Tukijipanga, kwenda AFCON inawezekana

23Apr 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tukijipanga, kwenda AFCON inawezekana

NI wiki ambayo Watanzania walishuhudia Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), ikipangwa kwenye Kundi F kuelekea kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuchezwa mwakani nchini Ivory Coast.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilichezesha droo ya michuano hiyo na Tanzania ikaangukia kwenye kundi ambalo lina timu za Algeria, Uganda na Niger.

Mara tu baada ya droo hiyo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema kundi hilo ni moja kati ya makundi magumu, lakini akasema wako tayari kwa michuano hiyo, kikubwa tu akasisitiza uwajibikaji wa pamoja na maandalizi mazuri.

"Algeria ni timu kubwa, Uganda ni timu nzuri ambayo wametuzidi kwenye viwango vya soka, Niger sijui sana habari zao, lakini mechi zitakuwa ngumu, kila mtu sasa ana wajibu kuanzia viongozi, benchi la ufundi na wachezaji ili tufuzu AFCON, kifupi tuko tayari kwa mashindano. Nadhani maandalizi ndiyo kitu kikubwa, tutacheza mechi mbalimbali za kirafiki ili kujiweka sawa," alisema kocha huyo na akaongeza:

"Tofauti ya michuano hii ni kwamba zinafuzu timu mbili za juu kwa hiyo ni faida kwetu, hii ni tofauti na ile ya kufuzu Kombe la Dunia ambapo timu moja tu ndiyo ilikuwa inasonga mbele," alisema Poulsen.

Si yeye tu, hata makocha wengine walitoa maoni yao mbalimbali na nini cha kufanya ili kuiwezesha Tanzania kufuzu fainali hizo. Mmoja wapo alikuwa ni Juma Mwambusi ambaye alikiri ni kundi gumu na kutahadharisha tusidharau wala kubweteka.

"Hakuna timu rahisi, zamani ikiandikwa Niger tunasema haina kiwango, lakini kwa sasa wako vizuri kimiundombinu ya soka na wana wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi yao tofauti na sisi, kwa hiyo ni kundi gumu.
Inahitajika jitihada kubwa kuhakikisha tunaweza kufanya lolote, mimi naamini kwa vijana wetu kama wakiweza kujitambua tunaweza kupita," alisema kocha huyo na kusisitiza.

"Tukiwatumia wachezaji wanaocheza nje ya nchi ambao nimewaona kwenye mechi zilizopita, wanaweza kutusaidia, ligi yetu kwa sasa ina ushindani, lakini tunahitaji mechi za majaribio nyingi, na tucheze na timu za Afrika Kaskazini na mataifa yaliyoendelea kisoka na pia tupate mechi ambazo tukachezee ugenini, siyo kila mechi ya kirafiki tunacheza hapa hapa, haitatusaidia," akasema.

Yote yaliyosemwa hapa yana mchango mkubwa kufanikisha azma ya Tanzania kufuzu fainali hizo kwa mara ya tatu tangu ipate Uhuru. Mwanzo ilikuwa mwaka 1979, na fainali zake zikachezwa 1980 nchini Nigeria, na mara ya pili ni 2019 huko Misri.

Tunatarajia maandalizi yataanza mapema, na kila mmoja awajibike kwenye nafasi yake kama alivyosema Poulsen, na Mwambusi amesisitiza kutoidharau timu yoyote, pia mechi ya kirafiki kwa sasa zikachezwe nje ya nchi. Ni kweli kabisa, kwa miaka ya karibuni hatujaona Stars ikienda kucheza mechi za kirafiki zilizo kwenye kalenda ya FIFA nje ya nchi.

Watanzania sasa tuanze kufanya juhudi za kuhamasisha wachezaji Stars kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa sababu ndiyo moja kati ya vitu vinavyowafelisha.

Stars inaweza kushinda au kutoa sare ugenini, lakini ikafungwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Kama tunataka kwenda Ivory Coast tusikubaliane na hilo.

Halafu maandalizi ya kisayansi yapewe zaidi nafasi kuliko kuundwa kamati za hamasa nyingi ambazo hazijulikani zinafanya kazi gani, badala yake zinaleta mkanganyiko tu usio na maana.

Kikubwa baada ya maandalizi mazuri, kutumia mechi tatu za nyumbani vizuri na kuisaka japo pointi moja ya ugenini kwa timu yoyote ile kati ya hizo. Nina uhakika tunaweza kufuzu AFCON.