipa mshahara wa kiwango cha chini ambao kila mmoja wa wafanyakazi wa kawaida analipwa. Hivyo, uwepo wa uwezekano wa kuajiri wasichana wa kazi ni njia mojawapo ya kinyonyaji ambayo inapaswa kuangaliwa sambamba na maslahi ya wakubwa yasiyo na faida wala ulazima kwa taifa.

Kwa vile Rais Magufuli anasifika kwa kubana matumizi, anapaswa kuanza kuangalia maeneo ya wasaidizi wake wa ngazi mbalimbali kuanzia wizara, mikoa, wilaya na idara.

Akifanya hivi, ataokoa mabilioni ya fedha ambayo yatamsaidia kufikia azma yake ya kuibadili Tanzania haraka iwezekanavyo.

Mwisho, hebu tujiulize. Ni fedha kiasi gani tunapoteza kama nchi na jamii kwa kuendekeza mfumo huu ambao waliouanzisha na kuuacha walishaachana nao zamani na kujua madhara yake kwa watu wao na mataifa yao? Wakoloni waliweka mfumo huu wa kinyonyaji na kivivu kwa vile walikuwa hawawatumikii wananchi bali kuwatumia na kuwanyonya kwa faida ya mataifa yaliyowatuma. Isitoshe, waliofaidi hizi huduma ni maofisa wa kikoloni tu na si wananchi.

Kama profesa au wakili anaweza kuendesha gari lake, inakuwaje vigumu kwa majaji kufanya hivyo?