Tucheze mpira badala ya kupenda kulalamika

15Feb 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tucheze mpira badala ya kupenda kulalamika

MBALI na kutoa adhabu mbalimbali kwa wachezaji, makocha na waamuzi, Kamati ya Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, imewatia hatiani wasemaji wa klabu kubwa mbili za Simba na Yanga.

Hao ni Haji Manara wa Simba na Antonio Nugaz wa Yanga. Hawa wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwenye kikao chao kilichokaa hivi karibuni, Kamati hiyo inawatuhumu wasemaji hao kwa madai wamekuwa wakishutumu na kutoa matamshi yenye kukashifu na kudhalilisha viongozi Chapa ya Ligi na Taasisi kwa ujumla kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa vipindi tofauti tofauti.

Mkumbo wa kupelekwa huko kwa makosa kama hayo, pia yamewakumba makocha wawili, Luc Aymael wa Yanga na Thierry Hitimana wa Namungo.

Binafsi niipongeze Kamati hiyo kwa kuamua kuwapeleka makocha na wasemaji hayo kwenye Kamati nyingine ili kama wana makosa basi waadhibiwe ili iwe fundisho kwa wengine.

Haiwezekani viongozi nao wawe ni watu wa kulalamika lalamika kama vile mashabiki.

Mimi ninavyojua ni kuwa kama timu haikufanyiwa haki, viongozi wanajua nini cha kufanya. Ni kuandika barua rasmi ya kulalamikia kile unachoona kuwa hakikuwa sawa na kwa miaka mingi ndivyo ilivyokuwa ikifanywa.

Kwa miaka ya karibuni kumekuwa na baadhi ya viongozi wamekuwa wakiishutumu waziwazi TFF, waamuzi au Bodi ya Ligi tena bila ushahidi, halafu hawaandiki barua ya malalamiko, badala yake wao wanakuwa wanatumia zaidi vyombo vya habari kuwasilisha wanachokiona.

Nadhani nia yao ni kuwasilisha ujumbe kwa wanachama na mashabiki wao ambao nao wanakichukua kama kilivyo na kuanza kusambaza kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuzidisha mlolongo wa mlalamiko na mihemko.

Kwa siku za karibuni kwenye Ligi Kuu kumekuwa na tabia ya makocha na viongozi kulalamika sana, mara timu fulani inabebwa, au tunaonewa, wengine wanakwenda mbali zaidi wanatuhumu kuwa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo kumepuliziwa dawa, au kuna harufu kali.

Malalamiko yote haya mimi nadhani kama kweli yapo ilibidi yawasilishwe kimaandishi, ili utafutwe ushahidi, au hata kama mlalamikaji akipeleka ushahidi usio na shaka ni sawa, kuliko kulalamika au kutuhumu watu kwa hisia tu.

Mfano kama tuhuma za kupulizia dawa kwenye vyumba vya kuvalia wachezaji ilikuwa ni suala jepesi tu.

Kocha yoyote au kiongozi anayetaka kuliongelea suala hilo, awe amefuatana na daktari yoyote ambaye ameingia kwenye chumba hicho na kugundua kuwa kuna harufu isiyo ya kawaida na atuambie ni harufu ya dawa gani, huwa inatumika kwa ugonjwa gani, na anadhani kupulizwa kwenye vyumba vya wachezaji lengo ni nini, ina athali gani kwa wachezaji na binadamu kwa ujumla.

Hapo ndipo uchunguzi unapoweza kufanyika ili kubaini jambo hilo. Ikumbukwe uchunguzi ni suala linalohitaji muda na pesa, hivyo haiwezekani tu mtu asiye na utaalamu aseme kuna harufu haielewiki, basi moja kwa moja uchunguzi ufanyike.

Kuhusu waamuzi nadhani tayari suala hili limeshaanza kushughulikiwa, kwani tayari baadhi wameshaanza kukutana na rungu.

Ifike wakati viongozi na makocha wawatayarishe wachezaji kucheza soka, badala ya kuonekana kulalamika kila kukicha kuja na staili mpya, hii inaleta sintofahamu na chuki kwa mashabiki, badala ya upendo na amani.

Haiwezekani TFF, Bodi ya Ligi, waamuzi wako sahihi timu yao inaposhinda tu, lakini ikifungwa basi inageuka kuwa haifai, haielewiki na inawahujumu.

Itafika wakati wakawaambukiza hata wachezaji ambao wakipoteza mechi badala ya kuangalia mapungufu yao, wao wataona ni kama wamehijumiwa tu.

Hakuna timu yoyote duniani ambayo haifungwi.

Hata Barcelona na Real Madrid zinafungwa, tena na timu za kawaida, sasa iweze Simba au Yanga zikifungwa inakuwa nongwa, kila mmoja anaonekana mbaya?