Tukoleze maandalizi Serengeti Boys, Mei sio mbali

06Mar 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tukoleze maandalizi Serengeti Boys, Mei sio mbali

HATIMAYE ni miezi miwili tu imebaki kabla ya wawakilishi wetu, Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ hawajaenda nchini Gabon kushiriki kwa mara ya kwanza fainali za Afrika.

Yapo maandalizi yanayoendelea ya timu hii kwa ajili ya mashindano haya yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Tayari hivi karibuni imeundwa kamati maalum kwa ajili ya kuisaidia timu hii kwenye maandalizi yake kuelekea Gabon, kamati hiyo inahusisha watu mbalimbali.

Ili kufanya vizuri kwenye michuano hii inayoanza mwezi Mei mwaka huu, yanahitajika maandalizi ya nguvu, maandalizi ya ndani na nje kwa wachezaji wetu.

Kuundwa kamati tu haitoshi, bado juhudi za hali ya juu zinahitajika katika kuhakikisha timu yetu inapata maandalizi ya asilimia 100 kabla ya kuanza kwa michuano hii ya Afrika kwa vijana.

Bila kuwa na maandalizi ya uhakika kwa vijana wetu, haitashangaza tukiondolewa mapema kwenye michuano hii.

Si wachezaji, makocha wala mashabiki wanaotaka kuona Serengeti Boys ikienda Gabon ‘kushiriki’ tu michuano hii, wanataka kuona timu ikipambana na kuiletea Tanzania sifa huku ikiwa mara yake ya kwanza kushiriki michuano hiyo.

Katika maandalizi ya timu hii, suala hili lisiachwe kwa TFF peka yake au Serikali peke yake, kila mdau na shabiki wa soka anapaswa kushiriki kikamilifu maandalizi ya timu hii.

Ikumbukwe mafanikio yoyote ya timu hii hayatakuwa mafanikio ya TFF au Serikali peke yake, yatakuwa mafanikio ya taifa zima.

Tushirikiane kuiandaa timu hii, na kama itafanya vizuri Gabon basi kwa pamoja tutakuwa tumechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio watakayokuwa wamefikia.

Miezi miwili iliyobaki tuitumie vizuri kwa kuhakikisha juhudi zinaongezwa katika maandalizi ya timu yetu hii kuelekea nchini Gabon.

Mikakati iwekwe na TFF kuwawezesha makocha wa timu hii na wachezaji kufanya maandalizi katika hali ya utulivu kwa kuhakikisha kila vitu vyote muhimu vinapatikana katika maandalizi yao.

Hakuna shaka uwezo wa Serengeti Boys kufanya vizuri kwenye michuano hii upo, imejionyesha timu hii inauwezo mkubwa hasa kutokana na safari yao kuelekea kwenye fainali hizi za Afrika.

Ilifanikiwa kuzitoa timu ngumu kama Afrika Kusini na Congo Brazzavile kabla ya kupata tiketi ya kuelekea Gabon.

Bila shaka yaliyoikuta Congo Brazzavile ya kuchezesha vijeba hayatatukuta Tanzania, TFF iangalie kwa karibu suala la umri kwa wachezaji wetu ili tuelekee kwenye michuano hii tukiwa na wachezaji wanaostahili kushiriki michuano hii.

Ni wazi vijana walipambana katika mchakato wa kusaka tiketi ya kushiriki michuano hii, hivyo kusitokee sababu zozote zisizo za lazima zitakazo athiri ushiriki wa timu yetu kwenye michuano hii.

Aidha, pia mafanikio ya Serengeti Boys kushiriki michuano hii iwe chachu na timu nyingine za Taifa hapa nchini kuanzia ile ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20, miaka 15 mpaka ile timu yetu kubwa ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuhakikisha inasaka tiketi ya kushiriki michuano mikubwa inayoandaliwa na CAF na ile ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kukiwa na mipango thabiti kama iliyokuwa imewekwa kwa Serengeti Boys, ni wazi timu nyingine za Taifa zinaweza zikafanikiwa kufuzu kushiriki michuano mikubwa Afrika na ile ya Dunia.