Tukiuchekea ukeketaji, kinamama tutateketea

20Dec 2016
Mariam Hassan
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tukiuchekea ukeketaji, kinamama tutateketea

TATIZO la ukeketaji wa wanawake, jambo linalofanywa bila ridhaa yao, ni sugu na athari zake ni mahsusi kwa watoto wa kike.

Ni tendo linalofupisha ndoto zao kwa kuwatia kasoro katika maumbile ya kijinsia na hata vifo, hasa mtu anapopoteza damu nyingi.

Kimsingi, ni ukatili mkubwa ambao hata hivyo unaendekezwa na jamii yenyewe katika baadhi ya maeneo, kwa kuzingatia mila na desturi.

Ukeketaji wa wanawake bila ya ridhaa yao ni tabia iliyodumu kwa karne nyingi, katika katika sehemu mbalimbali duniani.
Licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na serikali, limekuwa likifanyika kwa siri kubwa.

Inadaiwa, suala hilo si la wasichana peke yao, kwani kundi la kinamama waliofikisha umri wa miaka 40 au zaidi nchini, nao wako katika hatari hiyo ya kukeketwa.

Katika uhalisia wa vita hivyo, kinamama wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 19 ndio walioko kwenye hatari zaidi.

Nikuchukulia katika mtazamo mpana, ukeketaji ni tatizo linalotofautiana kutoka eneo moja na nyingine. Kuna namna tofauti inavyoendeshwa na vivyo hivyo, athari zake.

Uchunguzi umebainisha kwamba tangu kuanza vita dhidi ya tabia ya ukeketaji zaidi ya miaka 20 iliyopita, sheria na juhudi zilizopo bado hazijafanikiwa kufuta kabisa tabia hiyo.

Ripoti ya utafiti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumisha Watoto (Unicef), inabainisha mbali na athari inayowakabili wanawake, jamii nayo inaridhia tendo hilo,

Baadhi wanatafsiri jambo hilo katika mtazamo wa imani zaidi, ikichukuliwa katika mtazamo wa mila, desturi na hata dini za baadhi ya makabila.

Miongoni mwa baadhi ya makabila yaliyoathirika nchini ni pamoja na yanayotoka katika mikoa ya Manyara, Mara na Arusha, huku katika ulingo wa kimataifa, nchi ya Somalia inatajwa kuwa miongoni mwa vinara.

Nadharia iliyoko nyuma ya pazia ya dhana ya ukeketaji ni kwamba, suala hilo ni sehemu ya kuondoa mikosi kwa mwanamke na familia zao.

Hata hivyo, katika upande wa pili wa shilingi, mwanamke aliyekeketwa anadaiwa anakosa hamu ya tendo la ndoa, huku akiwa katika mazingira rahisi ya kuambukizwa maradhi ya Ukimwi, iwapo atahudumiwa na ngariba mwenye vifaa vifaa dunia na visivyo salama.

Changamoto kubwa inayojitokeza katika kukomesha tatizo hilo, ni wanawake wenyewe kuwa mstari wa mbele kuwapeleka kwa siri watoto wao kufanyiwa ukeketaji na magariba.

Wiki iliyopita, iliripotiwa kwenye vyombo vya habari kwamba jambo hilo linafanyika kwa siri nchini Uingereza, kupitia kivuli cha sherehe za kinamama.

Nini kifanyike? Mamlaka za dola kitaifa na kimataifa, taasisi zisizo za kiserikali na wanaharakati, wanapaswa kujitahidi kutoa elimu katika kukomesha suala hilo la ukeketaji, ili wanawake wasizidi kuumizwa katika afya na mustakabali mpana wa maisa yao.