Tukichekea wanasiasa tutavuna mabua

03Jan 2021
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Tukichekea wanasiasa tutavuna mabua

MUUZA jeneza siku zote huchukia kifo, lakini hukasirika majeneza yake yasipopata soko.

Hujiuliza kulikoni, na huombea apate wateja ili apate riziki, kwa sababu asiyefanya kazi na asile na asiyekula afe.

Mganga wa kienyeji siku zote huchukia kifo na magonjwa, lakini hukasirika sana asipopata mgonjwa, kwa sababu atakosa riziki yake. Naye atajiuliza kulikoni asipate wateja, na huishia kuichukia hospitali.

Na huyu huenda mbali zaidi, akiona amekosa wateja atafanya juu chini awatengeneze, kwa kuwaroga, ili wamtafute wampelekee riziki. Waswahili husema mbwa anakula miguuni kwake, huku mbuzi akila kwa kadri ya urefu wa kamba yake.

Nchi ikiwa na usalama wa raia na mali zao pia, yawezekana polisi wakakosa kazi, na wakikosa kazi watakosa riziki. Sasa wakikosa riziki itakuwaje, kwa sababu asiyefanya kazi hatakula na asipokula atakufa.

Polisi wanachukia sana uhalifu, wanachukia wanaohatarisha usalama wa raia na mali zao, lakini wakikosekana watu hawa wanaoitwa wahalifu, ina maana polisi hawatafanya kazi.

Magereza ambao husubiri kupokea wahalifu kutoka Polisi, nao hawapendi kusikia nchi ina wahalifu, kwa kuwa wanawasumbua kuwahifadhi wakiwa mahabusu au magerezani, lakini wasipokuwapo, askari Magereza watafanya kazi gani? Je, wasipofanya kazi itakuwaje?

Halikadhalika wauza dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa Ukimwi, nao hawapendi kuona watu wanapoteza maisha yao kwa ngono zembe, lakini itakuwaje kusipokuwa na waathirika wa Ukimwi, dawa hizo atauziwa nani?

Hivi mnadhani wauza barakoa walifurahi Uviko-19 ulipotoweka nchini ghafla? Fikiria barakoa la kitenge utalivalia wapi kama korona haipo? Nawe unayelishona utamuuzia nani?

Kwa hiyo haya mambo yapo tu na yanategemeana kwa kiasi fulani, tutayachukia, lakini tutayapenda pia. Hatupendi watu wapoteze maisha, lakini kumbe wakipoteza maisha pia ni fursa kwa wengine. Hebu fikiria wachimba makaburi!

Ndiyo sababu wanasiasa hata siku moja hawatakubali wananchi wa kawaida waondokane na ujinga kwa asilimia 100, kwa sababu kwa kufanya hivyo, watagundua njama zao chafu za kujipatia maslahi kupitia migongo yao.

Wanasiasa watapanda majukwaa kudanganya wananchi; tutakufanyieni hiki na kile ili kukuondoleeni kero na adha hizi na zile, lakini hatimaye hakitafanyika kabisa au nusu, ili wananchi waendelee kuogelea kwenye dimbwi la matatizo.

Uogeleaji huo ni wananchi kuendelea kuishi wakitegemea ahadi hewa, huku wanasiasa nao wakitegemea kura ili waendelee kula na kushiba migongoni mwa wananchi.

Kulithibitisha hili, ni kufuatilia kampeni na kusikiliza ahadi na kisha utekelezaji wa ahadi, ndipo utabaini kwamba kumbe wanafurahia raia kuumia ili waendelee kuula.

Sikiliza mijadala na maswali bungeni, hutakosa kusikia maswali ya barabara ile, jengo lile, mioundombinu ile, ziwa lile, mto ule na bwawa lile. Ili mradi ni mambo yale yale yataulizwa vile vile katika kila kikao na mkutano na kujibiwa vile vile na kupongezana na siku kusonga mbele.

Maswali na majibu ya wanasiasa wao kwa wao au kutoka kwa wananchi au kwa wanahabari, ni fursa ya kuaminiwa kushughulikia matatizo na ikiisha mitano, inatafutwa mitano mingine na maisha yanaendelea vile vile.

Inawezekana miaka mitano iliyopita, tuliwasikia wale wale wakitwambia yale yale, tukawachagua vile vile na maisha ya miaka mingine mitano yatakuwa yale yale na tutaendelea kuishi vile vile, tukiahidiwa ahadi zile zile. Muhimu ni amani na utulivu wetu tu.

Utakutana na mwanasiasa ambaye wakati wa uchaguzi hakuwa hivi, alikuwa mpole na mpiga magoti, mgalagala chini, akiomba kura yako ili akale, leo atataka wewe ndio umpigie magoti na ugalegale chini, ili akusikilize shida yako, akikusaidia haya, asipokusaidia shukuru Mungu pia.

Pengine miaka mitano hii ijayo, utakutana na mwanasiasa jeuri, atakayediriki kukushikia mjeledi, ili ukibiashana naye akulaze chini na kukucharaza, hata kama una mzuzu au sharubu. Lazima atataka akuonyeshe yeye ni nani na wewe ujitambue ni nani mbele yake...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com