Tuimarishe usalama kwa maboresho ya Sungusungu

21Dec 2018
Elizaberth Zaya
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tuimarishe usalama kwa maboresho ya Sungusungu

KATIKA maeneo mengi ya jiji letu la Dar es Salaam, hivi sasa wamejiimarisha kupitia vikundi vya ulinzi, maarufu kama Sungusungu.

Vikundi hivi ni kweli vina maana kubwa sana katika mfumo mzima wa utendaji wao, kwani kuna baadhi ya maeneo wahalifu ndani ya jamii kwa maana ya vibaka, wezi na wakabaji wanasumbua sana.

Kila eneo wana namna ya kero zao wanazozijua kuhusiana na dhana nzima ya uhalifu unaochukua sura ya wizi. Yapo maeneo ambayo kuna njia na mapito ya vichochoroni mjini hapa, ambako ni hatari kwa usalama wa wapitaji.

Wakazi wengi na hasa kinamama, ni kwamba wamekuwa wakiporwa katika namna ya kukabwa na unyang’anyi wa mtindo tofauti. Lengo kubwa katika hilo, huwa wanawania simu ambazo ndizo bidhaa wanayolenga.

Zamani vibaka hao walikuwa na tabia ya kuwania saa za watu, katika zama hizo simu zilikuwa bidhaa maarufu katika jumuiya za watu na zina thamani kubwa, kabla ya kunaguka bei zake.

Mtindo mwingine ni kwamba wezi hao wanazurura na fimbo ndefu zilizowekwa gundi, wanachana nyavu za madirisha na kujaribu kuzinasa simu na chochote cha thamani ndani ya nyumba za wakazi.

Hapo sipendi kuingilia sana ya majambazi, hawa ni wenye athari na matumizi makubwa ya silaha za hatari na za kisasa kama vile bunduki, ingawaje vibaka nao katika unyang’anyi wao wanatumia visu, bisibisi na mapanga.

Katika matukio mengi hawajawaacha watu salama, hasa kunapokuwapo kurupushani na anayeporwa, au wakati mwingine ni mbinu za kuimdhibiti anayeibiwa.

Ndipo katika mazingira kama hayo, umuhimu wa Sungusungu katika kamati za ulinzi na usalama zilizoko kimkoa, hadi ngazi za mitaa na kata zina umuhimu mkubwa.

Bado ninamkumbuka sana aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Ahaji Omar Mahita, katika zama za uongozi wake, yalipotokea matukio ya ujambazi mfululizo jijini Dar es Salaam, ‘aliwaka’ na kuita kikao cha polisi, katika Bwalo Kuu la Oysterbay, akihoji kwa msamiati wa nadharia ya kiaskari:”Bit’ system’ na ‘patrol system’ zimeenda wapi?”

Nililazimika kuhoji maana yake kwa askari, walionifuza kuwa ni ulinzi wa polisi kuweka kituo mahali fulani kwa muda na ‘patrol’ unarejea kuzunguka kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Tunajua kwamba mifumo yote ya ulinzi kama vile Mgambo, Sungusungu na walinzi binafsi wanaopatikana sasa kutoka kampuni mbalimbali ni walinzi wa ziada nje ya majeshi rasmi, ambayo ni Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na Magereza.

Hivyo, sungusungu ambao ni walinzi wa ziada katika majukumu ya polisi, wanapaswa kunolewa wakajipanga vyema kupambana na vibaka kupitia mbinu hizi kuu mbili za polisi kutokana na somo la Mzee Mahita.

Tunajua vikundi hivi vikiimarishwa kitaaluma na kiuwezo vinakuwa na nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa maboresho ya ulinzi katika jamii yetu.

Nimalize kwa kunena Sungusungu ni muhimu sana katika jamii yetu kwa sababu, ni walinzi wetu wanaoishi katika eneo letu na wanawajua vibaka wetu mitaani na namna ya kupambana nao.

Pia, hao ni msaada wa karibu kwa polisi walioko katika doria ndani ya maeneo yao.