Tubadili sheria zetu haraka kuepuka lawama

10Jan 2021
Nkwazi Mhango
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Tubadili sheria zetu haraka kuepuka lawama

KATIKA kufunga mwaka 2020, vyombo vya habari viliripoti kisa funga mwaka ambapo Watanzania wawili walipatikana na hatia ya kujaribu kutorosha almasi zenye uzito wa karati 71,654 zenye thamani ya shilingi bilioni sita na ushee.

Vito hivi vya thamani vilitaifishwa baada ya mahakama kuwakuta na hatia watuhumiwa. Ajabu ya maajabu, badala ya kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi ili kupewa adhabu kali, wahusika waliamriwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi milioni moja! Walilipa faini na kurejea kwenye uhalifu wao.

 Mbali na kisa hiki, vyombo vya habari viliripoti kubanwa na kurejesha chumo la wizi kwa wezi wengine wakubwa baada ya kuingia makubaliano na mwendesha mashtaka wa serikali.

Kama nchi tunataka kutenda haki na kunufaika na mali zetu tulizopewa na Mungu, shurti tufute sheria zinazotoa nafuu na motisha kwa wahalifu. Lazima tuwe na sheria kali kushughulikia ujambazi huu ambao madhara yake ni makubwa kwa wananchi walio wengi. Kimsingi, sheria hizi zinazowapa motisha na nafuu wahalifu zilitungwa na wakoloni ili kujilinda. Kwanini aliyeiba kuku afungwe badala ya kurejesha kuku aliyemwiba? Bunge linapaswa kuliangalia hili kwa makini kama kweli wanawawakilisha Watanzania tena maskini.

Naamini Rais John Magufuli atasoma makala hii kama si yeye, basi washauri wake wenye mapenzi mema na nchi yetu. Hivyo, watalifanyia kazi haraka kama ilivyokuwa utoroshaji madini kwa kuzungushia wigo machimbo ya tanzanite Mirerani na kuonyesha ufanisi wa hali ya juu. Kama kweli kutorosha madini ya mabilioni kama haya adhabu yake ni kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini, kwanini yeyote mwenye akili timamu asijaribu kamari hii inayolipa kirahisi na bila hatari kubwa yoyote?

Kama serikali haitakata rufani na kuwabadilishia mashtaka wahusika kwenda kwenye uhujumu uchumi, itajenga picha kuwa wahusika ni mawakala wa wakubwa wasiotaka wafungwe ili mwishowe wasimwage mtama kwenye kuku wengi. Hii inanikumbusha kesi moja maarufu iliyomhusisha mwizi mmoja toka India iliyohusisha wizi wa mabilioni ya fedha kwa kutumia mashamba yasiyoendelezwa ya mkonge.

Wizi huu ulipogundulika, wakubwa waliokuwa wakinufaika nao, walimfukuza nchini mhusika na taifa likapoteza mabilioni ya fedha.

Kama nilivyogusia hapo juu, nyingi ya sheria tunazotumia kwenye nchi za Kiafrika zilitungwa na wakoloni ili kurahisisha na kuwezesha ukoloni, unyonyaji na wizi kwao. Katika kufanikisha hili, wakoloni walianzisha makosa yanayojulikana kama white-collar crimes au jinai inayotendwa kwa kutumia kalamu.

Na kinachoendelea ni hiki ambapo wezi wengi wa kutumia kalamu ima hutozwa faini au kufungwa vifungo vifupi. Jinai hii, mara nyingi, hutendwa na watumishi wa umma, watawala, matapeli, wafanyabiashara na wengine wa kada hizi. Katika kuhalalisha jinai hii ya kimfumo, ukoloni ulikuja na msemo usemao kuwa the pen is mightier than a sword; yaani kalamu ni bora kuliko upanga. Hata madhara yatokanayo na kalamu kiuchumi ni makubwa kwa nchi na watu wake kuliko ya upanga. Mfano, fedha zinazoibiwa na majambazi kwa kutumia silaha ni kidogo kulinganisha na zinazoibiwa kwa kalamu. Na kutokana na kuacha sheria hizi bila kurekebishwa, wapo wanaosoma siyo kutumikia wala kusaidia taifa bali kutumia kalamu au elimu kulihujumu kama ambavyo Afrika imeshuhudia tangu kupata uhuru wa bendera ambao haukuleta nafuu kwa watu wetu.

Katika mambo ambayo safu hii imekuwa ikipigia kelele ni mfumo mzima wa uendeshaji nchi zetu za kiafrika. Mfano, katika nchi zilizotutawala, huwezi ukaishi bila kuelewa kipato chako ni kiasi gani na kinatokana na nini. Lakini kwa upande wa Afrika, mtu analala maskini anaamka tajiri.

Mamlaka hazimhoji au kumkamata na kumtaka aeleze alivyopata utajiri wake! Hapa Kanada, ikitokea, majirani wataripoti kwa serikali ambayo itakukamata wewe na mali zako hadi utakapotoa maelezo yanayoingia akilini. Kwa namna hii, hapa wizi hauna tija wala hakuna motisha kwa watu kuibia wenzao au serikali. Wanaogopa watakamatwa. Je hali ikoje kwetu? Wapo watu tunaowajua kwa sura na majina waliotajirika kwa kuibia nchi. Badala ya kuwakamata tunawanyenyekea na kuwaendekeza. Leo sitaongelea hili sana. Nitalidurusu kwenye makala zijazo nitakapotoa ushauri wa nini kifanyike kwa wafanyakazi na waliokuwa wafanyakazi wa baadhi ya idara za serikali ambao walitumia fursa zao kuliibia taifa wakastaafu na kuendelea kutumbua ukwasi wa wizi.