Tukijitolea inawezekana kupata walimu wa sayansi

10Mar 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tukijitolea inawezekana kupata walimu wa sayansi

MOJA ya changamoto inayozikabili sekondari za umma ni uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na Hisabati, hali inayosababisha wanafunzi kutofundishwa masomo hayo kwenye baadhi ya shule.

Hata hivyo, serikali imeshaweka wazi kwamba ina kipaumbele wenye ajira za walimu wa masomo hayo kwa kufuata utaratibu wa kutuma vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.

Ni maelekezo ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, katika moja ya mikutano yake na Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa).

Lakini, wakati serikali ikifanya jitihada hizo za kuajiri walimu wa kutosha, kuna haja wazazi wanaowatafuta walimu wa kujitolea wa masomo hayo, wanaosubiri ajira, ili wanafunzi wasiendelee kukosa masomo hayo.

Njia hiyo inaweza kuwasaidia wanafunzi kumudu masomo hayo kuliko kuendelea kusubiri hadi waajiriwe, wakati wapo mitaani bila kazi.

Hilo ni jambo ambalo wazazi na walezi wanaweza kuangalia na kuwa na uwezekano wa kuchangishana chochote kwa ajili ya posho za walimu hao.

Wale ambao wameona umuhimu, tayari wameshaanza kuutumia kwa kuchangishana fedha za posho na kupata walimu wa masomo hayo na sasa wanaendelea na kazi kufundisha watoto wao.

Mfano mmojawapo ni wazazi wa Sekondari za kata za Musoma Vijijini, mkoani Mara, ambao wamekubaliana kila mmoja kuchanga kati ya Sh. 200 hadi Sh. 1,000 kwa ajili ya walimu wa kufundisha watoto wao.

Hatua hii ni nzuri kutokana na ukweli kwamba kwa kawaida mtihani unapoandaliwa huwa ni wa masomo yote hata yale ambayo wanafunzi hawakuyasoma kutokana na uhaba wa walimu.

Kwa maana hiyo hatua iliyochukuliwa na wazazi hao ya kukaa na kuamua kwamba wapate walimu wa kujitolea kwa ajili ya kufundisha watoto wao masomo ya sayansi na Hisabati ni mfano mzuri wa kuigwa.

Walezi na wazazi hao wametimiza wajibu wao badala ya kuendelea kusubiri walimu waajiriwe wakati watoto wao wakikosa masomo hayo, huku wakiwa na uwezo wa kukabili changamoto hiyo.

Walimu hao wa kujitolea wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kufikia uchumi wa viwanda 2025, kwani watakuwa wamesaidia kuandaa wataalamu wa baadaye wakiwao wahandisi wa mitambo.

Hivyo wakati Tanzania ikiwa na walimu wachache wa masomo hayo, wazazi na walezi hawana budi kujiongeza na kuchukua hatua kama za wenzao wa Musoma Vijijini walioamua kuchukua hatua hizo.

Serikali imeshaeleza mipango yake hivyo kumaliza tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi na Hisabati nchini, lakini wakati ikiwa kwenye mkakati huo, ni muhimu jamii kuwa njia mbadala kama hiyo ya kupata walimu wa kujitolea.

Jambo hili linatakiwa kupata baraka za viongozi wa maeneo yenye shule hizo hasa wale ambao ni wabunifu, kuanzia wa serikali za mitaa, madiwani na wabunge na kuhamasisha wananchi ili watambue umuhimu wake.

Mchango wao ni wa muhimu kwa kutambua kuwa nchi imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati, ambao ni wa viwanda, hivyo umuhimu wa masomo hayo hauwezi kuepukwa, kwa sababu wataalamu zaidi wanahitajika.

Waliotambua umuhimu wote wameanza kwa kutafuta walimu wa kujitolea, ambao hadi sasa wanaendelea na kazi, kwani sasa ni wakati wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi.

Hao ndiyo watakaoweza kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini, kwa hiyo hatua hiyo itamlazimisha mwanafunzi kusoma kwa bidii, ili kuhakikisha anafaulu masomo hayo ingawa tatizo lililopo ni uhaba wa walimu.

Wanafunzi kuendelelea kukosa masomo hayo kunaweza kuwafanya wayaone ni magumu na kukimbilia mengine, na kumbe kama wangefundishwa kikamilifu wangeweza kuyamudu.

Kwa maana hiyo umuhimu wa kuwa na walimu wa kujitolea upo palepale, kwamba wazazi na walezi wanatakiwa kujiongeza na kuweka mkakati wa kupata walimu wa kujitolea kwa ajili ya kuwafundisha na kuwaendeleza watoto wao.